Monday, 28 October 2013

Takwimu za wapiga kura wapya katika majimbo matano ya Unguja zimepotea.


Chama Cha Wananchi (CUF) kimeanza kumtilia shaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha na kudai kuwa hana sifa za kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Akizungumza na wanachama na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Pwepweu Tumbe, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jecha ni mkereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kwamba kwa mazingira hayo hatoweza kutenda haki katika uchaguzi.
Akielezea zaidi kuhusu madai hayo Maalim Seif amedai kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Jecha aliingia katika mchakato wa kugombania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kwamtipura kupitia CCM, lakini hakuweza kupata nafasi baada ya kushindwa katika mbio za kugombea nafasi hiyo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameibua hoja hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa takwimu za wapiga kura wapya katika majimbo matano ya Unguja zimepotea kwenye Komputa, na kudai kuwa huo ni mkakati maalum ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Ameyataja majimbo yanayodaiwa kupoteza Takwimu zake za wapiga kura wapya kuwa ni Bumbwini, Donge, Kitope, Bububu na Mfenesini.
Maalim Seif ameenda mbali zaidi kwa kumtaka Mwenyekiti huyo ajiuzulu wadhifa huo na kama akishindwa basi Rais wa Zanzibar achukue jukumu la kumfuta kazi.
“Kwa kweli Mwenyekiti huyu hana sifa kabisa za kuwa Mwenyekiti wa ZEC kwa sababu ni mkereketwa wa CCM aliyegombea nafasi ya Ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2010, hawezi kabisa kutenda haki katika uchaguzi”, alisema Maalim Seif na kuongeza
“Kwa hivyo namuomba sana Mwenyekiti huyu ajiuzulu, na kama akishindwa basi kwa heshima zote namuomba Rais Dokta Shein amuwajibishe kwa kumfuta kazi”, alisisitiza.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa moyo wake wa kusimamia vyema mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Tanzania.
Amesema kitendo cha kukubali kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani ni hatua muhimu katika kuendeleza mchakato huo ambao ulionekana kuanza kuzorota baada ya vyama vya upinzani kuukataa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba.
Amewasisitiza wananchi wa Zanzibar kuacha tofauti zao katika kipindi hiki cha mchakato wa mabadiliko ya katiba, na badala yake  washirikiane katika kupata katiba iliyo bora, yenye maslahi kwa Zanzibar na vizazi vijavyo.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Tumbe Mhe. Rufai Said Rufai amesema atashirikiana na viongozi wengine wa Jimbo hilo pamoja na wa Wilaya ya Micheweni kuhakikisha kuwa vijana wote waliotimiza umri wa miaka 18 katika jimbo hilo wanapata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID).
Katika Mkutano huo Maalim Seif alikabidhi kadi 1536 kwa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho wote wakitokea jimbo la Tumbe, ambapo miongoni mwao wametoka Chama Cha Mapinduzi.

Saturday, 26 October 2013

SMZ yaridhishwa na jitihada za UN kuleta maendeleo Zanzibar 


un_flag
 
Wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 68 tangu kuasisiwa kwake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeelezea kuridhishwa na jitihada za Umoja huo katika kuiunga mkono Zanzibar kupitia nyanja tofauti zikiwemo kuwajengea uwezo vijana pamoja na elimu ya afya hasa kwa akina mama na watoto.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo katika hafla maalum ya kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa iliyofanyika hoteli ya Serena Mjini Zanzibar.
Amesema Umoja wa Mataifa umekuwa mstari mbele kuchangia juhudi za maendeleo nchini kupitia mashirika yake yakiwemo Shirika la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Shirika la kuhudumia watoto (UNICEF), Shirika la Kazi (ILO) na Shirika la Afya duniani (WHO).
Amesema mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na kuwepo kwa mashirika ya Umoja huo, na kwamba Serikali inathamini mchango wa Umoja wa Mataifa katika maendeleo ya nchi.
Amehamisha kuwa Serikali itaendeleza uhusiano mwema uliopo kati yake na Umoja wa Mataifa, na kuahidi kufanya juhudi za makusudi kuona kuwa malengo ya millennium yaliyoanzishwa na Umoja huo yanafikiwa ifikapo mwaka 2015.
Amesema pamoja na mambo mengine Umoja wa Mataifa umekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza umoja na mshikamano duniani, sambamba na kusimamia masuala ya amani, utawala bora na haki za binadamu.
Maalim Seif ametaja baadhi ya michango muhimu iliyotolewa na Umoja huo kwa Zanzibar kuwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za vijana hasa wa vijijini katika kukabiliana na tatizo la ajira, kusaidia mpango mkakati wa vijana Zanzibar, elimu, pamoja kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Hata hivyo ameuomba Umoja huo kuongeza misaada yake kwa Zanzibar, hasa katika kuwawezesha vijana kuweza kukabiliana na ukosefu wa ajira na kupunguza umaskini.
Nae Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alberic Kacou amesema  wanaadhimisha siku hiyo kutathmini hatua zilizofikiwa na Umoja huo katika kutunza amani na maendeleo duniani.
Amesema katika tathmini yake kwa mwaka 2013, Umoja huo unakabiliwa na changamoto ya kiusalama kutokana na mapigano yanayoendelea nchini Syria.
Amesema mamilioni ya watu wamekuwa wakiutegemea Umoja huo kwa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na janga la njaa, na kwamba hautosita kutoa misaada hiyo kwa kadri itavyohijatika katika nchi mbali mbali.
Kuhusu malengo ya millennium, Kacou amezitaka nchi wanachama kuendeleza juhudi ili kuona kuwa zinafikia malengo hayo ifikapo mwaka 2015, huku akilenga zaidi suala la kupunguza umaskini.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na vingozi mbali mbali wakiwemo mabalozi wadogo waliopo Zanzibar, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Abdulhamid Yahya Mzee.
Hassan Hamad (OMKR)
Oktoba 26, 2013

Serikali ya China yatoa msaada wa fedha kwa SMZ 


Waziri wa Fedha  Omar Yussuf Mzee
Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana Saini mkataba wa makubaliano na Serikali ya China  ambapo nchi hiyo itaipatia Zanzibar msaada wa zaidi ya  Dola milioni sita za Marekani ikiwa ni uendelezaji wa misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa Zanzibar katika nyanja mbali mbali za Uchumi.
Sherehe za utiaji saini makubaliano hayo  zilifanyika leo  katika Wizara ya Fedha, Vuga  ambapo Waziri wa Wizara hiyo  Omar Yussuf Mzee aliiwakilisha Zanzibar na Balozi mdogo wa China hapa Zanzibar Xie Yunliang aliiwakilisha nchi yake.
Akizungumza baada ya utiaji saini, Waziri wa Fedha alisema kua msaada huo utalenga katika nyanja mbali mbali ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, Uchimbaji wa visima vya maji safi na salama na kupambana na mbu wa malaria  katika maeneo ambayo maradhi hayo bado yapo.
Alisema kazi iliobakia hivi sasa ni kwa Idara ya  Hazina kuwasiliana na wahusika  ili utekelezaji wa makusudio hayo yaweze kufikiwa kwa haraka.
Nae Balozi Xie Yunliang alisema kuwa  Zanzibar na China ni nchi mbili zenye uhusiano mzuri  wa muda mrefu hali ambayo imeifanya kua ni rafiki wa karibu.
Alisema  makubaliano hayo ni muendelezo wa misaada wanayoitowa ili kuona Zanzibar inapiga hatua katika juhudi zake za kukuza Uchumi na Maendeleo ya wananchi.
Utiaji saini makubaliano hayo ulikwenda  sambamba na  kukabidhiwa hati za Taa za Barabarani zinazo tumia nishati ya jua katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar ambapo mradi huo ulifadhiliwa na Serikali ya China.

Friday, 25 October 2013

Mageuzi tena Katiba Mpya


Mwandishi Wetu
23 Oct 2013
RASIMU ya awali ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imekwishajadiliwa katika Mabaraza ya Katiba na sasa inafanyiwa uchambuzi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inafanyiwa mabadiliko kadhaa ya msingi huku mfumo wa Serikali Tatu ukiendelea kubaki kama ilivyopendekezwa, Raia Mwema limeelezwa.
Kati ya mambo ya msingi ambayo yataingizwa katika awamu ya pili ya rasimu ya Katiba Mpya ikakayowasilishwa kwa Rais na kisha katika Bunge la Katiba mara baada ya kukamilika ni pamoja na mipaka kati ya Tanganyika na Zanzibar, kuongozwa kwa mambo ya Muungano kutoka saba yaliyopendekezwa awali hadi 10, kinga dhidi ya mashitaka ya Rais, majimbo ya ubunge kwa Bunge la Muungano, ulinzi na usalama pamoja na vyama vya siasa kuweza kufukuza wabunge walioshinda kwa ridhaa ya vyama hivyo.
Mipaka ya Tanganyika na Zanzibar
Mipaka ya Tanganyika na Zanzibar ni lazima iwekwe ndani ya Katiba ili kila mamlaka ya nchi washirika iendeshe shughuli zake bila kuingiliana. Uchimbaji wa mafuta au uvuvi wa samaki, Tanganyika ijue iishie wapi na Zanzibar iishie wapi.
Kwa sasa katika rasimu ya Katiba Mpya, sura ya kwanza inayozungumzia mipaka, alama, lugha, utamaduni na tunu za taifa, ibara yake ya pili inaeleza kuhusu eneo la Jamhuri ya Muungano kuwa ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari.
Mambo ya Muungano kutoka saba hadi 10
Kwa sasa, katika rasimu ya kwanza ya Katiba mpya, mambo ya Muungano yanatajwa kuwa saba ambayo ni mosi, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pili, ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; tatu, uraia na uhamiaji; nne, sarafu na benki kuu; tano, mambo ya nje; sita, usajili wa vyama vya siasa na saba; ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Katika mambo hayo saba, yatanatarajiwa kuongezwa matatu kwa mujibu wa maoni yaliyotolewa wakati wa Mabaraza ya Katiba. Yanayoweza kuongezwa ni Haki za Binadamu, Tume Huru ya Uchaguzi, Maadili na Miiko ya Uongozi.
Kinga dhidi ya mashitaka ya Rais
Rasimu ya kwanza ya Katiba mpya iliyojadiliwa katika Mabaraza ya Katiba ilipendekeza katika Ibara ya 83(1) na (2) kuhusu kinga dhidi ya mashitaka ya Rais. Katika ibara hiyo ya 83 (1) inaeleza; Wakati Rais akiwa madarakani, hatashitakiwa wala mtu yeyote hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai.
Ibara ya 83(2) inaeleza; wakati Rais ameshika madaraka kwa mujibu wa Katiba hii, haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri la madai kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama raia ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ila tu kama angalau siku thelathini kabla ya shauri kufunguliwa mahakamani, Rais atapewa au ametumiwa taarifa ya madai kwa maandishi kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na taarifa hiyo ikiwa inatoa maelekezo kuhusu chanzo cha shauri hilo, kiini cha madai yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa analodai.
83 (3) inaeleza; isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na kura ya kutokuwa na imani na Rais, haitakuwa halali kwa mtu kumshitaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo alilofanya wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais.
Katika eneo hili kuhusu kinga dhidi ya mashitaka ya Rais, maoni mengi ambayo yanapewa nafasi kubwa kuwekwa katika rasimu ijayo ya Katiba mpya itakayowasilishwa katika Bunge la Katiba ni kutaka kuwapo na mwanya wa kumshitaki Rais baada ya kuondoka madarakani, hasa kwa makosa ambayo atakuwa amefanya yasiyohusiana na madaraka yake ya urais.
“Huwezi kuwa na kinga ya jumla katika kumshitaki Rais ambaye amekwishaondoka madarakani, tunaweza kuwa na kinga ya kutomshitaki kwa mambo ambayo ameyafanya kama Rais na lakini lazima kuwe na nafasi ya kumshitaki kwa mambo ambayo ameyafanya akiwa madarakani ambayo si sehemu ya majukumu ya Rais. Kwa mfano, ikitokea Rais amehusishwa na matukio ya hovyo kama ubakaji. Jiulize, ubakaji ni kazi za Rais…kama siyo kwa nini asishtakiwe baada ya kuondoka madarakani?” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Majimbo ya Bunge la Muungano utata
Kwa kuzingatia maoni ya wadau wengi wa Mabaraza ya Katiba, kumekuwa na hali ya kupaki njia panda katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo katika rasimu yake ya awali ilipendekeza katika Ibara ya 105 (2) kuhusu aina za wabunge ambao ni (a) waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi (b) wabunge watano watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuchaguliwa kuwa waunge kuwakilisha watu wenye ulemavu kwa kuzingatia uwiano wa Washirika wa Muungano.
Lakini sehemu inayoiweka njia panda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sasa, hasa baada ya kukusanywa kwa maoni ya Mabaraza ya Katiba ni kuhusu muundo wa majimbo ya ubunge, kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika rasimu ya awali, ilipendekezwa katika Ibara ya 105 (3) kwamba;…kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa jimbo la uchaguzi.
Hoja inayoibua utata hapo ni kwamba, kwa sababu, kwa mfano, Rais wa Tanganyika (Tanzania Bara) anaweza kugeuza wilaya kuwa mkoa na kwa hiyo akaweza kuongeza idadi ya majimbo ya ubunge na kwa sababu, Rais wa Zanzibar anaweza kubadilisha shehia kuwa wilaya ili kuwa na idadi kubwa ya majimbo na hatimaye idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Muungano, kwa sababu zozote zile ikiwamo kuwa na idadi kubwa ya wabunge kwa ajili ya kulinda maslahi ya upande anaoongoza, kigezo cha mkoa au wilaya kuwa jimbo la uchaguzi kinapoteza mantiki.
Sasa inaweza kupendekezwa, kuwapo kwa idadi mahsusi ya majimbo ya uchaguzi na hasa kwa kigezo cha idadi ya usawa kati ya Bara na Zanzibar, yaani asilimia 50 ya wabunge wa Bunge la Jamhuri watoke Bara na wengine asilimia 50 ya idadi ya wabunge wa Bunge hilo watoke Zanzibar, bila kujali ukubwa wa nchi hizo Washirika.
Ulinzi na Usalama
Katika rasimu ya sasa, kwa mfano Ibara ya 224, inaeleza; kutakuwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ambaye atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama wa Taifa. Baraza hilo la Ulinzi na Usalama wa Taifa linatajwa katika 221(1) kuundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano; Makamu wa Rais; Rais wa Tanzania Bara; Rais wa Zanzibar; Waziri mwenye dhamana na ulinzi; Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi, Waziri mwenye dhamana na mambo ya nje; Waziri mwenye dhamana na usalama wa taifa; waziri mwenye dhamana ya fedha; Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania; Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na mapendekezo ya Mabaraza ya Katiba, eneo hili linaweza kufanyiwa mabadiliko ili wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini wateuliwe na Rais lakini wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfano unaopendekezwa hapa ni kama wa sasa wa namna Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyopatikana, ambaye jina huteuliwa na Rais, kisha jina lake kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa au hata kukataliwa.
Chama kuweza kufukuza mbunge
Kwenye rasimu ya awali, kuhusu uwajibikaji wa wabunge katika Ibara ya 123(2) na (3) zinagongana kimantiki. Wakati ibara ya 123(2) ikieleza; Mbunge aliyependekezwa na chama cha siasa, hatapoteza ubunge wake ikiwa mbunge huyo atafukuzwa au kuvuliwa uanachama wa chama chake na Ibara ya 123(3) inaeleza; endapo mbunge, kwa ridhaa yake atajiondoa au kujivua uanachama kutoka chama chake cha siasa, mbunge huyo atapoteza sifa za kuwa mbunge na atasita kuwa mbunge.
Kutokana na mgongano huo wa kimantiki, mabadiliko yanatajwa kuweza kufanyika kwamba chama kinapomvua uanachama mbunge husika basi na ubunge wake ukomee hapo. Katika hili, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, inaelezwa vyama vyote vikubwa vya siasa nchini vimekubaliana na kuna nafasi kubwa ya kupitishwa.
Eneo jingine ambalo litafanyiwa marekebisho kwa mujibu wa vyanzo vyetu hivyo vya habari ni namna ya kumwondoa mbunge asiyejali maslahi ya wananchi wake kabla ya muda wake wa muhula kuhitimishwa.
Katika rasimu ya awali, ibara ya 124 (1) inaeleza, bila kuathiri masharti ya Ibara ya 123 ya Katiba hii, wananchi watakuwa na haki ya kumwondoa mbunge wao madarakani, endapo mbunge atafanya mojawapo ya yafuatayo; (a) kuunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume cha maslahi ya wapiga kura au kinyume cha maslahi ya taifa.
Katika kipengele hiki, uzoefu wa ushindani wa uvunaji, usafirishaji na matumizi ya gesi ya Mtwara unatumika kujenga hoja ya kuondoa kipengele hiki. Chanzo chetu cha habari kinaeleza; “Kwa mfano, Mtwara maslahi ya taifa yanaonyesha gesi hiyo isafirishwe na kuhudumia taifa zima lakini wananchi wa jimbo mojawapo kwa mfano walikuwa wanasema gesi hiyo isisafirishwe, kama mbunge wa jimbo husika atasema isafirishwe maana yake hazingatii maslahi ya wananchi wake kwa hiyo afukuzwe….hii haijakaa sawa.
“Kwa hiyo, kipengele hiki kinaweza kufanyiwa marekebisho bila kupora haki ya wananchi kumwondoa mbunge wao. Kwa mfano, inaweza kuelezwa katika Katiba wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kwa mujibu wa sheria itakayotungwa na Mbunge,” anaeleza mtoa habari wetu kutoka serikalini.
Mchakato unaendelea
Kwa sasa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ipo katika hatua ya uchambuzi wa maoni yaliyotokana na mikutano ya Mabaraza ya Katiba na baada ya hapo, itaandika rasimu ya Katiba Mpya awamu ya pili ambayo itakabidhiwa kwa Rais ambaye ataitisha Bunge la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na baada ya hapo, rasimu hiyo itawasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Bunge la Katiba linaweza kurekebisha au kuongeza masuala mbalimbali katika rasimu hiyo y awamu ya pili itakayowasilishwa kwao na baada ya kuridhika, na rasimu hiyo kuwasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa hizo kura za maoni, wananchi watapiga kura ya maoni kwa njia ya kujibu swali la ndiyo kama wanaikubali au hapana kama hawaitaki rasimu hiyo.
Mchakato wa upigaji na usimamizi wa kura ya maoni utaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo kwa sasa inaongozwa na Jaji Damian Lubuva.
..- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/mageuzi-tena-katiba-mpya#sthash.kX75XLfW.dpuf

Thursday, 24 October 2013

Mapendekezo ya wapinzani mazito

                                                                                                                                                                                                        WAREJESHA MENGI YALIYOKATALIWA NA CCM
Na Josephat Isango
SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete, kukutana na viongozi wa vyama vyenye wabunge kuzungumzia upungufu katika muswada wa marekebisho ya sheria ya sheria mabadiliko ya katiba, viongozi wa vyama hivyo wametoa mapendekezo mazito.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa mapendekezo hayo mengi ni yale yaliyokataliwa na wabunge wa Chama Cha mapinduzi (CCM) wakati wakipitisha muswada huo bungeni.
Mapendekezo hayo ya wapinzani yanaonekana yatazua mtafaruku mkubwa bungeni iwapo serikali itaamua kuyapeleka, hasa baada ya Rais Kikwete kuwataka wapinzani kuandaa mapendekezo ya kina ya upungufu wa sheria hiyo na wayawasilishe haraka iwezekanavyo serikalini ili iunde kamati maalumu ya kujadili upungufu.
Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa viongozi hao wa vyama vya upinzani waliokutana Oktoba, 17, 2013 walijadili na kutoa mapendekezo kadhaa mbayo wameyawasilisha serikalini kama walivyoagizwa na Rais Kikwete.
Mapendekezo
Wapinzani hao wanapendekeza kifungu 22 (2A) cha sheria kama ilivyo sasa kifutwe kabisa, na kwamba wajumbe waliotajwa katika kifungu cha 22 (1) (c) watateuliwa na taasisi watakazowakilisha, na kwamba idadi ya wajumbe hao iongezeke kutoka 166 kwa mujibu wa sheria ya sasa hadi 438.
Wamependekeza kuwa makundi yote yanayostahili kuwakilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba yatafafanuliwa na idadi ya wawakilishi wao kuwekwa wazi katika jedwali la pili la sheria.
Pendekezo jingine linataka kuzingatia usawa wa kijinsia, kifungu kidogo (2b) kifutwe na kuandikwa upya “uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu chini ya kifungu kidogo (1) ( c ) utazingazia kanuni za sifa na zuoefu wa watu walioteuliwa, na idadi ya wajumbe wanawake haitapungua theluthi moja ya wajumbe walioteuliwa kutoka katika makundi hayo.”
Kwa kuzingatia dhana ya usawa wa wabia sawa wa Muungano bila kujali ukubwa wa kila nchi, idadi ya watu wake na kuzingatia haja ya kujenga muafaka na maridhiano ya kisiasa kuhusu muungano wetu, viongozi wa vyama, wamependekeza kama ilivyokuwa katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Katiba ya Mabadiliko ya Katiba, kutakuwa na uwakilishi sawa katika Bunge Maalumu kati ya washiriki wa Muungano.
Vile vile wamependekeza kuwa kifungu 22(1) kirekebishwe kwa kuongeza aya ya (d) isomeke “wajumbe wa Bunge Tume ambao hawatakuwa na haki ya kupiga kura katika Bunge Maalumu yaani watakuwa wajumbe kwa nafasi zao ‘ex officio’ kwenye Bunge Maalumu.”
Hivyo kifungu (c) cha zamani za 37 (1) kirejeshwe ili kuwezesha uwepo wa tume hadi baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa, na idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu itakuwa 908, kwa mchanganuo wa 357 Bunge la Jamhuri, 81 Baraza la Wawakilishi, na 438 watakaoteuliwa na makundi tajwa katika kifungu 22(1) (c) na wajumbe 32 ‘ex officio’ wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia wamependekeza kwamba kifungu 26 (4) na (5) vifutwe badala yake kifungu (3) kirekebishwe ili kuweka wazi kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu wataendelea na majadiliano hadi kifungu husika kitakapoungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo kutoka Zanzibar.
Mapendekezo hayo pia yamesema kwa jinsi sheria ilivyopitishwa kuzungumzia nafasi ya kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu sifa zake ni lazima mgombea awe na Shahada ya Chuo Kikuu kilichotambulika na uzoefu na ujuzi uliothibitika wa kuongoza mihadhara na mabaraza, kifungu hicho kitakuwa cha kibaguzi miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu ambao wengine hawajahitimu vyuo vikuu hivyo kukosa sifa ya kuteuliwa au kuchaguliwa.
Hata hivyo kwa kuwa kifungu hicho hakikutoa tafsiri ya neno mihadhara au mabaraza na mthibitishaji mwenyewe kutotajwa, wamependekeza kuwa mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu awe na sifa ya kugombea na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, na viongozi hao wachaguliwe badala ya kugombea.
Wapinzani wataka ushirikiano
Wakati Tanzania Daima Jumatano ikidokezwa kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo serikalini, viongozi wakuu wa vyama vya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UPDP, wametaka mchakato wa kupata katiba mpya ulenge maslahi mapana ya nchi na wananchi kuliko kufikiria maslahi ya vyama au makundi fulani katika jamii.
Viongozi hao walikutana na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, ambapo Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), James Mbatia alisema kutokana na umuhimu wa upatikanaji wa katiba mpya, vyama vimedhamiria kuhakikisha kuwa mchakato wa katiba unafanyika kulenga maslahi mapana ya nchi.
“Sote kwa pamoja tunatambua tofauti mbalimbali ambazo ziko baina ya vyama vyetu kiitikadi na kimtizamo, lakini tunachukua jukumu kwa nia safi kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata katiba wanayoitaka,” alisema.
Vyama hivyo pia kwa tamko la pamoja vimesema vilikubali wito wa Rais Jakaya Kikwete alioutoa kupitia hotuba yake kwa Watanzania Septemba 4 na walipokutana naye Oktoba 5, mwaka huu, vimepongeza juhudi za rais kuhakikisha mchakato wa katiba unakwenda mbele ukihusisha wadau wote na wale walioachwa wasikilizwe kwa lengo la kuwaleta pamoja.
Mbatia alisema vyama vyao vinampongeza Rais Kikwete kwa nasaha zake kwa njia ya mazungumzo wakisema ni sahihi na ahadi ya kutoa ushirikiano mkubwa katika kila hatua ya mchakato wa katiba akiwa na lengo la kuona katiba inakuwa ya wote.
Kwa mujibu wa tamko hilo la TCD mkutano huo wa Ikulu na vyama sita vyenye wabunge na rais vilikubaliana kushirikisha vyama vingine 15 visivyo na wabunge kuandaa mapendekezo ya kina ya upungufu wa muswada ambao sasa umekuwa sheria na kupendekeza marekebisho maalumu na kuyawasilisha haraka iwezekanavyo.
Vile vile walipendekeza kuwa baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo serikalini ili serikali iunde kamati maalumu ya kukutana na vyama hivyo kujadili kwa kina juu ya upungufu katika sheria husika na kukubaliana juu ya maeneo muhimu yanayohitaji marekebisho kwa lengo la kuufanya mchakato wa katiba kuwa shirikishi.
Mbatia alisema kulingana na makubaliano waliyofanya na rais, baada ya pande zote kukutana serikali itaandaa hati ya dharura ili sheria husika irejeshwe bungeni haraka katika mkutano wa Bunge unaoanza wiki ijayo.
Alisema kuwa katika mjadala wa kitaifa, taasisi mbalimbali katika umma, makundi ya kijamii na wadau wote muhimu wahusishwe ili kutengeneza maridhiano ya kitaifa.
Mbatia alitoa wito kwa niaba ya vyama vyote vya siasa kuwaomba Watanzania wote hususani wabunge waunge mkono juhudi hizo za vyama na Rais Kikwete kuhakikisha mchakato wa katiba mpya unakuwa shirikishi utakaolinda maslahi mapana ya taifa.
Tamko hilo lililosomwa na Mbatia lilikuwa limesainiwa na Philip Mangula (CCM), Freeman Mbowe ambaye aliwakilishwa na Dk. Slaa (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema aliyewakilishwa na Nancy Karia (TLP), John Cheyo aliyewakilishwa na Isaac Cheyo (UDP) na Fahmi Dovutwa wa UPDP kwa niaba ya vyama visivyo na wabunge.
Mangula agoma kuisema CCM
Baada ya tamko hilo, wakati wa maswali, waandishi walitaka kujua kauli ya CCM kwani wamekuwa wakisisitiza kuwa mchakato huo ulikuwa huru na ulipitia hatua zote, kama wapo tayari kufanya mabadiliko kama alivyopendekeza rais na vyama vyenye wabunge.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula aligoma kuzungumza kwa undani na kusema: “Mimi sio mbunge siwezi kuwasemea wabunge.”
Kauli hiyo ilisababisha Mbatia kuanza upya kuwataka waandishi na Watanzania waache tofauti zao, waache kauli zote zilizowahi kutolewa na kutoa fursa mpya ya kuanza mchakato kwa njia ya amani kwa maslahi mapana ya taifa.
Chanzo – Tazania daima

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHESHIMIWA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI KUZUNGUMZIA MIAKA MITATU YA UTENDAJI WA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANAZIBAR AWAMU YA SABA HUKO KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HOTELI YA ZANZIBAR OCEAN VIEW – TAREHE 24 OKTOBA, 2013

                                                                                                                                                                                                       
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuweka katika hali ya uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia utendaji na majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika serikali yetu, hasa hii ya awamu ya saba ya uongozi ambayo imetimiza muda wa miaka mitatu sasa.
Mkutano huu ni mwendelezo wa uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya saba yenye mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, unaowataka viongozi wa juu na taasisi zote za serikali wawe wanajiwekea utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kila muda waliojipangia.
Pili natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari mliotenga muda wenu na kuja kuhudhuria kwa wingi na kuja kuitikia wito wetu wa kutusikiliza, ambapo baadaye mtapata fursa ya kuuliza, ili mpate ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii ya Wazanzibari kwa ujumla.
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Katika hotuba yangu nakusudia kugusia angalau kwa ufupi baadhi ya mambo muhimu yanayoendelea na kujitokeza katika nchi yetu hivi sasa, na katika siku za hivi karibuni. Kisha nitajikita zaidi kutoa maelezo kwa yale maeneo yaliyowekwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kama mjuavyo ofisi hii naiongoza mimi nikisaidiwa na Waziri wa Nchi makini, mchapakazi na muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji. Waziri wa Nchi ndiye msimamizi wa siku kwa siku wa shughuli zote za ofisi hii. Lakini pia nina Katibu Mkuu makini mjuzi na mzoefu wa taratibu za serikali, ambaye ndiye anayenishauri mimi na Waziri wa Nchi kuhusu masuala ya kitaalam, mbali kuwa Mtendaji Mkuu wa shughuli zote zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar Shajak akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii. Wote hao nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa, muda wote huu.
Waheshimiwa waandishi wa habari
Katika kipindi hiki cha muda wa miaka mitatu tunaendelea kushuhudia nchi yetu ya Zanzibar ikiendelea kuwa katika hali ya amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi wake. Hali hii imetuwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yetu Serikalini na kwa wananchi wote katika hali ya utulivu.
Kutokana na hali hiyo ndio maana hivi sasa ushiriki wa wananchi wote katika shughuli za kimaendeleo, kijamii na kisiasa umeendelea kuwa mkubwa, ambapo wamekuwa wakiiunga mkono Serikali yao katika mambo yote, ikiwemo yale mambo muhuimu ya Kitaifa tunayoendelea nayo hivi sasa. Kati ya mambo hayo ni Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yanafikia kilele chake Januari 12 mwakani. Ni matumaini yangu kuwa wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, watashiriki kwa ukamilifu katika maadhimisho hayo.
Waheshimiwa Wana Habari
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Saba yenye mfumo wa Kitaifa imeendelea kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika nyanja zote, zikiwemo za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Katika kipindi hichi cha miaka mitatu ya Serikali ya Mapinduzi yenye mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yapo mafanikio kadhaa yaliyopatikana. Kwanza ni kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa za kuimarisha uchumi wetu, lengo likiwa ni kuwaongezea kipato wananchi wetu.
Yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Saba. Miongoni mwa hatua hizo ni kupandisha bei ya karafuu. Wakulima wetu wamepata afueni kubwa ya bei, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma. Hali hiyo imewapa mwamko mkubwa wakulima wetu, lakini pia kuwa na mwamko wa kuziuza karafuu zao kunakohusika. Hadi jana jumla ya tani 1,540 tayari zimenunuliwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 21,560,805,000.
Kupandishwa bei ya karafuu kumewafanya wananchi wengi, hasa katika vijiji vya Pemba, kujenga nyumba bora zaidi na hivyo kuwafanya kuishi katika mazingira bora.
Halikadhalika, Serikali imechukua hatua za makusudi kabisa kumuendeleza mkulima, mfugaji na mvuvi. Katika hili Serikali imepunguza kwa kiwango kikubwa bei za pembejeo za kilimo, kama mbolea, dawa za kuulia magugu na wadudu, mbegu na kupunghuza gharama za kulimia kwa kutumia matrekta.
Serikali pia imechukua hatua za kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji, kwa nia ya kutumia njia za kisasa za ukulima na ufugaji. Jumla ya wavuvi wadogo 59 wamepelekwa China kujifunza njia za kisasa za ufugaji wa samaki. Pia Maafisa watatu wa Wizara ya Uvuvi na Ufugaji walipelekwa nchini Korea maalum kusomea ufugaji wa samaki.
Hatua hizi zote lengo lake ni kuwasaidia wananchi. Pia tumeona kwamba katika dhana hiyo hiyo ya kujaribu kuleta huduma kwa wananchi, serikali imekuwa ikijitahidi sana kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapata unafuu. Serikali pamoja na ufinyu wa bajeti yake inahakikisha kuwa zile dawa ambazo ni muhimu “essential drugs” zinapatikana katika hospitali zetu.
Kwa upande wa madaktari bado tuna upungufu, lakini juhudi za kuwasomesha watu wetu zinaendelea, vijana kadhaa wanapata mafunzo katika skuli ya udaktari ya Zanzibar yaani ‘Zanzibar Medical School’ na vijana hao watakapomaliza mwaka huu au mwakani, tutapata kwa mpigo mmoja madaktari 34. Hatua hiyo itaweza kupunguza sana pengo la upungufu wa madaktari katika nchi yetu.
Vile vile juhudi zinachukuliwa kuwataka wale madaktari ambao wanasoma nchi nyengine warudi, ili tumalize kabisa tatizo la uhaba wa wataalamu wa kada hii.
Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa vile vile imekuwa ikipambana na tatizo la upungufu wa maji kwa kushirikiana na wahisani na makampuni mengine ya nje. Tumekuwa na miradi mikubwa ya maji katika nchi na bado jitihada zinafanyika katika kupunguza tatizo hili.
Kwa mfano hivi sasa tumekubaliana na nchi ya Ras El Khaima kutusaidia katika suala la kuchimba visima kwa mintaaraf ya kupunguza tatizo la uhaba wa maji.
Tatizo la Umeme limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mradi wa MCC unaofadhiliwa na Marekani. Tunafahamu bado umeme unakatika katika kutokana na sababu tafauti. Lakini azma ya Serikali ni kulimaliza tatizo hili kabisa.
Ukiangalia sekta ya elimu, hivi sasa watoto karibu wote waliofikia umri wa kwenda skuli wanapatiwa fursa hiyo. Hivi sasa takriban kila Shehia ina angalau skuli moja, na zile Shehia chache ambazo bado hazijawa na skuli juhudi zinaendelea kufanywa, ili kuhakikisha kuwa kila Shehia inakuwa na skuli.
Serikali inaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuwekeza katika sekta mbali mbali, miradi ya kiuchumi imekuwa ikiongezeka. Kwa mfano mwaka jana pekee jumla ya miradi sita mipya na programu 18 mpya zilianzishwa. Ni azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushirikiana na sekta binafsi kuzidi mkuleta maendeleo.
Jengine ni kwamba tumeweza kuongeza maslahi ya wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika mwaka 2010/2011 mishahara ya wafanyakazi wa Serikali iliongezwa. Huko nyuma ilikuwa muda mrefu hawajapata nyongeza zao wala kupandishwa vyeo. Kwa kuwa katika mwaka 2011/2012 Serikali ilishughulikia suala la kupanga “Scheme of service”, kwa Wizara na Taasisi zote za Serikali ili kila mmoja ajijue yuko wapi. Lengo la Serikali ni kupandisha tena mishahara katika mwaka huu wa fedha 2013/2014.
Mengine ni Serikali hii kuona umuhimu wa sekta ya mifugo na uvuvi, Mhe. Rais ameunda Wizara Maalum inayoshughulikia Mifugo na Uvuvi. Kwa vile bado tuna changamoto, hatujaendeleza uvuvi katika bahari kuu na bado hatujawaendeleza ipasavyo wakulima wetu na hasa wafugaji, Wizara imepewa jukumu hilo kuona kuwa sekta ya uvuvi inakua sambamba na sekta ya ufugaji.
Pia tumefanya mabadiliko ya hapa na pale, sasa hivi sasa ipo Wizara maalum inayoshughulikia utalii, ambayo inaelekeza azma ya Serikali kuifanya sekta ya utalii kuwa sekta kiongozi katika uchumi wa Zanzibar. Chini ya Uongozi wa Rais Shein Serikali imebuni dhana ya utalii kwa wote, kwa min ajili ya kuwawezesha Wazanzibari wote washiriki katika kuundeleza utalii na kuweza kupata manufaa kutokan na utalii wenyewe.
Mafanikio haya pamoja na juhudi nyengine tunazoendelea kuzichukua, ikiwemo za kuliinua zao la Karafuu kwa kujali zaidi maslahi ya wakulima, yametuwezesha kukuza matumaini ya kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar ambao umeweza kukua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011hadi asilimia 7.0 mwaka jana.
Hayo ni kwa ufupi tu, lakini yapo mafanikio mengine makubwa ambayo yamepatikana katika kipindi hicho na hasa chini ya Serikali hii yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
Changamoto
Lazima tukiri kuwa pamoja na mafanikio hayo makubwa bado tunazo changamoto ambazo tunapaswa tusizifumbie macho.
Kwa mfano ni kweli tumeeneza skuli, lakini kwa sababu yale mahitaji ya elimu au mahitaji ya skuli ni makubwa, ukweli ni kwamba ule ubora wa elimu bado haujafikiwa kwa kiwango cha kuridhisha. Zamani darasa lilikuwa na wanafunzi kati ya 24 na 30, lakini sasa hivi si ajabu kukuta darasa lina wanafunzi 80 hadi 100. Sasa katika hali kama hiyo, ukweli mwalimu anakuwa na kazi pevu. Pia kuna upungufu wa walimu wa Hesabu, Sayansi, Kingereza na Jographia. Halikadhalika tuna upungufu wa zana za kufundishia, hasa kwa masomo ya Sayansi.
Vile vile kwa sababu ya kupanuka kwa huduma, uwezo wetu wa kiuchumi bado ni mdogo, hata huduma za afya hazijawa za kutosheleza. Wakati mwengine tunakabiliwa na upungufu wa dawa hasa dawa ambazo ni muhimu zaidi, upungufu wa wafanyakazi hasa madaktari na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya, kuna upungufu wa zana au vitendea kazi vya kutibia, Hizi ni baadhi ya changamoto ambazo tunapambana nazo.
Serikali katika awamu zote imekuwa zikichukua hatua mbali mbali katika kupunguza matatizo hayo ambayo yanatukabili.
Changamoto nyengine ambayo imejitokeza katika siku za hivi karibuni katika nchi yetu ni hili suala la vitendo vya hujuma, ikiwemo watu kumwagiwa tindikali na hujuma za aina nyengine.
Napenda kusema kuwa haya ni mambo ya kusikitisha kabisa, kwa sababu sisi Wazanzibari tumezoweya kuwa nchi yetu ni nchi ya amani.
Haya mambo ya raia kutumia risasi au mashambulizi kwa kutumia tindikali kwa Zanzibar ni mageni. Sisi ustaarabu wetu Wazanzibari, Utamaduni wetu na dini zetu, masuala haya ya ukatili na hujuma sio mambo yetu kabisa.
Mambo haya yananisononesha na kunisikitisha sana, hasa kipindi hiki ambacho tuna maridhiano katika nchi. Kama mambo haya yangetokea wakati ule wa tofauti za kisiasa, tungesema ni hujuma za kisiasa, lakini leo tunayo serikali ya pamoja. Kila chama ambacho kina viti katika Baraza la Wawakilishi kinashirikishwa katika serikali hii ya Umoja wa Kitaifa. Suala la kujiuliza kwanini jambo hili lizuke sasa? Ukweli ni mtihani mkubwa kwetu.
Sisi Wazanzibari tumekuwa ni watu wa dini mbali mbali kwa muda mrefu. Tokea enzi na enzi kiwango cha uvumilivu wa kidini ni kikubwa Zanzibar, mimi nadhani hakuna duniani kuliko Zanzibar. Hapa inajulikana kabisa kwamba asilimia 98 ni Waislamu. Lakini lazima wananchi wajue kwamba Ukristo katika Afrika Mashariki na Kati, mlango wake uliopitia kwenda huko ni Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Jambo jengine zito linalotukabili katika kipindi hichi cha Serikali ya Awamu ya Saba ni mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchakato huo unatokana na dhana na fikra za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Yeye kwa busara zake ameona kwamba sasa hivi miaka 50 imepita tangu Uhuru wa Tanganyika. Hivyo tunahitaji kuandika Katiba Mpya ambayo itawashirikisha wananchi wenyewe.
Kwa hivyo mimi nimpongeze kwa dhati Rais Jakaya Kikwete kuona umuhimu huu wa kuwashirikisha Watanzania wenyewe kuandika Katiba mpya. Yeye alisema wazi kwamba baada ya miaka 50 lazima tuwe na katiba ambayo inakidhi mahitaji ya wakati huu. Katiba ambayo angalau itatuchukua miaka 50 mingine. La msingi zaidi ni kuwa wananchi washirikishwe kikamilifu.
Ni uamuzi mzuri aliochukua Rais ingawa kuna changamoto zake. Hivi sasa tumemaliza hatua ya Tume kukusanya maoni ya wananchi, pamoja na ili hatua ya Mabaraza ya Katiba kuchambua Rasimu ya Kwanza ya Katiba hiyo. Hatua inayoendelea hivi sasa ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuendelea kuchambua maoni ya Mabaraza hayo, na hatimaye iweze kupatikana rasimu ya Pili ambayo ndiyo itapelekwa kwa Rais na yeye Rais kuiwasilisha kwenye Bunge la Katiba.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Hata hivyo, pamoja na azma njema ya kuifanya nchi yetu iwe na Katiba mpya ifikapo mwakani, lazima tukiri kwamba changamoto nyingi zinaendelea kujitokeza katika suala hili.
Waandishi wa habari mnakumbuka mfululizo wa matukio yaliyojiri, hasa baada ya Serikali kuamua kuwasilisha Bungeni mswada wa kurekebisha sheria ya Mabadiliko ya Katiba, pamoja na kadhia nzima ya vurugu zilizojitokeza Bungeni hivi karibuni na kusababisha baadhi ya Wabunge wa Upinzani, wakiwemo viongozi wa Kambi hiyo, kulalamika kutotendewa haki na kuamua kutoka nje.
Baada ya yote yaliyotokea, Rais wa Jamhuri ya Muungano ameona busara ya kukaa meza moja na viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyo sajiliwa, ili kuyajadili kwa upeo wake mambo yanayo lalamikiwa. Kati ya mdai ya msingi ni madai kwamba upande wa Zanzibar haujashirikishwa katika mabadiliko ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mambo mengine mengi, ikiwemo muundo na upatikanaji wa Wabunge wa Bunge Maalum, wasiokuwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Matarajio yangu ni kwamba vikao vilivyofanyika na maazimio ya vikao hivyo, kati ya Rais na Viongozi wa vyama vya siasa yataweza kuzaa maafikiano mema, ili hatua zinazofuata katika suala zima la kuandika Katiba mpya ziweze kuendelea kwa amani na utulkivu na matarajio ya wananchi walio wengi yaweze kufikiwa.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Baada ya kueleza kwa kifupi baadhi ya masuala mabli mbali yanayogusa nchi yetu kwa jumla, sasa naomba niruhusuni kuingia moja kwa moja katika utendaji wa majukumu ya Idara na Tume zilizopo katika Ofisi yangu. Hizo ni Tume ya Ukimwi Zanzibar, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Idara ya Mazingira na Idara ya Watu Wenye Ulemavu.
Tume ya Ukimwi
Tume hii ina umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa ustawi na afya za wananchi wa Zanzibar. Ndiyo maana ikapewa majukumu makuu ya kuhakikisha kwamba Sera na Mikakati ya Taifa ya kupiga vita ukimwi zinaandaliwa na kutekelezwa ipasavyo, nia ikiwa ni wananchi wetu wabaki salama na wasiambukizwe Virusi vya Ukimwi.
Mambo mengine yanayotekelezwa kupitia Tume hii ni kutafuta rasilimali zitakazo tumika katika kutekeleza Muitikio wa Kitaifa wa kupambana na Ukimwi, kuimarisha uwezo wa wadau katika kufanyia kazi program za ukimwi pamoja na kuratibu shughuli zao. Aidha majukumu mengine ya Tume ni kushajiisha utoaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu walioathirika na kuathiriwa, kufuatilia na kutathmini ufanisi wa mapambano dhidi ya ukimwi, pamoja na kutoa taarifa zote zinazohusiana na Ukimwi.
Mafanikio makubwa yameweza kupatikana chini ya utendaji wa Tume hii.
Kwa mfano mwaka jana Tume hii iliweza kusaidia Shehia 22 kuibua Mipango Mkakati ya kukabiliana na Ukimwi. Aidha, katika juhudi za kuongeza uwezo wa program za habari na kuchochea mabadiliko ya tabia katika masuala ya Ukimwi nyumba kadhaa za makaazi ya vijana walioacha dawa za kulevya ‘Sober Houses’ zimesaidiwa kwa kununuliwa televisheni na radio. Dada poa wapatao 307 na kaka poa 38 na vijana 271 wanaojidunga sindano waliweza kufikiwa kupatiwa taaluma kupitia waelimishaji rika.
Pia taasisi za Kidini zinaendelea kuhamasisha waumini wao kupitia katika mikusanyiko ya kidini juu ya mbinu muafaka za kuzuia maambukizi ya ukimwi, kusaidia upatikanaji wa taarifa za afya ya uzazi na usawa wa kijinsia.
Tukiwa tumo katika utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kupambana na Ukimwi, Mapitio ya Sheria ya Tume ya Ukimwi Nam.3 ya mwaka 2002 yamefanyika na rasimu ya mswada wa marekebisho yake yanatarajiwa kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi karibuni.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio katika juhudi hizo, bado changamoto kubwa inatukabili, changamoto hiyo imejitokeza wazi baada ya Utafiti wa mwisho uliofanywa juu ya Virusi vya Ukimwi na Malaria kuonesha kwamba kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Tanzania kwa mwaka 2011/2012, kwa upande wa Zanzibar kimepanda kutoka asilimia 0.6 hadi asilimia 1. Taarifa hizi sio nzuri kwetu na nguvu ya pamoja inahitajika kuhakikisha kwamba maambukizi zaidi yana zibitiwa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya
Kama mnavyoelewa, Zanzibar kama ilivyo kwa nchi nyengine Duniani, miongoni mwa changamoto kubwa zinazojitokeza ni kuwalinda vijana wake wasiathiriwe kwa matumizi ya dawa za kulevya, lakini pia kukomesha uingizwaji na biashara ya dawa hizo kwa jumla.
Suala hili ni changamoto kubwa kwetu. Juhudi kubwa tunazichukua ikiwemo, kuhakikisha Sheria ya Dawa za Kulevya inatekelezeka, mpango wa utekelezaji wa sheria hiyo ‘Road Map’ tayari imeandaliwa. Katika mwaka uliopita jumla ya watu 22 wamekamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya, kati yao wanaume ni 21 na mwanamke mmoja, ambapo jumla ya kesi 22 zipo mahakamani. Wizara yangu tayari imeandaa rasimu ya kanuni ya Sheria ya Dawa za Kelevya, ili kuona sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo.
Aidha, vipindi vya redio na televisheni vilivyolenga kuinua mwamko wa jamii juu ya athari za dawa za kulevya vimerushwa hewani kupitia vyombo mbali mbali vya habari. Vile vile kampeni kubwa inafanyika maskulini, ambapo kwa mwaka jana wanafunzi wapatao 6,270 Unguja na Pemba walipatiwa elimu juu ya athari za dawa za kulevya.
Vile vile kwa kutambua mchango wa taasisi zisizokuwa za kiserikali, katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Tume imezipatia ruzuku nyumba tisa za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober Houses), kwa ajili ya kusaidia mahitaji yao mbali mbali.
Jambo muhimu la kuzingatiwa katika kupiga vita dawa za kulevya Zanzibar na kwengineko, ni kuendelea kutoa elimu, ili watu wote wakatae kutumia dawa za kulevya. Kwani itakapofika pahala ambapo hakuna mtu anayetaka kutumia, ni wazi kwamba hata yule muingizaji naye atakuwa haingizi tena kwa sababu hakuna soko.
Waheshimiwa Wana Habari
Idara ya Mazingira
Hii nayo ni Idara muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa wananchi na uendelevu wa nchi yao katika suala zima la kuhakikisha mazingira hayaharibiwi.
Kati ya majukumu makubwa yanayotekelezwa na Ofisi yangu, kupitia Idara hii ni kukusanya na kuhifadhi taarifa za kimazingira, kwa azma ya kusaidia utayarishaji na utekelezaji wa mipango na miradi ya kimazingira. Vile vile kuhamasisha wananchi na wadau wote kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa jamii yetu.
Mbali na hayo majukumu mengine makubwa yanayosimamiwa chini ya Idara hii ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kimaendeleo haziwi chanzo cha uharibifu wa mazingira. Mwaka jana tuliweza kukagua jumla ya miradi 65 ya mahoteli, miradi 15 ya uwekezaji imefanyiwa tathmini ya Athari za Kimazingira. Aidha, kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi Pemba kimefanyiwa ukaguzi wa kimazingira na ripoti yake imekabidhiwa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, ikiwemo mapendekezo yaliyotolewa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya tabia nchi ni eneo jengine ambalo nchi yetu inalipa umuhimu wa kipekee, hasa kwa maumbile ya nchi yetu ikiwa ni ya visiwa vidogo. Kwa kawaida nchi kama hizi huathiriwa sana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Zanzibar imeendelea kuwa mshirika muhimu katika umoja wa nchi za visiwa katika Bahari ya Hindi (ISLANDS), na imekuwa ikinufaika kwa njia mbali mbali na ushiriki huo katika kuandaa na kutekeleza mikakati na program tafauti za kukabiliana na athari hizo na kuhifadhi mazingira kwa jumla, pamoja na kwamba hadi sasa sio mwanachama kamili wa jumuiya hiyo.
Miongoni mwa mikakati yetu Zanzibar katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ni suala hilo kulihusisha moja kwa moja katika ngazi za Shehia, ili wananchi wenyewe wahusike kikamilifu. Kamati 10 za majaribio za usimamizi wa ukanda wa pwani tumezisaidia kuandaa mipango ya utekelezaji ya usimamizi wa mazingira katika maeneo yao. Miongoni ya Shehia hizo ni Nungwi, Chwaka, Nyamanzi na Mtende.
Kazi ya kuyatambua maeneo yaliyoingiliwa na maji ya chumvi na hivyo kuathiri shughuli za kimaendeleo, kijamii na kiuchumi, ikiwemo kilimo kote Zanzibar inaendelea. Hatua hii itatuwezesha kujua ukubwa wa tatizo na hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.
Ofisi yangu imejikita zaidi kuhakikisha kwamba, Sera, Sheria na Kanuni za Mazingira zinatekelezwa. Kwa mfano kwa mwaka jana jumla ya operesheni 117 zimefanyika Unguja na Pemba na watu 33 walikamatwa na kuhukumiwa kwa faini ya TZS 3,280,000 kwa jumla. Operesheni za kudhibiti mifuko ya plastiki zinaendelea. Mwaka jana kilo 670 za mifuko ya plastiki ziliteketezwa katika eneo la Maruhubi.
Matarajio yetu ni kupata mafanikio makubwa zaidi katika utekelezaji wa majukumu yetu, hasa baada ya Serikali kuidhinisha Sera mpya ya Mazingira na Mpango wa Utekelezaji wa Usimamizi wa Mazingira kuandaliwa kwa mujibu wa Sera hiyo Mpya ya Mazingira.
Waheshimiwa Wana Habari
Idara ya Watu Wenye Ulemavu
Idara hii yenye majukumu ya kuratibu masuala mbali mbali ya watu wenye ulemavu Zanzibar, pia ina umuhimu mkubwa na wa kipekee katika kuhakikisha haki sawa inapatikana miongoni mwa wananchi wote wa Zanzibar bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote ile.
Katika kuhakikisha tunafanikisha hilo la kuleta usawa na kuona watu wenye ulemavu wanapata fursa zote, ikiwemo za kielimu, kiuchumi na kushirikishwa kikamilifu katika mambo yote yanayohusu nchi na jamii, mkazo mkubwa tumeuweka katika kufanya kazi kwa pamoja na jumuiya zote zilizopo za Watu Wenye Ulemavu.
Miongoni mwa Jumuiya hizo ni Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), Chama cha Viziwi (CHAVIZA), Umoja wa Watu Wenye Ulemavu (UWZ), Jumuiya ya Maalbino Zanzibar (JMZ), Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu (JUWAUZA), Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (ZADA), Chama Maalum cha Olympic kwa Watu Wenye Ulemavu (SOZ) na jumuiya nyenginezo.
Hata hivyo lazima tukiri kwamba tuna changamoto kubwa ya uhaba wa fedha, visaidizi na nyenzo nyengine kwa ajili ya kuweza kutosheleza mahitaji yote kwa wenzetu Wenye Ulemavu.
Kutokana na hali hiyo, Serikali, taasisi zisizokuwa za kiserikali na jamii kwa jumla, hatuna budi tushirikiane kwa pamoja katika kuwaandalia mazingira mazuri zaidi ya kujiletea maendeleo na kuwarahisishia maisha yao, na hatimaye tuweze kuondoa vikwazo vya aina zote na tujenge jamii Jumuishi kwa Wote.
Kati ya mikakati yetu pia ni kuhakikisha Watu wote Wenye Ulemavu Zanzibar wanatambuliwa. Katika kuendeleza usajili wa Watu Wenye Ulemavu jumla ya Wilaya tisa zimefanyiwa usajili, zikiwemo tano Unguja na nne Pemba, kwa azma ya kuweza kupata takwimu sahihi na kurahisisha upangaji wa Sera na Mipango ya Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ofisi yangu kupitia Idara hii imeendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya jumuiya za watu wenye ulemavu, pamoja na kuandaa njia mbali mbali zitakazowezesha kupunguza changamoto zinazojitokeza. Kati ya juhudi hizo ni kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu, ambapo kila mwenye moyo wa kusaidia anaweza kutumia Mfuko huo kusaidia shughuli za kimaendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu wanapata fursa na haki zote kama ilivyo kwa wananchi wote. Aidha, Ofisi inatoa shukuruni nyingi na za dhati kabisa kwa wananchi wote waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kusaidia Watu Wenye Ulemavu kwa njia mbali mbali.
Njia hizo ni misaada ya kifedha, matibabu na visaidizi. Miongoni mwa watu waliotoa misaada hiyo ni pamoja na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, mtu mmoja mmoja ndani nchi, pamoja na jumuiya na taasisi mbali mbali.
Kwa ufupi kabisa hayo ndiyo mambo tunayoyatekeleza.
Ahsanteni.
KAMPUNI YA NDEGE YA HAINAN KUFANYA SAFARI ZA MOJA KWA MOJA HADI TANZANIA
 KAMPUNI ya Ndege ya  Hainan ya China imekubali kufanya safari za ndege za moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kukuza sekta ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.
 
Ahadi hiyo imetolewa leo mchana (Alhamisi, Oktoba 24, 2013) na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la Hainan (Hainan Airlines), Bw. Chen Feng baada ya kuombwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika mazungumzo yao alimwomba akubali ndege za shirika lake ziwe zinatua Tanzania. Ndege za shirika hilo zinafanya safari kati ya China na Angola kupitia anga la Tanzania.
 
Waziri Mkuu ambaye yuko ziara ya kikazi nchini hapa, moja ya eneo ambalo amekuwa anaziomba kampuni za ndege za China ni kufikiria kufanya safari ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara pamoja na utalii pamoja na kuja kuweza katika ujenzi wa hoteli za kitalii. Pia alisema kuna Watanzania wengi ambao wanakuja China kuchukua bidhaa hapa China lakini wanalazimika kuunganisha safari mara tatu hadi nne kabla hawajafika China jambo ambalo alisema linawaongezea gharama mno.
 
Akijibu maombi hayo ya Waziri Mkuu, Bw. Chen alisema kutokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili, maombi yake watayafanyia kazi na mojawapo ni hilo la kufungua safari za moja kwa moja za ndege kutoka China kwenda Tanzania.
 
Lakini alishauri kuwa ili njia hiyo iendelezwe ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuhakikisha njia hiyo inakuwa ya kudumu kwa kuwa na abiria wengi na ikiwezekana Tanzania kiwe kitovu cha usafiri wa anga kwa abiria wanaotoka nchi jirani wanaokwenda na kutoka China.
 
Alisema ili kuweza kuwa kitovu cha usafiri wa China, ni lazima abiria kutoka nchi jirani wapate usafiri  wa uhakika wa kuwafikisha katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ambako wataunganisha safari yao wakitokea katika nchi zao.
 
Alisema dawa pekee ya kufanikisha hilo ni kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la taifa ambalo litashirikiana na Hainan kuhakikisha safari hizo zinakuwa zenye tija na faida kwa kuwafikisha abiria hao kwenye kitovu cha usafiri wa kuunganisha kwenda China.
 
Pia alisema ili Dar es Salaam iwe kitovu cha usafiri wa anga ni lazima kuwe na uwanja wa ndege mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa wenye kukidhi mahitaji ya kimataifa (international standards). Alisema kampuni yake iko tayari kuja nchini kushiriki katika kupanua uwanja wa ndege utakaotumiwa na shirika hilo ili uwe wa kisasa.
 
 “Tuna wataaalam waliobobea katika eneo hilo, maana sisi wenyewe tu tunamiliki viwanja vya ndege vipatavyo 16, hivyo mkitushirikisha mtakuwa na uwanja ambao kila aina ya ndege inaweza kutua,” alisema mwenyekiti huyo wa Hainan Airlines.
 
Bw. Chen pia alisema suala la utalii ni la muhimu zaidi kwani anatambua kuwa Tanzania kuna vivutio vingi kama fukwe za bahari, mbuga za wanyama na vingine vingi na akaongeza kuwa shirika lake lina uzoefu wa biashara ya utalii kwani lina kampuni zinazofanya kazi ndani ya China na Hong Kong. “Tunaweza kusaidia kuwaleta Wachina waje kutalii Tanzania,” alisema Bw. Chen na kusisitiza kuwa wataangalia katika kuwekeza kwenye hoteli karibu na hifadhi za taifa.
 
Hainan ni moja ya mashirika makubwa ya ndege duniani. Ina ndege 470  na imeajiri wafanyakazi wapatao 1,000. Shirika hilo pia lina hoteli 500 za kitalii duniani na lina viwanja vya ndege vipatavyo 16 vikiwemo vitatu vya kimataifa.
 
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimweleza mwenyekiti huyo kuwa Tanzania inafanya juhudi za kujikomboa kiuchumi; lakini bado inahitaji msaada wa China hasa katika masuala ya usafiri wa anga ili iweze kupiga hatua kutoka hapo ilipo.
 
Alisema Tanzania kuna shirika la ndege lakini liko taabani licha ya kuwa lina njia nyingi na akatumia muda huo kumwomba mwenyekiti huyo wa Hainan kufikiria pia namna ya kuweza kufufua ATC ili iweze kufanya kazi pamoja na Hainan.
 
“Ndio maana tunawakaribisha nyinyi Hainan ni shirika kubwa ambalo naamini linaweza kuisaidia Tanzania katika eneo hilo la usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanya safari za moja kwa moja hadi Tanzania; lakini pia na kuangalia namna ya kulifufua shirika la ndege  la Tanzania (ATC),” alisema Waziri Mkuu.
 
Alimwomba Bw. Chen aangalie uwezekano kuja kujenga hoteli za kitalii karibu na viwanja vya ndege. “Iweje hoteli za utalii katika nchi yetu zijengwe na wafanyabiashara wa nchi za magharibi tu wakati na nyinyi mna uwezo wa kufanya vizuri zaidi hata kuliko wao? Alihoji.

RAIS KIKWETE ATEMBELEA NA KUKAGUA JENGO LA BUNGE MJINI DODOMA LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Oktoba 24, 2013 ametembelea na kukagua Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma kujionea maandalizi ya jinsi Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba watakavyokaa katika Ukumbi wa Bunge hilo. 

Bunge hilo Maalum la Katiba litakuwa na Wabunge 600 tofauti ya Bunge la sasa lenye Wabunge 354 ambao ni pamoja na Wabunge 239 wa kuchaguliwa kutoka majimboni, Wabunge Wanawake Viti Maalumu 102, Wabunge wa kuteuliwa toka Baraza la Wawakilishi Zanzibar 5, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wabunge 7 (kati ya 10) wa kuteuliwa na Rais.



Rais Kikwete akikaribishwa kutembelea Jengo la Bunge mjini Dodoma na Naibu Spika Mhe. Job Ndugai leo Oktoba 24, 2013.


Rais Kikwete akiangalia sehemu ya viti ndani ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013.


Rais Kikwete akitembelea Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013.


Rais Kikwete akisindikizwa na Naibu Spika Mhe Job Ndugai na Katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashilila baada ya kutembelea Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013.


Rais Kikwete akizungumza na Naibu Spika Mhe Job Ndugai na Katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashilila baada ya kutembeleaUkumbi wa Bunge mjini Dodoma leo Oktoba 24, 2013.

PICHA NA IKULU

Tuesday, 22 October 2013

Busara za JK zimefufua matumaini ya Wananchi


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Ireland nchini, Fionnula Gislen katika hoteli ya Serena Dar es Salaam (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Ireland nchini, Fionnula Gislen katika hoteli ya Serena Dar es Salaam (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema busara za Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete zimefufua matumaini ya wananchi wengi kuweza kupatikana Katiba mpya, baada ya kujitokeza changamoto ambazo ziliwafanya kuanza kuvunjika moyo.
Maalim Seif ameyasema hayo leo 22/10/2013 huko hoteli ya Serena Dar es Salaam alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Fionnuala Gilsenan yaliyohusu mambo mbali mbali, ikiwemo maendeleo ya mchakato wa kupatikana Katiba mpya Tanzania.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema baada ya kujitokeza malalamiko yaliyotokana na kuletwa mswada wa mabadiliko ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais Kikwete Oktoba 14 mwaka huu aliamua kukutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini.  
Amesema katika mazungumzo ya Rais na viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini, walikubaliana viongozi wa vyama hivyo wawasilishe mapendekezo yao yatakayosaidia kupatikana Katiba nzuri na kumaliza malalamiko na mivutano iliyojitokeza.


Maalim Seif alisema pande hizo zilikubaliana kwamba mazungumzo hayo yataendelea na yatakuwa chini ya Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), ambapo vyama vyote vya siasa vitakuwa na fursa ya kutoa na kuwasilisha yale wanayoona yanapaswa kuwemo au kutolewa ili baadaye yafikishwe bungeni kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
“Ni kwa uamuzi wa busara kama aliouonesha Rais Kikwete hali ya kukosekana mafahamiano itaweza kuepukwa na nchi yetu itaweza kupata Katiba itakayokidhi mahitaji ya wananchi” alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alieleza kuwa baada ya hatua hiyo ya Rais Kikwete kuweza kukaa pamoja na wadau muhimu katika zoezi la kutafuta Katiba Mpya, viongozi wa vyama wamefurahi na wako tayari kushiriki kikamilifu kufanikisha lengo lililokusudiwa.


Akizungumzia Muungano, Maalim Seif amesema wananchi walio wengi wanataka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uendelee kutokana na mahusiano na maingiliano ya miaka mingi, hata kabla ya nchi mbili hizo kupata uhuru, lakini pia alisema Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ya kujiamulia mambo yake, ndiyo itakayoweza kuufanya Muungano huo imara zaidi.

“Hata katika maoni ya wananchi hakuna Mzanzibari aliyetaka Muungano huu uvunjwe, lakini kwa upande wa Tanzania Bara walikuwepo asilimi nane, hali hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani Wazanzibari wanavyopenda Muungano uwepo”, amesema.
 
Aidha, Balozi huyo wa Ireland akizungumzia haja ya kudumishwa amani na utulivu, alikubaliana na ushauri wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, juu ya haja ya mataifa kushirikiana katika kupiga vita matukio ya uvunjifu wa amani pamoja na ugaidi.
 
Balozi Gislenan alisema vitendo vya ugaidi havina mipaka na nchi yoyote ile inaweza ikalengwa, kama ilivyojitokeza hivi karibuni nchini Kenya kwenye eingo la maduka la West Gate.
 
Amesema ni wajibu wa mataifa yote kushirikiana na kuwa na mikakati ya pamoja kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayatokei, pamoja na kuwasaka wale wote wanaojihusisha ili waweze kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

Sunday, 20 October 2013

CUF kuhakikisha kila Mzanzibari anapata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi


Na Khamis Haji,  OMKR
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama hicho kimedhamiria kuhakikisha kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 anapata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (ZANID) ifikapo mwezi Julai mwakani.
Maalim Seif amesema hayo alipokuwa akihutubia wanachama wa chama hicho katika matawi na Baraza mbali mbali zilizopo katika Wilaya ya Magharibi Unguja, alipokuwa katika ziara ya siku mbili kukagua uhai wa chama.
Hatua hiyo aliitangaza baada ya kujitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wanachama na wapenzi wa CUF kuwa wamekuwa wakinyimwa kwa makusudi vitambulishi hivyo kutokana na kile wanachoamini ni sababu za kisiasa.
Wanachama hao, katika majimbo ya Bububu, Mtoni, Mfenesini, na Dimani wamewatuhumu baadhi ya Masheha kushirikiana na watendaji wa Ofisi ya Vitambulisha vya Mzanzibari Mkaazi, kuwanyima haki hiyo, ikiwemo baadhi yao kuzunguushwa licha ya kuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Walisema uonevu huo unafanyika, licha ya kuwa vitambulisho hivyo vina matumizi mengi muhimu zaidi ya kutumika kwenye kupigia kura, ikiwemo kumuwezesha mwanchi kupata ajira, mikopo, hati ya kusafiria na hata huduma ya kuunga maji na umeme nyumbani.
“Hatukubali tena, lazima iwe mwisho, lakulifanya tutalijua sisi, wala hatutajali mtu ana itikadi gani, awe CCM, awe CUF au Chadema au hana chama, madhali ni Mzanzibari ana sifa tutahakikisha ifikapo Julai mwakani ana ZANID”, alisema Maalim Seif.  
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, wakati kuna Wazanzibari walio wengi wananyimwa vitambulisho hivyo, kuna baadhi ya watu wasiokuwa Wazanzibari mara wanapofika Zanzibar hutafutiwa ZANID na kupelekewa majumbani.
“Mnawanyima wananchi haki yao kwa mujibu wa sheria eti kwasababu tu mnaogopa kushindwa katika uchaguzi, hii ni dhulma … Chama cha Afro Shirazi nchi hii kilifanya Mapinduzi kupinga dhulma, na sisi basi tunasema hatuwezi tena kuvumilia dhulma hii”, alisema Katibu Mkuu wa CUF.
Alisema uvumilivu mara zote una mwisho na kuwaonya wote wanaohusika na utoaji wa vitambulishi hivyo waache tabia hiyo, ili kuiepusha nchi kuingia kwenye matatizo.
“Uvumilivu mara zote una mwisho, msitusukume hadi tukafika ukutani, athari zake zinaweza kuwa mbaya kabisa”, alionya Maalim Seif.  
Malalamiko hayo ya CUF yamekuja, licha ya kutolewa kauli kutoka kwa viongozin wa Serikali ya Zanzibar yenye muundo wa umoja wa Kitaifa, kuahidi kwamba wananchi wote wenye sifa watapatiwa vitambulisho vya ZANID.
Miongoni mwa waliowahi kutoa ahadi hizo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, ambapo pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alitoa kauli kama hizo na kuchukua juhudi kadhaa, ikiwemo kuwakutanisha wadau wa vitambulisho hivyo na viongozi wa CUF.
Hata hivyo, katika ziara hiyo ya Katibu Mkuu wa CUF, baadhi ya wanachama walieleza kuwa wameanza kupatwa na mashaka, huenda kauli hizo zikawa zinatolewa hadharani, lakini nyuma ya pazia kuna maagizo mengine ya kunyimwa vitambulisho hivyo.
Maalim Seif aliwaagiza watendaji wa chama hicho katika ngazi za matawi, majimbo na Wilaya kuorodhesha wanachama wote ambao wamenyimwa vitambulisho hivyo, ili chama kiweze kujua hali halisi ya tatizo hilo na kutafuta njia muafaka za kulitatua.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu wa CUF, pia alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama wa CUF kuzidi kukiimarisha chama chao kwa kuendeleza utaratibu wa vikao na kuepuka makundi, wakati huu ambapo uchaguzi ndani ya chama hicho unakaribia.
Aliwatahadharisha baadhi ya viongozi na wanachama wenye tabia ya kujenga mitandao na makundi ndani ya chama kwa dhamira ya kupitisha watu wao kuwa wagombea Ubunge au Uwakilishi kuacha tabia hiyo haraka, kwa kile alichoeleza kuwa sasa CUF hakitaivumilia.
“Kuna tabia ya kuanzisha mitandao kwa baadhi ya viongozi, kama njia ya kujipanga kupata Ubunge au Uwakilishi, chama kimeagiza kufuatiliwa wenye tabia hiyo, na atakayethibitika kapita kwa njia hizo tutafuta uteuzi wake”, alitahadharisha.
Aidha, alisema kuna tabia ya viongozi wengine kuchaguliwa majimboni, lakini baada ya kushinda hawaonekani tena, amewataka wanachama kuwa macho na kuhakikisha wanawachagua wanachama ambao wako tayari kuwatumikia wanachama na wenye uchungu na chama chao.
Akizungumza huko katika jimbo la Bububu, Mkurugenzi wa Uenezi, Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani alisema chama hicho kina laani kwa nguvu zote hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwavunjia nyumba wananchi wa Bububu Magengeni na Mwanyanya.
Alisema kwamba uvunjwaji wa nyumba hizo umefanywa bila ya kuzingatia taratibu na sheria na huenda umefanyika kutokana na msukumo wa kisiasa, baada ya kuonekana wakaazi wengi wa eneo hilo ni wafuasi wa chama cha CUF.
Alielza kuwa CUF kinataka uchunguzi wa kina ufanywe juu ya hatua ya kuvunjwa nyumba hizo zipatazo 300, kitendo ambacho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu, kwa vile wananchi wengi wamekosa mafali mwa kuishi na kupata hasara kubwa, bila ya kulipwa fidia.

