Polisi: Hatujuia ugonjwa anaoumwa Dk. Mwakyembe
.jpg)
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Samson Kasala, alisema Dk. Mwakyembe kwenda kutibiwa nje ni kawaida kama watu wengine wanavyokwenda kutibiwa huko na kwamba kuhusu maradhi yanayomsumbua ni siri kati yake na daktari anayemtibu.
Jeshi hilo limezungumzia afya ya Dk. Mwakyembe ambaye amepelekwa India kupata matibabu, kufuatia uvumi kuwa alipewa sumu.
Akizungumzia kuhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulipa jeshi hilo miezi sita kusitisha kuwanyanyasa, alisema jeshi hilo sio chama cha siasa na kwamba linafanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kuangalia chama wala itikadi na kwamba hatua zinachukuliwa kwa yeyote anayevunja sheria.
“Kuhusu uharamia, wahusika huwa wanapanga uharamia kwa njia za siri sana hivyo ni vyema vyombo vyote vya ulinzi na usalama kushirikiana na raia katika kupambana na jambo hili” alisema na kuongeza:
“Jeshi la Polisi linaendelea kuwasihi wananchi kutoa ushirikiano pale wanapokuwa na mashaka na watu wasioeleweka popote nchini ili uchunguzi uweze kufanyika haraka na kubaini kama ni wahalifu au la” alisema Naibu Mkurugenzi huyo.
Pia alizungumzia kuhusu askari polisi wawili, Konstebo Saad na Sajenti James, wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge, Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe, na dereva taksi Juma Ndugu katika msitu wa pande uliopo wilaya ya Kinondoni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Januari 14, mwaka 2006.
Alisema askari hao walifunguliwa jalada la kesi hiyo Februari Mosi, mwaka 2006, lakini hadi leo hawajapatikana na jeshi ambalo lilitoa picha zao kwenye vyombo vya habari ili wasamaria wema wasaidie kuwakamata bado linawasaka.
Kasala alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, ameshawafuta kazi askari hao na kwamba jeshi hilo haliwatambui tena kama watumishi wake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment