Monday, 31 October 2011

UK yataka Tanzania itambue haki za mashoga  
 
 
PERTH, Australia UINGEREZA imetoa shinikizo la kutambua haki za mashoga kwa nchi zinazoendelea na kutishia kusitisha misaada yake kwa nchi zinazokiuka agizo hilo. Waziri Mkuu David Cameron amesema Uingereza ina mpango ya kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria zake hazitambui ndoa za jinsia moja na mashoga.

"Nimeshawajulisha baadhi ya wakuu wa nchi kuhusu suala hilo kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Perth, Australia," alisema Cameron kupitia BBC.Nchi 41 kati ya nchi 54 wanachama wa Jumuiya ya Madola, zina sheria zinazopinga ndoa za jinsia moja.

Suala la haki za binadamu ni moja ya agenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano huo ambao rais Kikwete pia alihudhuria. Cameron alisema: "Tunasema hii ni moja ya vitu vinavyoongoza sera yetu ya misaada kwa mataifa mbalimbali na tayari tumeanza kuitekeleza katika maeneo kadhaa," alisema.

Aliendelea: "Nchi zote zinazopata misaada kutoka kwetu (Uingereza), zinapaswa kukubaliana kikamilifu na sera hii ya haki za binadamu," alisema. Cameron alisema ameshazungumza na nchi mbalimbali za Afrika kuhusu suala hilo na utekelezaji wake utafanywa na Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo, William Hague.
Kukomesha vizuizi vya ndoa ya jinsia moja, ilikuwa moja ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya ndani ya matarajio ya baadaye ya Jumuiya za Madola. Katika mkakati huo, Uingereza imetishia kusitisha sehemu ya misaada ya bajeti kuu kwa nchi zisizokubaliana na msimamo huo lakini imeahidi kwamba haitaondoa bajeti yote.

Nchi ya Malawi imeshaathirika na mpango huo wa Uingereza kwa sehemu ya misaada yake kusitishwa kutokana na misimamo yake kuhusu haki za mashoga. Nchi ambazo huenda zikafuatia hivi karibuni ni Uganda na Ghana. Cameron ameieleza BBC kuwa nchi zinazopokea misaada kutoka Uingereza zinapaswa kuachana na sheria kandamizi. Lakini akaeleza kuwa ingawa sio rahisi nchi kubadilika ghafla, ni bora zikaanza sasa mchakato wa mabadiliko hayo kuliko kuendelea kubweteka.

"Hili ni suala ambalo tunaendelea kulisukuma ili lifanikiwe na tumejiandaa kuwekeza hela pia katika kuhakikisha tunafanikiwa lakini ninashaka kwamba hatuwezi kutegemea mabadiliko hayo kuja mara moja," alisema. Mjadala mzito ulioibuka katika bunge la Uganda mwaka 2009 kuhusu ndoa za mashoga, ni sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ya Uingereza.

Mwaka huu mwanaharakati wa kutetea haki za mashoga nchini Uganda David Kato alipigwa hadi kifo kutokana na kuongoza kampeni hizo. Bunge la Nigeria sasa linaendelea kujadili Muswada wa kuzuia ndoa ya jinsia moja ikiwamo kuweka adhabu kali kwa watu wanaosadia au kuhamishwa kufungwa kwa ndoa hiyo.

Zanzibar yazindua teknolojia baharini  
 
Tausi Mbowe, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imezindua mfumo mpya wa kuongoza vyombo vya usafiri majini utakaotumia kompyuta kwa lengo la kuvifuatilia vikiwa njiani.

Teknolojia hiyo ya Digitali inayofanana na ile ya ndege, inaingia sokoni kukabiliana na ajali za meli zisizokuwa za lazima.Akizindua teknolojia hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, alisema mfumo huyo utasaidia kuwabana wafanyabiashara wote wasio waaminifu ambao wanaweka mbele maslahi yao na kusahau utu.

Hivi karibuni zaidi ya watu 1,000 wanasadikiwa kupoteza maisha kufutia ajali ya meli ya Mv Spice Islands, baada ya kuzama katika mkondo wa Nungwi kufutia boti hiyo kujaza mizigo kupita uwezo wake.

Hata hivyo, Dk Shein aliwataka wafanyakazi wa vyombo vya baharini kutumia sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika, badala ya kutoa huduma hiyo kwa matakwa yao na kuwasumbua abiria.

Dk Shein alisema kufanya kazi katika vyombo hivyo vya baharini bila ya kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na mamlaka husika, inaharibu biashara na kuondoa imani kwa wasafiri kwani nia ya wamiliki wa vyombo hivyo ni kutoa huduma kwa wananchi tofauti na watoa huduma wanavyofanya.
Rais Shein alisema siku zote abiria wanatakiwa kupewa huduma bora ambazo zitawavutia katika safari zao, siyo bugudha wanazopewa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

Aliitaka wizara na taasisi husika kusimamia vizuri taratibu na sheria zilizowekwa katika kuhakikisha wanaoingia baharini wanafuata taratibu, siyo kila mtu anaingia eneo hilo na kusababisha usumbufu kwa wasafiri huku akisisitiza kuwapo nidhamu ya baharini.

Kuelekea kuundwa Katiba Mpya, mchakato wapamba moto


 
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Sheria na Utawala Mhe. Pindi Chana
 

 

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala Mhe. Tundu Lisu akichangia leo wakati kamati hiyo ilipokutana Dar es Salaam kujadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.
 
Mjumbe wa Kamati ya Sheria, Katiba Utawala Mhe. Andrew Chenge akitoa angalizo na ushauri wa kitaalamu wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011
Mhe. Ole Konnay, Mjumbe wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala akitoa ushauri wake wakati wa majadala.
 
Wajumbe wa Kamati
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala ikiwa imekaa leo katika Ofisi ndogo ya Bunge Dar es Salaam.
 
 

UZINDUZI WA TAWI LA PBZ PEMBA



Rais Dk. Shein azindua tawi jipya la Benki ya PBZ chakechake Pemba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na wananchi wa chake chake kisiwani pemba wakati wa uzinduzi wa tawi la Benki ya PBZ,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Tawi la Benki ya PBZ huko Chake chake Pemba,(kushoto) Mkurugenzi wa PBZ Juma Amour na (kulia) Kaimu Waziri wa Fedha Mhe,Mwinyihaji Makame





Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akitoa pesa kutoka huduma ya ATM mara baada ya kulizindua Tawi jipya la PBZ humo chake chake Pemba



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akionyesha pesa alizotoa kupitia mtandao wa ATM





Baadhi ya waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la bank ya Watu wa Zanzibar PBZ Wilaya ya chake chake Pemba.

Sunday, 30 October 2011

Barabara zilizofurika maji ya mvua Zanzibar


Waendesha magari wakipita kwa taabu katikazilizofurika maji ya mvua barabara  katika moja ya mitaa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali Zanzibar jana.
Marais wastaafu Z`bar kupewa Ofisi za maisha
 
 
Wawakilishi wapinga na kutoa masharti mazito
Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais (Ikulu) Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini
Muswada wa kuweka sheria mpya ya kuwalipa pensheni wajane na watoto wa marais wastaafu umekwama kuwasilishwa barazani baada ya wajumbe kudai haujazingatia maslahi ya taifa.
Muswada huo ulikuwa uwasilishwe na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais (Ikulu) Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, ambao ungewanufaisha viongozi wa kisiasa wa kitaifa Zanzibar.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini muswada huo umepingwa mara mbili na wajumbe katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo na katika kamati ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wa kitaifa chini ya Mwenyekiti wake, Hamza Hassan Juma.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Hamza amethibitisha kuwa kamati yake imetoa mapendekezo ya kutaka ufanyiwe marekebisho makubwa kabla ya serikali kuwasilisha tena katika baraza hilo Mwakani.
Aliyataja miongoni mwa mapendekezo hayo kuwa ni viongozi wastaafu wasipewe Ofisi na Serikali, pamoja na wasaidizi wasiopungua 12 ili kuepusha kuwabebesha mzigo wananchi wa Zanzibar.
Aidha, wajumbe hao wametaka wajane wa marais wastaafu na watoto wao waondolewe katika utaratibu mpya wa kuanza kulipwa pensheni kila mwezi pamoja na washauri wa rais ambao wameelezwa sio viongozi wa kisiasa.
Kamati hiyo imetoa mapendekezo mengine kuwa wajumbe wa baraza la wawakilishi pia watambuliwe na sheria hiyo kama viongozi wa kisiasa badala ya sheria hiyo kuwatenga na kuwatambua viongozi wachache wa kitaifa.
Aidha kamati hiyo imesema kiwango kilichopendekezwa na Serikali kuwa mjane wa rais alipwe pensheni kila mwezi sawa na mshahara aliyokuwa akilipwa rais ni kikubwa na hakilingani na hali halisi ya uchumi wa Zanzibar.
Hamza alisema kwamba viongozi wengi wana watoto kati ya 10 hadi 15 hivyo wameitaka Serikali iweke idadi maalumu ya watoto ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha za umma ya kuwalipa pensheni sawa na kima cha chini cha mshahara kila mwezi pale wazazi wao wanapofariki wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
Hata hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamuwa kuitisha semina kwa wajumbe iliyofanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View mwishoni mwa wiki kujadili muswada huo lakini wajumbe waliendelea kuupinga muswada huo na kulazimika kushindwa kuwasilishwa katika mkutano wa tano wa Baraza hilo.
Upande wake Mwakilishi wa jimbo la Mkwajuni, Mbarouk Mussa Mtando alisema kabla ya wajane wa marais kuanza kulipwa pensheni sawa na mshahara anaolipwa rais aliyopo madarakani lazima kiwango chake kijulikane ili waweze kutathmini kabla ya kuamua kupitisha sheria hiyo.
Alisema kwamba kujulikana kwa kiwango cha mshahara wa rais wa Zanzibar kutawafanya wajumbe kutathmini kiwango cha fedha na hali ya uchumi wa Zanzibar.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya fedha na uchumi ya Baraza la Wawakilishi, Ali Omar Shehe, alisema muswada huo wanaukataa kwa sababu haujazingatia maslahi ya taifa na utawabebesha mzigo mkubwa wananchi wake.
Alisema kwamba kitendo cha Serikali kupendekeza wajane na watoto marais wastaafu kuanza kulipwa pensheni pale waume zao wanapofariki sawa na kuwabagua wajane wengine katika jamii.
Shehe alisema iwapo Serikali watalazimisha kupitisha bila ya kufanyika marekebisho hayo lolote litakalotokea ndiyo itakayowajibika.
Akizungumza katika semina hiyo Spika Pandu Amer kificho alisema kwamba kuna mambo ndani ya sheria hiyo yanahitajika kuangaliwa kwa umakini kabla ya kupitishwa na kuwa sheria.
Alitoa mfano yeye binafsi ana watoto 19 kati ya hao 12 wapo chini ya umri wa miaka 18 na kushauri suala la watoto wa viongozi wa kitaifa kuingizwa katika utaratibu wa kulipwa pesheni wazazi wao wanapofariki kuangaliwa kwa umakini.
Kwa mujibu wa muswada huo kifungu cha 10(1)(2) kimesema iwapo rais mstaafu atafariki mjane wake atastahili kulipwa penmsheni kila mwezi swa na mshaara wa rais aliyepo mdarakani wakati watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 watalipwa kima cha chini cha mshahara kila mwezi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Kikombe cha `Babu` chazidi kupoteza umaarufu

 
Wabunge wataka kipigwe `stop`
Mchungaji Ambilikile Masapila `Babu`
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, wameitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kumfungia Mchungaji Ambilikile Masapila 'Babu', kutoa huduma kwa madai kwamba, amekuwa akisababisha vifo vingi tangu alipotangaza dawa yake.
Ushauri huo ulitolewa na wajumbe hao jijini Dar es Salaam, wakati kamati hiyo ilipotembelea TFDA, ambako walitumia fursa hiyo kujionea utendaji kazi wa maabara pamoja na maeneo mengine muhimu ya mamlaka hiyo.
Walidai 'Babu' alipotangaza kutibu magonjwa sugu matano, kikiwamo kisukari na Ukimwi, wagonjwa wengi walishawishika na kutoka hospitalini kwenda kupata kikombe chake.
Walisema matokeo yake vifo vingi vimetokea, hivyo wakaihoji TFDA sababu ya kutomsimamisha 'Babu' kuendelea kutoa huduma yake.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge
wa Chaani (CCM), Ali Juma Haji, ambaye alisema 'Babu' amekuwa akiwaumiza watu, hivyo akashauri kusimamishwa kwa huduma yake ili kuondokana na tatizo hilo.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zarina Madabida.
Alisema 'Babu' alitangaza kutibu magonjwa makubwa na dunia nzima ilishamjua anayatibu, lakini tayari watu wengi wamekwishakufa kwa kuacha dawa za hospitali.
Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vipodozi, Mitangu Fimbo, alisema TFDA haitoi vibali vya dawa kama anazotumia 'Babu' kutibu.
Fimbo alisema vibali vya dawa za aina hiyo hutolewa na Baraza la Dawa Asilia.
Alisema kazi ya kumchunguza 'Babu' hadi kusimamishwa inaweza kuchukua mwaka mmoja.
Fimbo alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini tatizo hilo na kwamba, katika uchunguzi huo wanashirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia.
Alisema utafiti huo unasimamiwa na NIMR na kwamba, utakapokamilika, majibu yatatolewa na wananchi watapewa taarifa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margareth Sitta, alisema kuna haja kwa Serikali kuendelea kuwekeza katika masuala yanayohusu maabara, kwani ni sehemu muhimu.
Alisema maslahi ya wafanyakazi katika maabara ya TFDA, yanatakiwa kuboreshwa na kusema usalama wao sio mzuri kiafya kwa kuwa wanapokea harufu tofauti katika kazi ya uchunguzi.
Aliwataka wananchi kuacha kuingiza dawa kwa njia za panya kwani hali hiyo ni hatari kwa afya.
Sitta, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, alisema dawa hizo hazina kiwango cha ubora unaotakiwa na matokeo yake ni madhara kwa binadamu.
Mkurugenzi wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni wananchi kutokuwa na uelewa juu ya matumizi ya dawa, ambazo zina viwango kwani wengi wao wamekuwa wakijinunulia dawa katika maeneo yasiyohusika.
Uingereza yaipiga nyundo serikali  
 

 
David Cameron
YATOA ASILIMIA 30 KWENYE FUNGU LA BAJETI
Claud Mshana
SERIKALI ya Tanzania imepata pigo kiuchumi baada ya Uingereza kupunguza msaada wake katika fungu la bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 kwa asilimia 30, Mwananchi Jumapili limebaini.Hatua hiyo ya Uingereza kupitia Idara ya yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), imekuja wakati nchi wahisani zinazochangia bajeti ya serikali (GBS), zikisema zitapitia misaada ya fedha wanazotoa ili kujua kama serikali imefikia malengo yaliyokusudiwa. Jumla ya Washirika wa Maendeleo (DPs) 12 wanasaidia bajeti ya Tanzania, ambapo kwa mwaka huu wa fedha, nchi hizo zilitoa kiasi cha Dola 453 milioni.
Hata hivyo, katika mchango wao wa bajeti ya mwaka huu wahisani wamezuia kiasi cha Dola 100 milioni( karibu Sh170bilioni) ambazo zitatolewa iwapo nchi hizo zitaridhishwa na utendaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2010/11 nchi hizo zilitoa Dola 534 milioni ( karibu Sh907.8 bilioni) kuchangia bajeti ya serikali.
Hatua ya kuzuiwa kwa kiwango hicho cha msaada wa Uingereza kwenye bajeti inatokana na serikali kushindwa kusimamia vizuri masuala mbalimbali, kubwa ikiwa ni mazingira ya uwekezaji na kupambana na umasikini, kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Andrew Mitchell.
Mitchell katika barua yake ya Agosti 3, 2011 kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Uchumi ya Bunge la Mabwanyenye la Uingereza (House of Lords), amesema mawaziri wa Uingereza na serikali yake kwa ujumla wamekuwa wakisisitiza Tanzania kuimarisha mazingira ya kufanya biashara kama njia muafaka ya kupunguza umasikini.
“Hatua za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji zimehusishwa katika kitengo cha ufuatiliaji wa misaada kwenye bajeti unaotolewa na Uingereza,” “Mwaka huu nimepunguza msaada wa Uingereza kwenye bajeti ya Tanzania kwa asilimia 30, kuonyesha kuwa tuko makini katika hili,” alisema Mitchell katika barua hiyo.
Mei 2010, Mitchell, aliiagiza Tume ya Mapitio ya Misaada (Bilateral Aid Review) kuchunguza kwa makini nchi ambazo DFID inafanya kazi kupitia programu za Uingereza za moja kwa moja za nchi na kanda. Mapitio hayo kwa mujibu wa mpango kazi wa DIFD nchini wa mwaka 2011 – 2015, yalitazama njia bora ambazo Uingereza inaweza kutumia kupambana na umaskini na kuhakikisha unakuwepo ufanisi wa kila fedha ya nchi hiyo inayotumika. Machi 2011, matokeo ya mapitio hayo yalitangazwa ambapo pamoja na mambo mengine, walifanya mapitio ya misaada inayotolewa kwa nchi mbalimbali.
“Mapitio hayo yalifanya tubadili kidogo mtazamo wa programu zetu na yametufanya tulenga nchi chache zaidi ili misaada yetu iende pale ambapo italeta tofauti na pale palipo na mahitaji makubwa,” inasema sehemu ya mpango kazi huo wa DIFD wa miaka mine kuanzia 2011.
Mapitio hayo pia yamependekeza DFID Tanzania kupunguza kutumia mfumo wa kupitisha msaada kwenye Bajeti ya Serikali (General Budget Support), kama tathmini ya programu ya nchi ya mwaka 2010 ilivyoshauri.
“Tathmini hii ilionyesha kuwa katika hali ya sasa, kupitisha msaada kwenye bajeti ya serikali si njia yenye ufanisi zaidi ya kuwasilisha matokeo ya misaada yetu na ilipendekeza tupunguze matumizi ya mfumo huo.” Naibu Waziri wa Fedha Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Naibu Waziri wa Fedha, Pereira Silima, alisema uamuzi huo wa Uingereza hautaiathiri serikali kwani ilishapanga bajeti kulingana na kiasi cha fedha walichokwisha fahamu kuwa watakipata.
“Unajua tunapopanga bajeti, tunajua wafadhili wanatoa nini, kwa hiyo taarifa tunapoipata kuwa fulani atapunguza, inakuwa iko nje ya bajeti yetu,” alisema Silima. Alifafanua kuwa kiasi kilichoingizwa kwenye bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 ni kile ambacho kiliahidiwa kutolewa na kuongeza kuwa bajeti haitadhurika kwani kama ni kutafuta njia mbadala, serikali ilishafanya hivyo tayari. Alikiri kuwa taarifa ya kupunguzwa kwa kiasi hicho cha fedha kwenye mchango wa bajeti walishaipata kwenye vikao vya awali vya kupanga bajeti na kuongeza: “Kuna wakati tunakuwa na vikao vya kuulizana ambapo kila nchi husema kile ambacho itachangia katika bajeti ya mwaka husika.”
Alipoulizwa kuwa kama Uingereza ilitoa sababu ya kupunguza fedha hizo, Silima alisema nchi hiyo ilibadilisha utaratibu kulipoingia serikali mpya. “Unajua serikali ni nyingine kwa hiyo zile taratibu zilibadilishwa na walipunguza nchi nyingi katika orodha ya nchi walizokuwa wakizisaidia,” alisema Silima. John Mnyika Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika aliitaka Uingereza kuweka wazi sababu za kupunguza misaada kwani kuna mambo mengi ambayo nchi wahisani wa maendeleo hawaridhiki nayo lakini hawaweki wazi. Aliongeza kuwa wadau wa maendeleo hawaridhiki na jinsi Serikali ya Tanzania inavyoshughulikia ufisadi, hususan suala la EPA.
“Baada ya EPA kujadiliwa bungeni, Serikali ya Tanzania ilikubaliana na wahisani kutengeneza mpango kazi wa kushughulikia ufisadi wa EPA, sasa hawaridhishwi na jinsi hatua zinavyokwenda,” alisema Mnyika. Aliongeza kuwa wahisani hao bado hawaridhishwi na jinsi serikali inavyoshughulikia mianya ya ubadhilifu wa fedha za bajeti ndani ya serikali. “Sehemu kubwa ya pesa za bajeti zinaishia mikononi mwa mafisadi badala ya kuwafikia wananchi na kuendeleza miradi yao,” aliongeza.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, aliongeza kuwa sababu nyingine ya Uingereza kupunguza misaada yake kwa nchi nyingi, ni mgogoro wa kiuchumi kwa nchi za ukanda wa Ulaya hususan tatizo la madeni linalozikabili nchi hizo hivi sasa. Alishauri kupunguzwa kwa matumizi yasiyo ya lazima ya serikali ili kufidia upugufu huo.

