Sunday, 30 October 2011

Marais wastaafu Z`bar kupewa Ofisi za maisha
 
 
Wawakilishi wapinga na kutoa masharti mazito
Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais (Ikulu) Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini
Muswada wa kuweka sheria mpya ya kuwalipa pensheni wajane na watoto wa marais wastaafu umekwama kuwasilishwa barazani baada ya wajumbe kudai haujazingatia maslahi ya taifa.
Muswada huo ulikuwa uwasilishwe na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais (Ikulu) Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, ambao ungewanufaisha viongozi wa kisiasa wa kitaifa Zanzibar.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini muswada huo umepingwa mara mbili na wajumbe katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo na katika kamati ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wa kitaifa chini ya Mwenyekiti wake, Hamza Hassan Juma.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Hamza amethibitisha kuwa kamati yake imetoa mapendekezo ya kutaka ufanyiwe marekebisho makubwa kabla ya serikali kuwasilisha tena katika baraza hilo Mwakani.
Aliyataja miongoni mwa mapendekezo hayo kuwa ni viongozi wastaafu wasipewe Ofisi na Serikali, pamoja na wasaidizi wasiopungua 12 ili kuepusha kuwabebesha mzigo wananchi wa Zanzibar.
Aidha, wajumbe hao wametaka wajane wa marais wastaafu na watoto wao waondolewe katika utaratibu mpya wa kuanza kulipwa pensheni kila mwezi pamoja na washauri wa rais ambao wameelezwa sio viongozi wa kisiasa.
Kamati hiyo imetoa mapendekezo mengine kuwa wajumbe wa baraza la wawakilishi pia watambuliwe na sheria hiyo kama viongozi wa kisiasa badala ya sheria hiyo kuwatenga na kuwatambua viongozi wachache wa kitaifa.
Aidha kamati hiyo imesema kiwango kilichopendekezwa na Serikali kuwa mjane wa rais alipwe pensheni kila mwezi sawa na mshahara aliyokuwa akilipwa rais ni kikubwa na hakilingani na hali halisi ya uchumi wa Zanzibar.
Hamza alisema kwamba viongozi wengi wana watoto kati ya 10 hadi 15 hivyo wameitaka Serikali iweke idadi maalumu ya watoto ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha za umma ya kuwalipa pensheni sawa na kima cha chini cha mshahara kila mwezi pale wazazi wao wanapofariki wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
Hata hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamuwa kuitisha semina kwa wajumbe iliyofanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View mwishoni mwa wiki kujadili muswada huo lakini wajumbe waliendelea kuupinga muswada huo na kulazimika kushindwa kuwasilishwa katika mkutano wa tano wa Baraza hilo.
Upande wake Mwakilishi wa jimbo la Mkwajuni, Mbarouk Mussa Mtando alisema kabla ya wajane wa marais kuanza kulipwa pensheni sawa na mshahara anaolipwa rais aliyopo madarakani lazima kiwango chake kijulikane ili waweze kutathmini kabla ya kuamua kupitisha sheria hiyo.
Alisema kwamba kujulikana kwa kiwango cha mshahara wa rais wa Zanzibar kutawafanya wajumbe kutathmini kiwango cha fedha na hali ya uchumi wa Zanzibar.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya fedha na uchumi ya Baraza la Wawakilishi, Ali Omar Shehe, alisema muswada huo wanaukataa kwa sababu haujazingatia maslahi ya taifa na utawabebesha mzigo mkubwa wananchi wake.
Alisema kwamba kitendo cha Serikali kupendekeza wajane na watoto marais wastaafu kuanza kulipwa pensheni pale waume zao wanapofariki sawa na kuwabagua wajane wengine katika jamii.
Shehe alisema iwapo Serikali watalazimisha kupitisha bila ya kufanyika marekebisho hayo lolote litakalotokea ndiyo itakayowajibika.
Akizungumza katika semina hiyo Spika Pandu Amer kificho alisema kwamba kuna mambo ndani ya sheria hiyo yanahitajika kuangaliwa kwa umakini kabla ya kupitishwa na kuwa sheria.
Alitoa mfano yeye binafsi ana watoto 19 kati ya hao 12 wapo chini ya umri wa miaka 18 na kushauri suala la watoto wa viongozi wa kitaifa kuingizwa katika utaratibu wa kulipwa pesheni wazazi wao wanapofariki kuangaliwa kwa umakini.
Kwa mujibu wa muswada huo kifungu cha 10(1)(2) kimesema iwapo rais mstaafu atafariki mjane wake atastahili kulipwa penmsheni kila mwezi swa na mshaara wa rais aliyepo mdarakani wakati watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 watalipwa kima cha chini cha mshahara kila mwezi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment