Thursday, 27 October 2011

Mswaada wa kupambana na madawa ya kulevya wapita (BLW) Zanzibar.

Na Salma Said

Mwanasheria mkuu wa Zanzibar Mh Othman
Posted on October 27, 2011 by zanzibaryetu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema barazani kwamba vigogo nao wanapaswa kuchukuliwa hatua wakibainika kuleta madawa ya kulevya
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha kwa sauti moja mswaada wa kupambana na kudhibiti madawa ya kulevya Zanzibar ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud amewataka wananchi kuwapeleka serikalini na kuwataja watuhumiwa ikiwemo vigogo wanaotajwa.
Aliwataka wananchi sasa kuleta taarifa za vigogo wanaotuhumiwa kuingiza madawa ya kulevya nchini na Serikali haitosita kuzifanyia kazi taarifa hizo kwa maslahi ya taifa.
´Wajumbe na wananchi kwa ujumla mswada huu lengo lake kupambana na watu wa aina zote wanaojishungulisha na biashara ya madawa ya kulevya wakiwemo vigogo….waleteni na serikali itawashungulikia’ alisema Mwanasheria huyo.
Masoud alisema hayo wakati akijibu hoja mbali mbali za wajumbe wa baraza la wawakilishi zilizowasilishwa katikia kikao ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe hao walichangia mswaada wa kuweka masharti bora ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya ambayo yamekuwa kero kwa jamii hapa Zanzibar.
Alisema Zanzibar imeamuwa kuja na sheria yake ya kupambana na madawa ya kulevya na kuachana na ile ya Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kulifanyia kazi tatizo hilo ambalo ni janga la kitaifa huku vijana wengi wakiathirika na matumizi ya madawa hayo ambayo huingizwa nchini kwa uficho mkubwa.
Akifafanua zaidi alisema wapo baadhi ya watu walikuwa wakisema kwamba Zanzibar hatupo makini katika kulishungulikia suala la madawa ya kulevya kiasi ya kutuhumiwa kuwepo mitaani na kwa uingizaji wa madawa ya kulevya katika uwanja wa ndege na bandarini.
Aidha alisema Serikal inalishungulikia suala la usafirishaji nje ya nchi kiasi kikubwa cha fedha, kazi ambayo inafanywa na baadhi ya watu binafsi na taasisi za fedha.
Othman alisema Serikali katika mswaada huu itaimarisha ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuona kwamba inakuwa na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa sampuli mbali mbali zitakazowasilishwa hapo na tabia ya kuwaachia watuhumiwa haitaachiwa.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha mswaada huo wa marekebisho na kuweka masharti mengine ikiwemo ya kupambana na madawa ya kulevya.
mwisho.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri na kusema licha ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji safi na salama wa mkoa wa mjini magharibi, tatizo la maji bado lipo.
Kauli hiyo imetolewa na naibu waziri Ardhi,Makaazi Maji na Nishati Haji Mwadini Makame wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la Kiwani (CUF) Hijja Hassan Hijja aliyetaka kujuwa tatizo la maji litakwisha lini licha ya juhudi za washiriki wa maendeleo kusaidia sekta hiyo.
Mwadini alisema mradi wa maji safi na salama uliokuwa ukifadhiliwa na serikali ya Japan umemalizika lakini tatizo la maji lipo kwa wananchi wa Unguja.
Alizitaja baadhi ya sababu ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha kushindwa kufanikiwa kwa mradi huo ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi.
‘Hili ni moja ya tatizo kubwa ambalo tumelibaini lipo kwa wananchi wetu……wananchi wanavamia vyanzo vya maji na kuharibu mazingira yake’alisema Mwadini.
Hata hivyo alisema ipo zaidi ya miradi mitatu inayofadhiliwa na washiriki wa maendeleo ambayo lengo lake kubwa ni kumaliza tatizo la maji safi na salama kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Aliitaja miradi hiyo ikiwemo ule unaofadhiliwa na Benki ya maendeleo ya Afrika ADB,Serikali ya Watu wa China pamoja na Serikali ya Denmark ambayo itatoa utaalamu wa kazi za ofisi katika mamalaka ya maji safi na salama ZAWA.
Alisema tayari Mamlaka ya maji safi na salama (ZAWA) imeanza kufanya utafiti na kuangalia vyanzo vyake vya maji ili kuona kwamba hakuna uvamizi unaofanywa.

No comments:

Post a Comment