Zitto atoboa siri ya kinachomsibu  
 

 
NI UGONJWA WA KIPANDA USO, UMESHAMWANGUSHA MARA NNE
Kizitto Noya na Fredy Azzah
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amebainisha tatizo linalomsibu akisema madaktari wamemweleza kwamba anasumbuliwa na ugonjwa wa kipanda uso unaofahamika kitalaamu kama sinusitis ambao kwa hatua uliokuwa umefikia, tiba yake isingepatikana nchini.Kutokana na kubainika kwa maradhi hayo, amesema anatarajia kufanyiwa upasuaji wakati wowote kuanzia sasa huko India anakotibiwa.Zitto alieleza hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, katika ulingo wa wazi wa majadiliano ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika wenye zaidi ya wanachama 3,110.

“Tatizo lililogundulika ni sinusitis, ambayo tayari imekuwa sugu. Daktari Bingwa wa magonjwa haya, Dk Kimaryo (wa Muhimbili) akanieleza kwa kirefu juu ya tatizo hili na kuniambia suluhisho ni 'surgery' (upasuaji) na pale Hospitali ya Taifa hawafanyi hiyo operesheni,” alisema Zitto.
Naibu Kiongozi huyo wa upinzani Bungeni, alisema kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo Dk Kimaryo alishauri apelekwe India ambako kuna daktari bingwa mpasuaji wa ugonjwa huo...
“Baada ya kuwa malaria imedhibitiwa kwa kufikia nusu ya dozi niliyopewa na wadudu kuonekana kutokomea, Ofisi ya Bunge ikaandaa safari. Nimefika India. Nimebakiza sindano mbili ili kumaliza dozi hiyo na tayari nimefanyiwa taratibu zote kwa ajili ya 'surgery' hiyo.”

Juzi, Zitto alipelekwa India baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maradhi yanayomsumbua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alibainika kuwa na vijidudu 150 vinavyosababisha ugonjwa wa malaria.
Sunusitis ni ugonjwa gani?

Akizungumzia ugonjwa huo, Dk Idd Mujungu wa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga alisema ni ugonjwa unaofahamika na wengi kama kipanda uso.

“Kwenye kichwa cha mwanadamu kuna matundu ya hewa ambayo kitaalamu yanaitwa simus. Kipanda uso kinaweza kuyaziba matundu hayo kama ni cha siku nyingi na ikifikia hatua hiyo, upasuaji ni lazima.”

Alisema dalili nyingine za kipanda uso ni mgonjwa kutokwa machozi, kichwa kuumwa sana, macho kuwa mekundu na kuwa na mafua makali.

Alianza kuugua miaka 10 iliyopita
Zitto alisema tatizo hilo lilimuanza takriban miaka 10 iliyopita na katika kipindi chote hicho, amepoteza fahamu na kuanguka mara nne.
“Mara ya kwanza mwaka 2000 nikiwa Mwanza nikielekea kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum, mara ya pili Dodoma katika mkutano kama huo mwaka 2001, lakini ilikuwa usiku.
Mara ya tatu nilikuwa chumbani Hall II, mara baada ya kutoka ‘prep’ (kujisomea), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2002 na mara ya Nne Bungeni siku ya kupitisha Muswada wa Madini 2010 kufuatia wiki nzima ya Kamati na Mjadala wa Bunge," alisema na kuongeza:

“Nilianza kupatwa na maumivu ya kichwa usiku wa Ijumaa tarehe 20, (Oktoba, mwaka huu) Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kutoka jimboni tayari kwa kazi za Kamati za Bunge ambapo Kamati yangu ilikuwa imekwishaanza kazi wiki hiyo kwa kupitia mahesabu na utendaji wa mamlaka za maji nchini.”

“Kama kawaida yangu niliona maumivu hayo makali kama ni sehemu tu ya uchovu wa ziara za jimboni na safari za mara kwa mara nilizofanya ikiwamo kuhudhuria Mdahalo wa Umeme na Mkutano wa Uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika.
Hivyo nililala na nilipoamka kichwa kilikuwa kimepona na hivyo nikahudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma katika Ofisi ya Bunge mpaka saa saba mchana.”“Siku ya Jumapili saa 11:00 jioni nikiwa katika Hoteli ya Southernsun nilipatwa na homa kali ghafla.

Nilikatisha mkutano niliokuwa nao na kuamua kurejea nyumbani, lakini nilishindwa kuendesha gari na hivyo kumwomba dereva wa mheshimiwa Mhonga (Saidi Ruhwanya Mbunge wa Viti Maalumu Chadema), anifuate ili anisaidie kunifikisha nyumbani.”

“Nilipofika nyumbani kwangu Tabata, homa ilizidi kupanda na hivyo kuamua kwenda Hospitali mara moja. Nikapelekwa Aga Khan Hospital na nikapata huduma. Walituliza homa, nikapewa Panadol na baadaye nikaruhusiwa kurudi nyumbani mnamo saa tano usiku.
Nilipoamka siku ya Jumatatu nikaenda kazini kuongoza Kikao cha Kamati ya Bunge ambapo tulikuwa tunashughulikia hesabu za Bodi ya Utalii na Benki ya Posta Tanzania.”

“Nilipita Aga Khan kupata majibu ya ziada na kuambiwa nipo sawa ila nipumzike nisifanye kazi kwa siku kadhaa na nitakuwa sawa.”

“Siku ya Jumanne, niliamka nikiwa salama, kichwa kikiuma kwa mbali lakini siyo vya kutisha. Nikawajulisha wajumbe wenzangu wa kamati kuwa sitakwenda kazini na wao waendelee na kazi. Ilipofika saa 6:00 nilianza kutetemeka mwili mzima na homa kuwa kali sana huku kichwa kikiniuma sana sana sana!” Alisema alipelekwa tena Hospitali ya Aga Khan na vipimo kubainisha kuwa alikuwa na joto la nyuzi 39.8 na kupatiwa matibabu.

Alisema usiku wa Jumatano hali ilikuwa mbaya na joto lilipanda tena kufikia nyuzi 40 na kichwa kilianza kuuma zaidi na kuongeza... “Nilikuwa kama ninatwangwa kwenye kinu kwa kweli. Nilikuwa natetemeka sana. Ilikuwa taharuki kubwa sana katika chumba nilicholazwa.
”Alisema wageni waliofika kumjulia hali wakati hali inabadilika walikuwa Murtaza Mangungu na Mohamad Chombo ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC)... “Walishauri mara moja nihamishiwe Muhimbili.”

“Muda si mrefu kupita Waziri Lukuvi (William, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge) na Katibu wa Bunge walifika, wakaafiki na nikahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwa hali niliyokuwa nayo nikalazwa katika chumba wanachokiita mini-ICU. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Blandina Nyoni alikuwapo hospitalini tayari,” alisema.Alisema usiku huo alifanyiwa vipimo upya... “Ikaonekana nina wadudu wa malaria 150 na mara moja nikaanza matibabu. Namshukuru sana daktari kijana Dk Juma Mfinanga kwa umahiri mkubwa aliouonyesha tangu nilipofika pale mini ICU.”

