Zanzibar yazindua teknolojia baharini |
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imezindua mfumo mpya wa kuongoza vyombo vya usafiri majini utakaotumia kompyuta kwa lengo la kuvifuatilia vikiwa njiani. Teknolojia hiyo ya Digitali inayofanana na ile ya ndege, inaingia sokoni kukabiliana na ajali za meli zisizokuwa za lazima.Akizindua teknolojia hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, alisema mfumo huyo utasaidia kuwabana wafanyabiashara wote wasio waaminifu ambao wanaweka mbele maslahi yao na kusahau utu. Hivi karibuni zaidi ya watu 1,000 wanasadikiwa kupoteza maisha kufutia ajali ya meli ya Mv Spice Islands, baada ya kuzama katika mkondo wa Nungwi kufutia boti hiyo kujaza mizigo kupita uwezo wake. Hata hivyo, Dk Shein aliwataka wafanyakazi wa vyombo vya baharini kutumia sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika, badala ya kutoa huduma hiyo kwa matakwa yao na kuwasumbua abiria. Dk Shein alisema kufanya kazi katika vyombo hivyo vya baharini bila ya kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na mamlaka husika, inaharibu biashara na kuondoa imani kwa wasafiri kwani nia ya wamiliki wa vyombo hivyo ni kutoa huduma kwa wananchi tofauti na watoa huduma wanavyofanya. Rais Shein alisema siku zote abiria wanatakiwa kupewa huduma bora ambazo zitawavutia katika safari zao, siyo bugudha wanazopewa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu. Aliitaka wizara na taasisi husika kusimamia vizuri taratibu na sheria zilizowekwa katika kuhakikisha wanaoingia baharini wanafuata taratibu, siyo kila mtu anaingia eneo hilo na kusababisha usumbufu kwa wasafiri huku akisisitiza kuwapo nidhamu ya baharini. |
No comments:
Post a Comment