Wednesday, 16 October 2013

Vyama vya Upinzani Tz na Serekali wakubaliana haya yafuatayo


Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UDP wamekubaliana mambo mawili makubwa baada ya kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa walipokutana jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliitishwa na Rais Kikwete ili kuondoa sintofahamu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa Septemba na Bunge lilipokutana mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana jioni ilisema katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya sheria hiyo.
Pia Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema. Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao waliambatana na wenyeviti wao ni Mohamed Mnyaa na Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na John Mnyika wa Chadema na Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Vicheko Ikulu
Vicheko na bashasha vyatawala Ikulu
Ilikuwa fursa kwa Rais Kikwete kukutana na viongozi hao baada ya kipindi cha miezi miwili cha kurushiana maneno baina ya viongozi wa Bunge, Serikali, CCM waliokuwa wakivutana na viongozi wa vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi.
Kama mtu yeyote angeulizwa kutabiri katika tukio lililotokea jana lingetokea basi angekuwa na wakati mgumu kutokana na ukali wa maneno na malumbano katika kipindi chote baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa Septemba.
Rais Kikwete alionekana mwenye furaha tele wakati alipokutana na viongozi wa vyama hivyo na kivutio zaidi ilikuwa pale alipokutana na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu.
Viongozi hao walisalimiana huku wote wakitabasamu na kuashiria kuwa waliamua kuweka tofauti zao pembeni na kuangalia masilahi ya nchi.
Kumbuka katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Septemba, Rais Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa yeye hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alikaririwa akisema kauli hiyo ya Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu, huku akisisitiza kuwa mbunge huyo alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alipinga tuhuma hizo na kusisitiza Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) bila ya ridhaa yao.
Chikawe, Wassira na Lukuvi ndani
Mawaziri watatu, ambao walitetea kwa nguvu kupitishwa kwa muswada ule ndani na nje ya Bunge walihudhuria mazungumzo hayo.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira walikuwemo kwenye mazungumzo ya jana.
Mawaziri hawa kwa nyakati tofauti walitetea kuwa mchakato wa muswada ule haukuwa na matatizo yeyote na kushikilia kuwa lazima Rais lazima asaini muswada kwani ulikuwa umepitishwa kihalali na Bunge.
Pia walikuwa wameshikilia kuwa safari hii kulikuwa hakuna mambo ya mazungumzo kati ya Rais na upinzani.
Chanzo cha sintofahamu
Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia mjadala wa muswada huo wakipinga matayarisho yake kutoshirikisha upande wa Zanzibar na pia walikuwa hawakubaliani na baadhi ya vipengele vya muswada huo.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka Ikulu zilisema kwamba Rais Kikwete alisaini muswada huo tangu Oktoba 10 mwaka huu siku ambayo wapinzani walipanga kufanya maandamano nchi nzima.
Katika mahojiano na Mwananchi jana jioni, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema muswada huo tayari ulikwishasainiwa na Rais na kama kuna marekebisho yatafanywa.
Mwananchi ilimtafuta Rweyemamu baada ya kusikia akithibitisha kusainiwa kwa muswada huo katika mahojiano na BBC Idhaa ya Kiswahili jana.
Akizungumza na Mwananchi Rweyemamu alisema, “Rais ameshasaini tangu Oktoba 10, unajua kulikuwa hakuna tatizo lolote kuhusu muswada huu kwa sababu ulifuata taratibu zote bungeni.”
Rweyemamu alisema kuwa awali Ikulu ilitoa taarifa kuwa Rais atakutana na wapinzani, pia atausaini muswada huo.
“Muswada umepitishwa bungeni na yeye amekamilisha kazi kwa kuusaini ili kuwa sheria. Alipokutana na wapinzani leo (jana) amewaeleza hilo na wameridhika” alisema Rweyemamu.
Chanzo : Mwananchi
JK ALIPOKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU MSTAKABALI WA KATIBA MPYA


Tuesday, 15 October 2013

Mahujaji milioni moja na nusu wamekusanyika kwenye mlima wa Arafat kutekeleza ibada ya Hijja huku idadi ikupungua kwa asilimia hamsini mwaka huu
Na Ali Bilali

Takriban mahujaji milioni moja na nusu kutoka katika pembe nne za dunia, wamekusanyika leo kwenye mlima wa Arafat, ikiwa ni wakati muhimu wa ibada ya Hijja ambayo hufanyika kila mwaka jijini Makka nchini Saudia Arabia. Ulinzi na Usalama vimeimarishwa kuhakikisha ibada hiyo inafanyika bila msuguano wowote.

Mahujaji waliokusanyika katika mlima arafat 

Kufuatia hali ya hewa ambapo jua kali, mahujaji wengi wameonekana wakijifunika kwa kutumia myamvuli huku wengine wakijikinga na jua chini ya miti kukiwa na joto kubwa lililofikia kwenye nyuzi 40. Ndege za Helikopta na wanajeshi wameonekana kila kona wakihakikisha usalama inaimarika vya kutosha.

Gavana wa mji wa Makka, mwanamfalme Khaled al-Fayçal, mabaye ni kiongozi wa kamati ya hijja, amefahamisha kuwa takriban mahujaji milioni moja na nusu wanashiriki ibada hiyo mwaka huu, huku mahujaji 117.000 wakiwa ni mahujaji wa ndani.

Hata hivyo amesema kiongozi huyo, idadi ya mahujaji imepungua kwa asilimia 50 ukilinganisha na mwaka uliopita ambapo idadi ya mahujaji ilifikia milioni 3.2.
Serikali ya Riyad ililazimisha asilimia 20 ya mahujaji kutoka katika mataifa mengine na asilimia 50 kutoka nchini Saudia Arabia wakihofia kulipuka kwa maradhi ya kuambukia, lakini pia kutokana na shughuli za ujenzi wa kulipanua eneo tofauti.

Katika msisitizo huo serikali hiyo iliwafukuza watu elfu sabini wa saudia na raia wa kigeni huku watu elfu 38 ambao walikuwa hawana kibali cha kuendesha ibada ya kijja walitiwa nguvuni pamoja pia na magari 138.000 yaliokiuka sheria na taratibu za Hijja.

Ibada hiyo ya Hijja inafanyika katika hali tulivu, hakuna taarifa yoyote ya kutokea kwa maradhi ya kuambukia ya homa ya ndege iliosababisha maafa ya watu elfu 60 kote duniani 51 wakiwa ni kutoka nchini Saudia.

Katika mlima wa Arafat, ikiwa ni kiashiria cha siku ya hukumu, mahujaji wanatumia fursa hiyo kwa kufanya ibada na kumuomba Mungu na kumtaka msamaha.

Baadae mchana mahujaii hao watashiriki ibada ya pamoja katika msikiti wa Namera, uliojengwa katika eneo hilo na ambao Mtume Muhamad alitowa hutuba yake ya mwisho Karne 14 zilizopita.

Baada ya kuzama kwa juwa, mahujaji watapiga kambi katika eneo la Mouzdalifa, kwenye umbali wa kilometa kdhaa na eneo hilo ambapo watalala katika eneo hilo.

Kulingana na mila, mahujaii hao watakusanya kokoto kwa ajili ya ibada ya kumlaani Shetani katika bonde la Mina, ikiwa ni siku ya kwanza ya Eid al-Adha, Sikukuu ya kujitolea ambayo itaadhimishwa siku ya Jumanne.

Ibada ya Hajj, ni moja miongoni mwa nguzo tano za kiilam na hufanyika kila mwaka na ambapo kila muumini mwenye uwezo anatakiwa kufanya angalau mara moja katika maisha yake.
Rais Dkt. Kikwete akutana na viongozi wa vyama vya Upinzani Ikulu

D92A8182
 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha ikulu kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Mh.Freeman Mbowe ikulu jijini Dar es Salaam leo.Nyuma kushoto ni Kiongozi wa NCCR Mageuzi James Mbatia na Professa Ibrahim Lipumba wa CUF.
 
D92A8214
 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya Pamoja na Viongozi wa Vyama vya upinzani muda mfupi kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu rasimu ya katiba ikulu jijini Dar es Salaam.Wengine katika picha kutoka kushoto Isaack Cheyo UDP, James Mbatia NCCR Mageuzi, Professa Ibrahim Lipumba CUF, Freeman Mbowe CHADEMA, Philip Mangula CCM, na Bibi Nancy Mrikaria aliyemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Mhe.Agustine LyatongaMrema .
 
D92A8241
 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyama vya upinzani na wasaidizi wao waandamizi muda mfupi kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu rasimu ya katika ikulu jijini Dar es Salaam leo.Kutoka kushoto mbele Isaack Cheyo UDP, James Mbatia NCCR Mageuzi, Professa Ibrahim Lipumba CUF, Freeman Mbowe CHADEMA, Philip Mangula CCM, na Bibi Nancy Mrikaria aliyemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Mhe.Agustine Lyatonga Mrema.Waliosimama Nyuma kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu CUF Bwana Julius Mtatiro,Mhe. Tundu Lissu CHADEMA, Bwana Martin Mng’ong’o NCCR Mageuzi ,Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu na Bunge William Lukuvi, Mhe.Habib Mnyaa CUF, Mbunge wa Ubungo Kwa tiketi ya CHADEMA Mhe.John Mnyika, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Mhe.Steven Wassira na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Mathias Chikawe.
 
D92A8156
 
Rais Dkt.Jakaya Kikwete akisalimiana na  Mhe.Tundu Lissu CHADEMA Nyuma ni Mhe.James Mbatia NCCR Mageuzi
 
D92A8158
 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Mhe. John Mnyika
 
D92A8179
 
 Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mzungumzo na Viongozi wa Vyama vya Siasa ikulu jijini Dar es Salaam leo