Maalim Seif awakia Masheha Zanzibar

Na Talib Ussi Zanzibar
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF ambaye piya ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema viongozi wa serikali za mitaa (Masheha) wanawanyima fomu za kuombea vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi wafuasi wa CUF kwa makusudi ili kinapoteza nguvu ya ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Malim Seif aliyasema hayo leo ( jana) wakati akihutubia kwenye sherehe zilizoandaliwa na jimbo la Mtoni kuadhimisha mwaka mmoja wa ushindi wa chama hicho katika jimbo hilo zilizofanyika Bwawani mjini Zanzibar.
Alisema Masheha wanawanyima fomu wananchi hao kwa makusudi baada ya kupokea maagizo kutoka kwa viongozi wasioitakia mema Zanzibar na ambao wanachukizwa na hali ya amani na utulivu inayoendelea kudumu Zanzibar, tokea kufikiwa maridhiano ya kisiasa Novemba 2009.
Alielekeza Masheha wenye tabia hiyo wanapaswa kuiacha mara moja kwasababu vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi mbali na kutumika kwenye kura, lakini pia vinatumiwa na wananchi kupata huduma muhimu na kwa mujibu wa sheria.
“Masheha hawa wanaowazuia Wazanzibari wasipate vitambulisho hivyo wanatenda makosa” aliseam Maalim Seif.
“Mheshimiwa Rais kama hujui hili nakwambia, tumevumilia mwaka mzima, leo hii tumefikia hatua anatokea kiongozi wa CCM kutoka Bara anatoa maelekezo kama hayo kwa Masheha”, aliendelea kwa kulalamika Maalim Seif.
Alisema kwamba viongozi wa CUF kuwemo ndani ya serikali haimaanishi kuwa wakae kimya.,
“Vitambulisho vya ukaazi ni haki ya kila Mzanzibari aliyefikia umri wa miaka 18 ni haki yake ya kidemokrasia ambayo viongozi wote wa CCM na CUF wameahidi watailinda katika utekelezaji wa majukumu yao” alifahamisha katibu Mkuu huyo wa CUF.
Katibu Mkuu wa CUF alisema hali hiyo inasikitisha hasa kuona wananchi wanaokoseshwa vitambulisho hivyo ni wa upande mmoja tu na wale wa CCM wote wanapatiwa vitambulishi vya ukaazi mara wanapovihitaji.
Alieleza kwamba anahaki ya kuwashitua viongozi wenye tabia hiyo kwa sababu kuja kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar hakumaanishi vyama vya siasa havipo tena.
“Vyama hivyo vipo pale pale kila kimoja kikitekeleza majukumu yake” alikemea Malim Seif.
Akizungumzia suala la Katiba mpya, Maalim Seif ambaye pia ni Makamo wa Rais wa Zanzibar aliwataka wafuasi wa CUF na wananchi wote wa Zanzibar kujiweka tayari kwa ajili ya kuchangia mjadala huo.
Alisema baada ya Bunge kipitisha mswada wa marekebisho hayo ambayo huenda utawasilishwa Bungeni katika vikao vya hivi karibuni.
Alisema kuhusu suala la mfumo wa Muungano, sera ya chama cha Wananchi CUF iko wazi juu ya hilo, ambapo chama hicho kinataka mfumo wa Muungano wa serikali tatu, kama njia muafaka ya kumaliza migogoro mingi inayojitokeza ndani ya Muungano huo .
“Naamini Bunge linalokuja mswada wa marekebisho ya Katiba utafikishwa naomba waheshimiwa tutumie nafasi vizuri , wana CUF tunajua sera ya chama chetu inataka mfumo wa serikali tatu kuondoa malalamiko ndani ya Muungano”, alisema Maalim Seif.
Katika mkutano huo, Mwakilishi wa jimbo la Mtoni ambaye ni Waziri wa Biashara na Viwanda, Nassor Ahmed Mazrui alisema hadi sasa wamefanikiwa vizuri kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati walipokuwa wakiwaomba kura kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.
Waziri Mazrui alisema katika kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinawafikia wananchi wa jimbo hilo, ikiwemo maji safi na salama yeye binafsi hadi sasa ameshatumia shilingi milioni 280, ikiwemo kufanikisha ujenzi wa visima vya maji tisa, kufanikisha upasuaji kwa akinamama wenye matatizo, pamoja na kuhudumia mazishi na elimu

RAIS WA ZANZIBAR AZINDUA BOTI MPYA YA KILIMANJARO III



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Boti Mpya ya Kilimanjaro 111, inayomilikiwa na kampuni ya usafiri wa Baharini (Azam Marine) inayomilikiwa na Nd.Salim Said Baghresa,(wa pili kulia) ambayo hufanya safari zake kutoka Zanzibar- Dar es Salaam, na uwezo wa kuchukua abiria 540 kwa wakati mmoja,uzinduzi huo ulifanyika leo katika bandari ya Malindi Zanzibar,(kushoto) ni Waziri wa Miundimbinu na Mawasiliano Masoud Hamad Masoud,(Kulia) ni Baharia Kassim Siri Matola
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amezindua boti mpya ya Kilimanjaro111 na kueleza haja kwa wafanyakazi wa vyombo vya baharini kutumia sheria na taratibu zilizowekwa na Mamlaka husika badala ya kutoa huduma hiyo kwa matakwa yao na kuwasumbua wasafiri.
Alieleza kuwa kufanya kazi katika vyombo hivyo vya bahari bila ya kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na Mamlaka husima inaharibu biashara na kuondoa imani kwa wasafiri kwani nia ya wamiliki wa vyombo hivyo ni kutoa huduma kwa wananchi na ni tofauti na watoa huduma wanavyofanya.
Dk. Shein aliaysema hayo leo katika uzinduzi wa boti mpya ya Kilimanjaro 111 inayomilikiwa na Kampuni ya Coastal Fast Ferries Limited chini ya Mkurugenzi wake Mkuu Salim Said Baghressa.
Dk. Shein alieleza kuwa jitihada za pamoja zinahitajika katika suala zima la utoaji wa huduma katika usafiri wa vyombo vya baharini na kukemea baadhi ya mambo yanayofanywa na wahudumu hao ikiwa ni pamoja na kuuza tiketi kinyume na sheria.
Katika mazungumzo yake Dk. Shein aliipongeza Kampuni ya Coastal Fast Ferries Limited kwa kufanya kazi zake na kutoa huduma nzuri za usafiri na kuepuka hali hiyo kutokea katika vyombo vyake vya usafiri.
Dk. Shein alisema kuwa siku zote abiria wanatakiwa kupewa huduma bora ambazo zitawavutia katika safari zao.
Alisema kuwa ipo haja ya kuiga huduma zinazotolewa katika usafiri wa angani ikianzia viwanja vya ndege pamoja na huma ndani ya ndege.
Aidha, Dk. Shein aliitaka Wizara na taasisi husika kusimamia vizuri taratibu na sheria zilizowekwa katika kuhakikisha wanaoingia banharini wanafuata taratibu na sio kila mtu anaingia katika eneo hilo na kusababisha usumbufu kwa wasafiri.
Dk. Shein alisisitiza kuwepo nidhamu ya bandarini na Kuitaka Wizara husika kubadilika huku akieleza haja ya kuvitumia vyombo vya habari kwa kuielimisha jamii juu ya shughuli na taratibu za bandari.
“Wasiohusika na shughuli za bandarini wasiingie, na wale wenye kazi maalum wapewe vibali vitakavyoonesha shughuli zao”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa lengo la serikali ni kubadilisha haiba ya mji wa Unguja ikiwa ni pamoja na bandari yake na kueleza kuwa tayari visiwa vyote vilivyokuwa karibu na Zanzibar vimebadilika.
Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa Bwana Said Salim Baghresa kwa kutimiza ahadi yake ya kuleta boti mpya kwa ajili ya usafiri hapa nchini, hatua ambayo pia, itachangia uiimarishaji wa sekta ya utalii.
Alisema kuwa tayari serikali imeaza juhudi za kuimarisha huduma za usafiri kwa ajili ya kuimarisha sekta ya Utalii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa sehemu ya kushukia abiria katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume sanjari na azma ya kuimarisha uwanja wa ndege wa Pemba kufanya kazi usiku na mchana na kupelekea ndege kubwa aina ya Boing kuruka na kutua.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa usafiri wa watu walio wengi hapa Zanzibar ni usafiri wa bahari hivyo serikali bado ina azma ya kununua meli yake ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi na sio kushindana kibiashara ambapo pia inaendelea kuwashajiisha wafanyabiashara kuwa na meli kubwa na ya mizigo ili kutoa huduma hiyo.
Alisema kuwa bado kuna tatizo la uhaba wa vyombo vya baharini hivyo meli ya abiria na mizigo kati ya Unguja na Pemba, Tanga, Dar-es Salama na sehemu nyengine katika ukanda wa Afrika Mashariki inahitajika na serikali imo katika mchakato huo.
Dk. Shein pia, aliitaka Wizara husika kushirikiana na Salim Baghressa katika kuhakikisha ujenzi wa terminal ya abiria katika bandari ya Malindi Zanzibar linafanyiwa kazi kama ilivyo azma ya mfanyabiashara huyo.
Nae Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Masoud Hamad Masoud alisisitiza azma ya serikali ya kununua meli mpya kama historia ya usafiri wa baharini kwa upande wa Zanzibar inavyojionesha.
Waziri huyo pia, alieleza mchakato unaoendelea wa kuanzisha Chuo cha Mabaharia hapa Zanzibar ambapo Kamati ya kuanzisha chuo hicho inaendelea na kazi vizuri ambapo Mkurugenzi Salim Baghressa nae ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo.
Mapema Bwana Salim Baghressa alieleza kuwa uzinduzi wa boti hiyo unaenda sambamba na kusherehekea pia, miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kueleza kuwa hatua hiyo yote imekuja kutokana na kuwepo kwa amani na utulivu nchini chini ya viongozi wenye hekima na busara kama Dk. Shein.
Alieleza kuwa ujenzi wa boti hiyo umechukua zaidi ya miezi 10 katika Mji wa Hobart huko Australia na kueleza kuwa ametimiza ahadi aliyoahidi ya kuleta vyombo vipya vitakavyolingana na matakwa ya wananchi ambapo chombo hicho kinachukua abiria 540m na kutumia dakika 90 kati ya Unguja na Dar-es Salaam.
Baghressa alieleza kuwa kampuni yao ya Coastal Fast Ferries Limited aliyoanzishwa mwaka 2008 tayari imeshawekeza kiasi cha Dola za Marekani Milioni 20, hiyo ni kutokana na meli zake mpya tano, ikiwemo Kilimanjaro 1, Zanzibar Explorer, Kilimanjaro 11, Sea Rocket Limousine na Kilimanjaro 111.
Aidha, Baghresa alitoa compyuta mbhili kwa ajili ya waongoza meli zao na ya pili kwa ajili ya Mamlaka ya Usafiri Baharini ambapo alisema vyombo vengine vitaruhusiwa kutumia mtandao huo kwa gharama zao kwani gharama za mwanzo tayari wameshatoa.
Pia, Baghresa alieleza kuwa imefika wakati wa Zanzibar kuwa na ‘Passenger terminal’ ambayo itakuwa ya mfano na kivutio kwa watu na wasafiri wanaoingia na kutoa visiwani na kueleza kuwa si kweli kama ameomba kujenga terminal kwa boti zake pekee na hayo ni maneno tu yanayovumisha mitaani.

Picha mbali mbali za uzinduzi wa boti ya Kilimanjaro 111




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akitoa hutuba yake wakati wa sherehe za uzinduzi wa Boti Mpya ya Kilimanjaro111,inayomilikiwa na kampuni ya Usafiri wa Baharini ya Azam Marine



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akipata maelezo kutoka kwa nahodha wa Kilimanjaro111,Clement R.Mgalula



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akipata maelezo kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya usafiri wa Baharini (Azam Marine) Nd.Salim Said Baghresa,


Baadhi ya waalikwa katika hafla ua uzinduzi wa Boti Mpya ya Kampuni ya Azam Marine,Kilimanjaro111,wakiwa katika sherehe hizo zilizofanyika katika viwanja vya Bandarini Malindi Zanzibar,

  
















Saturday, 29 October 2011

Malkia Elizabeth II amkaribisha Rais Kikwete Perth
Malkia Elizabeth II wa Uingereza na Mumewe Philip Wakiwakaribisha Rais Dkt.Jakaya Kikwete, Mama Salma na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola katika dhifa aliyoiandaa kwaajili ya viongozi hao wanaohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Perth,Australia

Wake wa viongozi wakuu wa mkutano wa nchi wanachama wa jumuia ya madola wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano uliofunguliwa na Malkia - 0ct- 28-2011. Watano kutoka kushoto na mke wa rais Mama Salma Kikwete
Rais Kikwete akutana na Waziri Mkuu wa Australia
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete wakisalimiana na Waziri Mkuu wa Australiua Julia Gillard mjini Perth wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola unaoendelea mjini Perth, Australia

Friday, 28 October 2011

Kenya yaanza mapigano ndani ya Somalia



Vikosi vya Kenya
Vikosi vya Kenya
Vikosi vya Kenya vimepambana na wanamgambo wa kiislamu wa al-Shabab ndani ya Somalia kwa mara ya kwanza tangu kuvuka mpaka na kuingia nchini humo wiki mbili zilizopita.
Msemaji wa jeshi la Kenya Major Emmanuel Chirchir ameiambia BBC kuwa msafara ulishambuliwa kati ya miji ya Tabda na Bilis Qoqani.
Kila upande umesema mwenzake alishambuliwa.
Major Chirchir alisema kuwa wapiganaji tisa wa al-Shabab waliuawa na wanajeshi wawili kujeruhiwa, mmoja vibaya sana.
Al-Shabab kwa upande wake unakanusha idadi hiyo na kusema kuwa wakenya 20 ndio wameuawa na msemaji wa kundi hilo Abdul Asis Abu Muscab, amewaambia waandishi kuwa huu ndio mwanzo tu wa mapigano na mashambulizi zaidi yatafuatia.
Wakazi katika eneo hilo wanasema kuwa makabiliano yaliohusisha pia ufyatulianaji risasi yalidumu kwa nusu saa.
Kenya iliwatuma wanajeshi wake kusini mwa Somalia mapema mwezi huu, ikishutumu kundi la al-Shabab kwa msururu wa utekaji nyara Kenya.
Al-Shabab, kundi linalodhibiti eneo la kati na kusini mwa Somalia limekuwa likikanusha madai hayo na limetishia kuishambulia Kenya kulipiza kisasi.

Marekani yajiandaa kwa mashambulizi



Wakati huohuo Marekani imeanza kufanyia majaribio ndege zake za kivita zisizo na rubani nchini Ethiopia katika maandalizi ya kuanza mashambulio dhidi ya ngome za wapiganaji wa Al Shabaab Somalia.
Ndege hizo ambazo zinaweza kubeba makombora na mabomu yanayoelekezwa kwa kutumia mtambo wa satelite zitaruka kutoka kituo cha jeshi la Marekani katika mji wa kusini mwa Ethiopia wa Arba Minch.
Marekani hatahivyo imeihakikishia serikali ya Ethiopia kwamba ndege hizo hazina silaha kwa hivi sasa na zinatumika tu kuchunguza hali ya usalama.
Marekani imekuwa ikitumia ndege hizi nchini Djibouti ambako majeshi yake yana kambi yake ya kijeshi ikiwa ndio kambi ya kipekee ya majeshi ya Marekani barani Afrika.
Hayo yakiendelea Mkenya mmoja ambaye amekiri kuwa mwanachama wa al-Shabab, amehukumiwa kifungo cha maisha baada ya kukiri kuhusika na mashambulizi mawili ya gurunti katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.
Mwandishi wa BBC Noel Mwakugu akiwa mahakamani amesema kuwa Elgiva Bwire Oliacha alionekana kutabasamu wakati akipigwa picha na kusema kuwa hajuti kwa kile alichokifanya na kuwa hatakata rufaa kupinga hukumu yake.
Mtu mmoja aliuawa na wengine 29 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo mawili katika kilabu kimoja na kituo cha basi.

ICC yawasiliana na mtoto wa Gaddafi



Saif
Saif al-Islam hajaonekana hadharani tangu mwezi Agosti
Waendesha mashtaka wa kimataifa wamekuwa na "mawasiliano yasiyo rasmi" na mtoto wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi.
Mahakama ya uhalifu ya Kimataifa (ICC) imesema watu wa kati wametumika katika mazungumzo hayo yasiyo rasmi na Saif al-Islam.
Waendesha mashtaka wamesema mahakama imeweka wazi kwa mtoto huyo wa Gaddafi, kuwa anatakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kuwa hana hatia hadi itakapo thibitishwa mahakamani.

Washirika

Saif al-Islam, ambaye alidhaniwa kuwa huenda angerithi utawala wa baba yake, amekuwa akijificha kwa miezi kadhaa.
Taarifa za hivi karibuni zinadai kuwa alikuwa kwenye msafara unaoelekea kwenye Jangwa la Libya karibu na mpaka na Niger, nchi ambayo washirika wengine wa Gaddafi wamekimbilia.
Lakini taarifa hizo hazijathibitishwa, na ICC imesema haifahamu yuko wapi.
Mwendesha Mashtaka wa ICC Luis Moreno Ocampo amesema katika taarifa kuwa ICC inamtaka afikishwe mahakamani.

Mauaji

"Ofisi ya mwendesha mashtaka imeweka wazi kuwa iwapo atajisalimisha kwa ICC, atakuwa na haki ya kesi yake kusikilizwa mahakamani, na hana hatia hadi itakapothibitishwa.
Majaji ndio wataamua," imesema taarifa hiyo. Amri ya ICC ya kukamatwa kwa Saif al-Islam ilitolewa mwezi Juni na inamtuhumu kwa mauaji na utesaji.
Taarifa hiyo inadai kuwa alihusika kwa kiasi kikubwa katika kufanya mashambulio dhidi ya raia katika miji mbalimbali ya Libya, yaliyofanywa na majeshi ya Gaddafi mwezi Februari.

Zimbabwe

Bw Moreno-Ocampo amesema ICC imefahamishwa kwa "kupitia njia zisiizo rasmi" kuwa mamluki walikuwa wakijitolea kumhamisha Saif al-Islam kwenda katika nchi ambayo haijatia saini makubaliano ya ICC. "Ofisi ya mwendesha mashtaka pia inatazama uwezekano wa kukamata ndege yoyote inayoshukiwa ili kumkamata," imesema taarifa hiyo.
Taarifa zinasema huenda Saif al-Islam akaenda Zimbabwe iwapo ataamua kuikimbia ICC. Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe alikuwa mshirika wa muda mrefu wa Muammar Gaddafi.
Kiongozi huyo wa zamani wa Libya, ambaye aliiondolewa madarakani mwezi Agosti baada ya miezi sita ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, alikufa kutokana na jeraha la risasi wiki iliyopita baada ya mapigano makali katika jiji la Sirte.

 

    Polisi: Hatujuia ugonjwa anaoumwa Dk. Mwakyembe

     
     
     
    Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe
    Jeshi la Polisi nchini limesema halina taarifa kuhusu maradhi yanayomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe kwani suala hilo ni siri kati ya mgonjwa na daktari wake.
    Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Samson Kasala, alisema Dk. Mwakyembe kwenda kutibiwa nje ni kawaida kama watu wengine wanavyokwenda kutibiwa huko na kwamba kuhusu maradhi yanayomsumbua ni siri kati yake na daktari anayemtibu.
    Jeshi hilo limezungumzia afya ya Dk. Mwakyembe ambaye amepelekwa India kupata matibabu, kufuatia uvumi kuwa alipewa sumu.
    Akizungumzia kuhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulipa jeshi hilo miezi sita kusitisha kuwanyanyasa, alisema jeshi hilo sio chama cha siasa na kwamba linafanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kuangalia chama wala itikadi na kwamba hatua zinachukuliwa kwa yeyote anayevunja sheria.
    “Kuhusu uharamia, wahusika huwa wanapanga uharamia kwa njia za siri sana hivyo ni vyema vyombo vyote vya ulinzi na usalama kushirikiana na raia katika kupambana na jambo hili” alisema na kuongeza:
    “Jeshi la Polisi linaendelea kuwasihi wananchi kutoa ushirikiano pale wanapokuwa na mashaka na watu wasioeleweka popote nchini ili uchunguzi uweze kufanyika haraka na kubaini kama ni wahalifu au la” alisema Naibu Mkurugenzi huyo.
    Pia alizungumzia kuhusu askari polisi wawili, Konstebo Saad na Sajenti James, wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge, Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe, na dereva taksi Juma Ndugu katika msitu wa pande uliopo wilaya ya Kinondoni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Januari 14, mwaka 2006.
    Alisema askari hao walifunguliwa jalada la kesi hiyo Februari Mosi, mwaka 2006, lakini hadi leo hawajapatikana na jeshi ambalo lilitoa picha zao kwenye vyombo vya habari ili wasamaria wema wasaidie kuwakamata bado linawasaka.
    Kasala alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, ameshawafuta kazi askari hao na kwamba jeshi hilo haliwatambui tena kama watumishi wake.
    CHANZO: NIPASHE
    Zitto: Niombeeni
      

     

    Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akiwa amepumzika katika chumba cha uangalizi maalumu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya kusafirishwa jana kupelekwa nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi. Picha na Mpigapicha Wetu
    APELEKWA INDIA, VIGOGO WAMIMINIKA KUMWONA MUHIMBILI
    Waandishi Wetu
    WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda jana alikuwa miongoni mwa viongozi mbalimbali wa kitaifa waliofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kumjulia hali, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe muda mfupi kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema, anakuwa kiongozi wa nne kupelekwa India kwa matibabu katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, akitanguliwa na mawaziri wawili na naibu waziri mmoja. Hao ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

    Mbali ya Pinda, viongozi wengine waliofika kumjulia hali mbunge huyo ambaye alikuwa amelazwa katika chumba za uangalizi maalumu (ICU) ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed.

    Katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, viongozi kadhaa wa Serikali wakiwamo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira walimjulia hali na kumtakia safari njema.

    Baada ya kumwona, Pinda hakuwa tayari kuzungumza lolote juu ya afya ya Zitto ambaye pia Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na badala yake kuwataka waandishi wa habari waliokuwapo Muhimbili kuzungumza na daktari aliyekuwa akimtibu.

    Daktari wa Mbunge huyo, Profesa Victor Mwafongo alisema: “Mgonjwa anaendelea vizuri leo (jana) zaidi ya juzi. Hakupelekwa ICU kwa sababu alikuwa mahututi, tulimuweka hapa ili tuweze kuangalia afya yake kwa karibu zaidi.”

    Profesa Mwafongo alisema wingi wa watu ndiyo uliwalazimisha kumhamishia ICU ili madaktari wapate fursa ya kumhudumia vizuri.
    Alisema mbunge huyo amepelekwa India kwa lengo la kufanyiwa uchunguzi zaidi licha ya wao kubaini kuwapo kwa vijidudu 150 vya malaria.

    “Vipimo vinatofautiana, sisi tumempima, lakini pia wenzetu ni wataalamu zaidi, hivyo tunaamini kuwa kupelekwa huko kutasaidia kubaini matatizo yake,” alisema.

    Kuhusiana vijidudu 150 vya malaria, Dk Mwafongo alisema ni hali ya kawaida kwa mgonjwa yoyote kukutwa na vidudu hivyo na kwamba inategemea utamaduni wa kuangalia afya yake.

    Kauli ya Zitto
    Jana asubuhi, Zitto alitembelewa na mwandishi wetu na kueleza kuwa hali yake ilikuwa imeimarika na tatizo la maumivu ya kichwa lililokuwa likimsumbua limepungua kidogo.
    “Hali yangu inazidi kuimarika, nimetumia dawa za malaria, lakini bado tatizo la kichwa linanisumbua kidogo,” alisema Zitto.
    Zitto aliwataka Watanzania kuondoa hofu na badala yake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili aweze kushiriki katika Mkutano wa 10 wa Bunge.“Naendelea vyema, naomba Watanzania waelewe hivyo, waondoe wasiwasi na uvumi unaoenezwa,” alisema Zitto.
    Alisema tangu aanze kupata matibabu Muhimbili, amemudu kula chakula kama kawaida na hali ya uchovu imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, alisema: “Ninakwenda India kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwani kichwa kinauma,” alisema.
    Udhibiti Muhimbili
    Kulikuwa na udhibiti mkubwa wa watu kuingia katika wodi alikokuwa amelazwa mbunge huyo kijana kutoka na kile kilichoelezwa kuwa ni kumpa fursa ya kupumzika kutokana na maradhi aliyonayo.

    Msemaji wa Hospitali ya Muhimbili, Jezza Waziri alisema Spika wa Bunge, Anna Makinda alitoa maagizo ya kutoruhusiwa kwa mtu yoyote kuingia katika chumba alicholazwa Zitto isipokuwa kwa utaratibu maalumu.

    “Spika ameacha maagizo hayo kwamba taarifa za hali ya Zitto zitatolewa na Profesa Mwafongo, ila kwa ufupi Zitto anaendelea vizuri,” alisema Jezza.
    Hata alipokuwa akiondolewa hospitalini hapo kwenda uwanja wa ndege, kulitumika udhibiti wa aina yake hasa wa kukutana na kalamu na kamera za waandishi wa habari. Baada ya matayarisho yote ya safari kukamilika, waandishi wote waliokuwapo Muhimbili waliitwa kuzungumza na kaka yake Zitto, Salum kuhusu taratibu za safari hiyo.

    Wakati akifanya kazi hiyo pamoja na kujibu maswali kadhaa, muda huo ulitumika vyema kumtoa wodini na kumpakia kwenye gari na kuondoka.

    Safari ya India
    Kutoka Muhimbili, Zitto alikuwa katika gari la kawaida lililosindikizwa na mengine mawili ambayo kwa pamoja, yalitanguliwa na pikipiki ya polisi. Msafara huo ulifika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 8.55 mchana.

    Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Zitto aliteremka katika gari mojawapo lililokuwa katikati ya yale mawili na kisha kutembea mwenyewe hadi katika chumba cha Watu Mashuhuri (VIP). Lakini muda wote huo alikuwa amezungukwa na watu waliodhaniwa kuwa ni maofisa wa usalama.

    Baadaye ilibainika kwamba katika msafara huo alikuwapo pia Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na watu wengine waliotajwa kuwa ni ndugu zake.

    Waandishi wa habari waliokuwa uwanjani hapo waliondolewa na kupelekwa mbali na aliposhukia mbunge huyo na hata baada ya kuingia katika chumba cha VIP hawakuruhusiwa kusogea karibu na eneo hilo.

    Zitto aliondoka jana mchana akiwa na kaka yake, Salum Kabwe na mmoja wa wauguzi wa Muhimbili ambaye jina lake halikufahamika mara moja.

    Dk Slaa anena
    Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ameipongeza Ofisi ya Bunge kwa jinsi ilivyojitoa kushughulikia tatizo la kiongozi huyo.

    “Ninatoa shukrani kwa Ofisi ya Bunge kwa namna inavyowashughulikia viongozi, wamekuwa bega kwa bega tangu alipougua na kulazwa katika Hosptali ya Aga Khan na Hospitali ya Muhimbili na ndiyo wanaoratibu mipango ya kumsafirisha kwenda India kwa matibabu” alisema Dk Slaa.
    Habari hii imeandikwa na Zaina Malongo, Patricia Kimelemeta, Fidelis Butahe, Said Powa na Michael Jamson

    TUNAKUTAKIA UWAKILISHI MWEMA VODACOM MISS TANZANIA 2011 SALHA ISRAEL HUKO MISS WORLD 2011



    Vodacom Miss Tanzania 2011 Salha Israel akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya warembo wanaoshiriki shindano la Dunia, Picha wakiwa Scotland .



    Warembo wakiwa katika mitindo yao ya kupiga kelele
    WAZIRI MKUU MHE PINDA AKIMJULIA HALI MHE ZITTO KABWE MUHIMBILI




    Waziri Mkuu Mizengo Pinda akimuaga Mhe Zitto Kabwe Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini wakati alipomtembelea katika Hospitali ya Muhimbili ambako amelazwa kwa Matibabu Baada ya kuugua.



    Waziri Mkuu Mizengo Pinda akimfariji na kumpa pole Mhe Zitto Kabwe wakati akiwa amelala katika wodi ya Hospital ya Muhimbili.

    MALIKIA AHUTUBIA WAKUU WA NCHI ZA JUMUIA YA MADOLA LEO

    Malkia Elizabeth II wa Uingereza akihutubia wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola jijini Perth, Australia leo asubuhi
     
    Malikia akiwa katika picha ya pamoja na viongozi hao baada ya kuwahutubia

    Thursday, 27 October 2011

    Mswaada wa kupambana na madawa ya kulevya wapita (BLW) Zanzibar.

    Na Salma Said

    Mwanasheria mkuu wa Zanzibar Mh Othman
    Posted on October 27, 2011 by zanzibaryetu
    Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema barazani kwamba vigogo nao wanapaswa kuchukuliwa hatua wakibainika kuleta madawa ya kulevya
    WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha kwa sauti moja mswaada wa kupambana na kudhibiti madawa ya kulevya Zanzibar ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud amewataka wananchi kuwapeleka serikalini na kuwataja watuhumiwa ikiwemo vigogo wanaotajwa.
    Aliwataka wananchi sasa kuleta taarifa za vigogo wanaotuhumiwa kuingiza madawa ya kulevya nchini na Serikali haitosita kuzifanyia kazi taarifa hizo kwa maslahi ya taifa.
    ´Wajumbe na wananchi kwa ujumla mswada huu lengo lake kupambana na watu wa aina zote wanaojishungulisha na biashara ya madawa ya kulevya wakiwemo vigogo….waleteni na serikali itawashungulikia’ alisema Mwanasheria huyo.
    Masoud alisema hayo wakati akijibu hoja mbali mbali za wajumbe wa baraza la wawakilishi zilizowasilishwa katikia kikao ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe hao walichangia mswaada wa kuweka masharti bora ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya ambayo yamekuwa kero kwa jamii hapa Zanzibar.
    Alisema Zanzibar imeamuwa kuja na sheria yake ya kupambana na madawa ya kulevya na kuachana na ile ya Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kulifanyia kazi tatizo hilo ambalo ni janga la kitaifa huku vijana wengi wakiathirika na matumizi ya madawa hayo ambayo huingizwa nchini kwa uficho mkubwa.
    Akifafanua zaidi alisema wapo baadhi ya watu walikuwa wakisema kwamba Zanzibar hatupo makini katika kulishungulikia suala la madawa ya kulevya kiasi ya kutuhumiwa kuwepo mitaani na kwa uingizaji wa madawa ya kulevya katika uwanja wa ndege na bandarini.
    Aidha alisema Serikal inalishungulikia suala la usafirishaji nje ya nchi kiasi kikubwa cha fedha, kazi ambayo inafanywa na baadhi ya watu binafsi na taasisi za fedha.
    Othman alisema Serikali katika mswaada huu itaimarisha ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuona kwamba inakuwa na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa sampuli mbali mbali zitakazowasilishwa hapo na tabia ya kuwaachia watuhumiwa haitaachiwa.
    Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha mswaada huo wa marekebisho na kuweka masharti mengine ikiwemo ya kupambana na madawa ya kulevya.
    mwisho.
    Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri na kusema licha ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji safi na salama wa mkoa wa mjini magharibi, tatizo la maji bado lipo.
    Kauli hiyo imetolewa na naibu waziri Ardhi,Makaazi Maji na Nishati Haji Mwadini Makame wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la Kiwani (CUF) Hijja Hassan Hijja aliyetaka kujuwa tatizo la maji litakwisha lini licha ya juhudi za washiriki wa maendeleo kusaidia sekta hiyo.
    Mwadini alisema mradi wa maji safi na salama uliokuwa ukifadhiliwa na serikali ya Japan umemalizika lakini tatizo la maji lipo kwa wananchi wa Unguja.
    Alizitaja baadhi ya sababu ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha kushindwa kufanikiwa kwa mradi huo ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi.
    ‘Hili ni moja ya tatizo kubwa ambalo tumelibaini lipo kwa wananchi wetu……wananchi wanavamia vyanzo vya maji na kuharibu mazingira yake’alisema Mwadini.
    Hata hivyo alisema ipo zaidi ya miradi mitatu inayofadhiliwa na washiriki wa maendeleo ambayo lengo lake kubwa ni kumaliza tatizo la maji safi na salama kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
    Aliitaja miradi hiyo ikiwemo ule unaofadhiliwa na Benki ya maendeleo ya Afrika ADB,Serikali ya Watu wa China pamoja na Serikali ya Denmark ambayo itatoa utaalamu wa kazi za ofisi katika mamalaka ya maji safi na salama ZAWA.
    Alisema tayari Mamlaka ya maji safi na salama (ZAWA) imeanza kufanya utafiti na kuangalia vyanzo vyake vya maji ili kuona kwamba hakuna uvamizi unaofanywa.
    Serikali isicheze na bei ya mkate
    Na Ally Saleh


    Waswahili wana msemo wao iwapo kuna jambo ambalo waliamini kuwa ni baya au uovu lilikuwa litokee lakini kikavunjika. Huwa wana sema Mwenyeenzi Mungu amepitisha kheri yake. Na Mswahili humtegemea sana Mungu kuwa ndio nguzo yake.Naamini wengi wa Waswahili wa Zanzibar waliinua mikono juu kushukuru kuwa kwa sababu moja au nyengine, Muswada uliokuwa ujadiliwe na pengine baadae kupitishwa, uliondolewa katika Baraza la Wawakilishwi kwa kurudishwa Serikalini.
    Wengi wa watu mitaani walikuwa wakilalamika kuwa Muswada huo haukuwa zingatifu kwa wakati na umma kwa sababu nyingi na kwamba kuondoshwa kwake Barazani kumeleta faraja kwa watu wa kawaida ambao maisha yanazidi kubana kwao.
    Muswada huo ukipania kuongeza marupurupu ya kustaafu viongozi wa kisiasa basi ni wiki iliyopita tu chakula kikuu cha Mzanzibari, ambacho karibu kila siku hula mara mbili, yaani boflo, kimepanda bei.
    Wakati Serikali ikipeleka Muswada kunenepesha mafurushi ya ustaafu ya viongozi hao ambao wametafsiriwa katika Muswada huo kuwa ni Rais, Makamo wa Rais, Mwanasheria Mkuu, Maspika, Mawaziri na Manaibu, mkate wa boflo umepanda kutoka shs 150 hadi shs 200.
    Bila ya shaka tafsiri ya kupeleka Muswada huu Mahakamni ni kuonyesha kuwa Serikali haijui kinachotokea mtaani, na kama inajua basi si zingatifu. Kuongezeka kwa kitanzi cha boflo katika baadhi ya nchi moja nikikumbuka ni Sudan kulimuondosha Rais Jaffar Numeir.
    Ila kwa Zanzibar hilo lisingetokea hata siku moja baada watu wake ni wataratibu, watiifu kiasi ambacho wachache kama sisi ambao huwa tunasema tunaonekana kuwa ni wakorofi na kuna wakati hata tulibandikwa jina la wachochezi.
    Lakini ni haki gani aliyonayo kiongozi wa kisiasa kumwita mtu mkorofi au mchochezi kwa kudai kuwa si haki kabisa kupanga kuongeza marupurupu ya viongozi hao ilhali wananchi waliowaweka madarakani wanasota na kudhikika?
    Kuongezeka kwa bei ya boflo kwa mtu mwenye familia ya watu 7 ambao ni ya wastani hapa Zanzibar ina maana ni ongezeko la zaidi ya shs 20,000 kwa mwezi ambazo hazijaongezeka katika kipato chake kwa njia moja au nyengine.
    Kama Serikali ina wachumi imara itajua ni kiasi gani nakisi ya kipato cha watu kinachodidimia kwa kuhesabu shs 20,000 kwa kaya moja na kisha izidishe kwa kaya zote za Zanzibar na kisha ifanye hesabu hiyo kwa mwaka.
    Lakini sidhani kama wapangaji wa haya wanafikiria yote hayo. Ni kama ile hadithi ya Mfalme wa Ufaransa aliyeshangaa kwa nini watu wanaandamana kwa kukosa boflo na akasema kwa nini basi wasile keki.
    Nilisema hapo awali kuwa bei ya boflo ilitosha kumuondosha Numeir madarakani kwa sababu wananchi wake walikereka seuze sasa na kuongezewa vunge la marupurupu ya wakubwa wetu ilhali nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi ikawa ni nyimbo ya kisiasa ya mafanikio yajayo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
    Kumbe, kwa macho yangu sasa naona ni chambo. Hata kabla ya nyongeza hiyo haijalipwa kwa wafanyakazi, pengine kama nakumbuka uzuri italipwa mwezi huu, ndoana ikachapuzwa kwa Muswada huu.
    Muswada umeenda mbali zaidi kwa kuongeza tafsiri ya viongozi wa kisiasa kujumuisha pia Washauri wa Rais ambao hivi karibuni waliteuliwa kwa mkururo. Lakini pia baadhi ya washauri hao wanashikilia nafasi nyengine mbali mbali ambazo kwa wakati huu zinawapatia kipato kikubwa na hata pia waliapata viinua mgongo vyao kwa kazi zao za huko nyuma na pia kwa maana hiyo wanakula pensheni zao kama kawaida.
    Muswada una vifungu vinavyoelezea juu ya marupurupu ya mwanasiasa kulipwa kwa mjane wake iwapo atafariki lakini pia kulipwa kwa watoto wake wakiwa ni warithi wake halali.
    Huyu kizuka mbali ya kitita cha kustaafu ataendelea kupata pensheni ya kila mwezi. Kwa Rais hakuna suala la muda na kwa maana hiyo kizuka wake atalipwa uhai wake wote lakini kwa Makamo wa Rais wajane wamewekewa muda wa miaka mitatu
    Ila Kifungu cha 26 kimenitisha kidogo kwa sababu kinajenga mazingira magumu ambayo kuachwa wazi yanaweza kuleta hali ya kujipendelea kwa Rais aliye madarakani au pia kutumika vibaya. Kifungu kinasema Rais aliye madarakani ataweza kuweka utaratibu wa malipo ya mafao kwa kizuka wa Kiongozi wa Kisiasa.
    Kuna kipengele cha watoto wa Rais kulipwa pensheni ya kila mwezi hadi watapotimia miaka 18 na kwa mtoto wa kile iwapo ataolewa kabla ya umri huo, jambo amblo naliona ni la kibaguzi kwa nchi ambayo inajenga usawa wa raia wake na watoto wa Makamo wa Rais pia watastahili pensheni hiyo.
    Halafu kwenye mpangilio wa Jadweli ndiko ambako hesabu hasa mtu unaziona za marupurupu ya viongozi hao wa kisiasa yangekuwa iwapo Muswada ungepita au pengine utapopelekwa tena iwapo hakuna watu watalalamika juu ya mkubwa wake.
    Mfano Rais kulipwa kiinua mgongo kwa kiasi cha asilimia 50 ya mshahara wake, posho la kumaliza muda , pensheni ya kila mwezi kwa asilimia 80 ya posho la matunzo analolipwa Rais aliye madarakani, nyumba ya makaazi na msururu mwengine mrefu.
    Na haya pia hufanyiwa Makamo wa Rais na Spika kwa mujibu wa kiwango chao kwa kuoneyesha tofuati ya daraja zao ambazo pia kisiasa ziko wazi.
    Sasa haya yakipita tujue kuwa Zanzibar ina wastaafu wengi kabisa na Sheria ikapendekeza kuwa waliowahi kuwa Mawaziri Viongozi nao wahesabiwe kuwa na hadhi ya Makamo wa Rais, naam na wao wataula kwa staili mpya kabisa ya vyeo ambavyo hawakuvitumikia lakini wanavyofananishwa navyo.
    Nilisema pale mwanzo kuwa baadhi ya watu walishukuru kuwa Muswada huo umeondoshwa Barazani lakini sote tunajua kuwa Muswada huo utarudi tena kwa hoja kuwa kuwepo kwa sheria ya viinua mgongo na pensheni za viongozi ni jambo la lazima, na hilo tunalikiri.
    Lakini jambo ambalo halitasemwa ni kwa nini marupurupu hayo ni makubwa sana, yanahusisha wigo mpana sana na kwa hivyo yanameza sehemu kubwa ya mapato ya nchi? Sijajaribu kupanga hesabu itavyokuwa lakini naamini kwa msururu wa viongozi tulionao basi bajeti ya kuwalipa viongozi wa kisiasa kwa mwaka itakuwa kubwa kiasi mabega ya taifa yataelemewa.
    Ila najua kama kawaida ya Wazanzibari hili litapita. Wachache tutaosema, wachache tutaolalamika na wachache tutaotoa sauti na kuandika, lakini hakuna ataesikia na kuona athari kubwa ya kuwa na msururu wa viongozi wanaolipwa mafao makubwa kwa ukosefu wa dawa, ukosefu wa madeski maskulini mwetu.
    Na maisha ya Mzanzibari yatasonga mbele kwa bei ya boflo, petroli, vyakula kuongezeka na akisononeka yeye na watoto wake kimya kimya. Na kesho wakati wa kampeni utafika na atakwenda kupiga kura. Mungu iweke Zanzibar na watu wake watiifu.

    Wednesday, 26 October 2011

    Walibya waiomba Nato kukaa zaidi

    Bw Mustafa Jalil
    Mkuu wa baraza la mpito la Libya NTC ametoa wito kwa majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya Nato kuongeza muda wake wa kukaa Libya mpaka mwisho wa mwaka.
    Mkuu wa NTC Mustafa Abdel Jalil amesema kuongeza muda huo kunahitajika ili kusaidia kudhibiti silaha za ziada na kupambana na wanaomtii Kanali Gaddafi.
    Nato imechelewa kutoa uamuzi rasmi wa lini utamaliza harakati zake nchini humo.
    Ilitoa uamuzi wa awali wa kumaliza harakati zake Oktoba 31.
    Wanadiplomaisa walitarajiwa kuthibitisha tarehe hiyo siku ya Jumatano.
    Bw Jalil aliwaambia mkusanyiko wa watu huko Qatar kwa mataifa yaliyotoa msaada wa kijeshi kwa NTC, "Tuna matumaini kuwa Nato itaendelea na harakati zake mpaka angalau mwisho wa mwaka huu ili kutusaidia sisi na nchi jirani."
    Alisema ombi lake lilikusudia "kuhakikisha hamna silaha zozote zinazopenyezwa katika nchi hizo na kuhakikisha usalama wa Walibya kutoka kwa baadhi ya majeshi ya aliyekuwa kiongozi Kanali Gaddafi waliokimbilia nchi jirani".
    Bw Jalil aliongeza kuwa NTC lilitaka msaada " kuendeleza ulinzi wa Libya na mifumo ya usalama".
    Nato, ambayo ilianza shughuli zake Libya tangu mwezi Machi chini ya azimio la Umoja wa Mataifa kwa minajil ya kulinda raia, ilisema sasa itatoa uamuzi rasmi wa muda wa kukaa nchini humo siku ya Ijumaa.
    Msemaji wa Nato Bi Carmen Romero alisema, "kama ilivyokubalika, NATO itaendelea kuangalia hali, na itaendeleza uwezo wake wa kupambana na vitisho vyovyote dhidi ya raia.

     

      CCM wahaha kujinusuru   
       
      WASSIRA AJIFUNGIA ARUSHA KUSAKATA SULUHU, YUMO PIA SHIGELLA WA UVCCM
      Peter Saramba, Arusha
      MSUGUANO wa kisiasa ndani ya CCM ambao umekitikisa chama hicho siku chache zilizopita umechukua sura mpya, na sasa chama hicho kinamtumia kada wake mkongwe, Steven Wassira kuanza harakati za kutatua mgogoro huo.Wassira ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), yupo Arusha ambako jana alianza mchakato wa vikao vinavyowashirikisha viongozi na baadhi ya makada wa chama hicho wa Wilaya na Mkoa wa Arusha, eneo ambalo limekuwa kitovu cha vurugu zinazoonekana kukitikisa CCM hadi ngazi ya taifa.

      Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka jana, CCM Arusha kimegeuka kuwa kitovu cha vurugu na mpasuko unaotikisa chama hicho na Umoja wake wa Vijana (UVCCM).

      Wassira ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, alifanya kikao na UVCCM mkoani humo ambacho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Martin Shigella.

      Vyanzo vya habari vilidokeza kwamba, katika siku yake ya kwanza ya ziara mkoani hapa, Wassira jana alikutana na UVCCM Wilaya ya Arusha ikiwa ni mwanzo wa safari hiyo ya kusaka suluhu.

      Wassira aliyewasili Arusha juzi, katika kikao chake hicho alikutana na wajumbe wa Baraza la Vijana la Wilaya ya Arusha katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Youth League eneo la Faya, ambako vijana hao walimtaka kutumia nafasi yake ya ulezi na uwaziri kukutana na pande zote zinazonyukana kutafuta ufumbuzi kabla mambo hayajaharibika zaidi.

      Pamoja na kujadili mgogoro ulioko kati ya makundi ya vijana ambao uongozi wake wilayani Arusha chini ya Godfrey Mwalusamba unadai unachochewa na mwenyekiti aliyepita, Ally Bananga, kikao hicho pia kilijadili ziara ya Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa iliyopingwa na kususiwa uongozi wa Mwalusamba.

      Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kuwa, Wassira alielezwa na vijana hao wakiongozwa na mmoja wa wajumbe aliyetajwa kwa jina la Mussa Daudi Lungo kwamba tatizo la UVCCM na chama hicho kwa ujumla ni harakati za urais 2015 zinazohusisha baadhi ya makada, viongozi na wanachama.

      Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, zaidi ya nusu ya wajumbe wa kikao hicho walimuunga mkono Mwalusamba katika kila hoja aliyotoa.

      Kauli ya Wassira
      Akihitimisha kikao hicho, Wassira aliahidi kuchukua maelezo yatakayotolewa na pande zote kwa ahadi kwamba atayawasilisha kwenye Kamati Kuu (CC) ya CCM inayotarajiwa kukutana siku chache zijazo.

      Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alithibitisha ujio wa Wassira na kwamba ziara hiyo ni ya kawaida katika kuimarisha chama na kufuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

      Chatanda aliyezungumza kwa simu jana jioni, alisema Wassira alitarajiwa kukutana na kamati ya siasa ya wilaya hiyo kabla ya leo asubuhi kukutana na wajumbe wa baraza la vijana mkoa na kuhitimisha kwa kukutana na wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa mchana.

      “Kama mjumbe wa NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM) na mlezi wa chama mkoa, atafanya (Wassira) vikao na ngazi mbalimbali ya uongozi wa chama na jumuiya zake na kwa sababu hii ni ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa mlezi wetu, tutampa taarifa ya hali ya mkoa kisiasa,” alisema Chatanda.
      Ingawa Chatanda hakutaka kuzungumzia kwa undani maudhui ya ziara hiyo iliyokuja kukiwa na fukuto na minyukano kati ya makundi yanayodaiwa kuchochewa na harakati za urais 2015, moja kati ya ajenda muhimu ya vikao vya waziri huyo ni kutafuta chanzo, sababu na ufumbuzi wa migogoro ya mara kwa mara miongoni mwa viongozi na wana CCM Arusha.

      Migogoro ilikoanzia
      Katika siku za karibuni, Arusha imegeuka kuwa chimbuko la vita ya maneno miongoni mwa makada wa CCM, hulka ambayo imesambaa hadi kwa viongozi wa kitaifa wa chama hicho.

      Tuhuma za hivi karibuni ni zile zinazomtaja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba amekuwa akikivuruga chama hicho kutokana na jinsi anavyopigia chapuo utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba.

      Wanaopinga falsafa hiyo wanasema inatumika vibaya kuwabana watu wenye nia ya kuwania urais wa 2015 lakini Nape mara kadhaa amekanusha kutokuwa na lengo hilo.

      Awali, mgogoro ulikuwa baina ya baadhi ya vijana wilaya na mkoa wa Arusha na katibu wa CCM Mkoa, Chatanda ambaye pamoja na viongozi na makada wengine walituhumiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kusababisha chama hicho kipoteze kiti cha ubunge wa Arusha Mjini.

      Katikati ya mwaka huu baada ya kikao cha NEC, mkoa huo ulitoa onyo kali kwa baadhi ya vijana waliohusishwa na mvutano huo, akiwamo Mwenyekiti wa Vijana Mkoa, James Ole Millya aliyedaiwa kumtolea Chatanda maneno makali.

      Wakati hali ikionekana kutulia, mgogoro mwingine mpya umeibuka mwezi huu na safari hii ukitanuka hadi kuhusisha viongozi wa UVCCM Taifa akiwamo Malisa, baada polisi kuwanyima kibali kufungua matawi na kufanya mikutano ya hadhara.
      Hata hivyo, vijana hao walikaidi amri ya polisi na kuendelea na ratiba yao ambayo ilihitimishwa kwa mkutano wa hadhara ambao waliutumia kumtuhumu mtu waliyemwita mtoto wa kigogo wa chama na Serikali kwamba ndiye alitoa maelekezo ya wao kunyimwa kibali cha polisi.

      Siku chache baadaye, polisi walitangaza kumsaka Ole Millya ili wamhoji juu ya tuhuma hizo lakini tangu alipojisalimisha, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na jeshi hilo kuhusiana na mahojiano hayo.

      Wakati polisi wakiwa kimya, Ole Millya alitoa taarifa ndefu yenye kurasa 12 ambayo pamoja na mambo mengine, alirejea na kusisitiza kuwa wapo watoto wa vigogo wa chama na Serikali wanaotumia madaraka ya wazazi wao kuvuruga UVCCM na kuingilia baadhi ya utendaji serikalini.