Thursday, 24 October 2013

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHESHIMIWA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI KUZUNGUMZIA MIAKA MITATU YA UTENDAJI WA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANAZIBAR AWAMU YA SABA HUKO KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HOTELI YA ZANZIBAR OCEAN VIEW – TAREHE 24 OKTOBA, 2013

                                                                                                                                                                                                       
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuweka katika hali ya uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia utendaji na majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika serikali yetu, hasa hii ya awamu ya saba ya uongozi ambayo imetimiza muda wa miaka mitatu sasa.
Mkutano huu ni mwendelezo wa uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya saba yenye mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, unaowataka viongozi wa juu na taasisi zote za serikali wawe wanajiwekea utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kila muda waliojipangia.
Pili natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari mliotenga muda wenu na kuja kuhudhuria kwa wingi na kuja kuitikia wito wetu wa kutusikiliza, ambapo baadaye mtapata fursa ya kuuliza, ili mpate ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii ya Wazanzibari kwa ujumla.
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Katika hotuba yangu nakusudia kugusia angalau kwa ufupi baadhi ya mambo muhimu yanayoendelea na kujitokeza katika nchi yetu hivi sasa, na katika siku za hivi karibuni. Kisha nitajikita zaidi kutoa maelezo kwa yale maeneo yaliyowekwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kama mjuavyo ofisi hii naiongoza mimi nikisaidiwa na Waziri wa Nchi makini, mchapakazi na muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji. Waziri wa Nchi ndiye msimamizi wa siku kwa siku wa shughuli zote za ofisi hii. Lakini pia nina Katibu Mkuu makini mjuzi na mzoefu wa taratibu za serikali, ambaye ndiye anayenishauri mimi na Waziri wa Nchi kuhusu masuala ya kitaalam, mbali kuwa Mtendaji Mkuu wa shughuli zote zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar Shajak akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii. Wote hao nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa, muda wote huu.
Waheshimiwa waandishi wa habari
Katika kipindi hiki cha muda wa miaka mitatu tunaendelea kushuhudia nchi yetu ya Zanzibar ikiendelea kuwa katika hali ya amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi wake. Hali hii imetuwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yetu Serikalini na kwa wananchi wote katika hali ya utulivu.
Kutokana na hali hiyo ndio maana hivi sasa ushiriki wa wananchi wote katika shughuli za kimaendeleo, kijamii na kisiasa umeendelea kuwa mkubwa, ambapo wamekuwa wakiiunga mkono Serikali yao katika mambo yote, ikiwemo yale mambo muhuimu ya Kitaifa tunayoendelea nayo hivi sasa. Kati ya mambo hayo ni Maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yanafikia kilele chake Januari 12 mwakani. Ni matumaini yangu kuwa wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, watashiriki kwa ukamilifu katika maadhimisho hayo.
Waheshimiwa Wana Habari
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya Saba yenye mfumo wa Kitaifa imeendelea kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika nyanja zote, zikiwemo za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Katika kipindi hichi cha miaka mitatu ya Serikali ya Mapinduzi yenye mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yapo mafanikio kadhaa yaliyopatikana. Kwanza ni kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa za kuimarisha uchumi wetu, lengo likiwa ni kuwaongezea kipato wananchi wetu.
Yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Saba. Miongoni mwa hatua hizo ni kupandisha bei ya karafuu. Wakulima wetu wamepata afueni kubwa ya bei, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma. Hali hiyo imewapa mwamko mkubwa wakulima wetu, lakini pia kuwa na mwamko wa kuziuza karafuu zao kunakohusika. Hadi jana jumla ya tani 1,540 tayari zimenunuliwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 21,560,805,000.
Kupandishwa bei ya karafuu kumewafanya wananchi wengi, hasa katika vijiji vya Pemba, kujenga nyumba bora zaidi na hivyo kuwafanya kuishi katika mazingira bora.
Halikadhalika, Serikali imechukua hatua za makusudi kabisa kumuendeleza mkulima, mfugaji na mvuvi. Katika hili Serikali imepunguza kwa kiwango kikubwa bei za pembejeo za kilimo, kama mbolea, dawa za kuulia magugu na wadudu, mbegu na kupunghuza gharama za kulimia kwa kutumia matrekta.
Serikali pia imechukua hatua za kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji, kwa nia ya kutumia njia za kisasa za ukulima na ufugaji. Jumla ya wavuvi wadogo 59 wamepelekwa China kujifunza njia za kisasa za ufugaji wa samaki. Pia Maafisa watatu wa Wizara ya Uvuvi na Ufugaji walipelekwa nchini Korea maalum kusomea ufugaji wa samaki.
Hatua hizi zote lengo lake ni kuwasaidia wananchi. Pia tumeona kwamba katika dhana hiyo hiyo ya kujaribu kuleta huduma kwa wananchi, serikali imekuwa ikijitahidi sana kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapata unafuu. Serikali pamoja na ufinyu wa bajeti yake inahakikisha kuwa zile dawa ambazo ni muhimu “essential drugs” zinapatikana katika hospitali zetu.
Kwa upande wa madaktari bado tuna upungufu, lakini juhudi za kuwasomesha watu wetu zinaendelea, vijana kadhaa wanapata mafunzo katika skuli ya udaktari ya Zanzibar yaani ‘Zanzibar Medical School’ na vijana hao watakapomaliza mwaka huu au mwakani, tutapata kwa mpigo mmoja madaktari 34. Hatua hiyo itaweza kupunguza sana pengo la upungufu wa madaktari katika nchi yetu.
Vile vile juhudi zinachukuliwa kuwataka wale madaktari ambao wanasoma nchi nyengine warudi, ili tumalize kabisa tatizo la uhaba wa wataalamu wa kada hii.
Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa vile vile imekuwa ikipambana na tatizo la upungufu wa maji kwa kushirikiana na wahisani na makampuni mengine ya nje. Tumekuwa na miradi mikubwa ya maji katika nchi na bado jitihada zinafanyika katika kupunguza tatizo hili.
Kwa mfano hivi sasa tumekubaliana na nchi ya Ras El Khaima kutusaidia katika suala la kuchimba visima kwa mintaaraf ya kupunguza tatizo la uhaba wa maji.
Tatizo la Umeme limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mradi wa MCC unaofadhiliwa na Marekani. Tunafahamu bado umeme unakatika katika kutokana na sababu tafauti. Lakini azma ya Serikali ni kulimaliza tatizo hili kabisa.
Ukiangalia sekta ya elimu, hivi sasa watoto karibu wote waliofikia umri wa kwenda skuli wanapatiwa fursa hiyo. Hivi sasa takriban kila Shehia ina angalau skuli moja, na zile Shehia chache ambazo bado hazijawa na skuli juhudi zinaendelea kufanywa, ili kuhakikisha kuwa kila Shehia inakuwa na skuli.
Serikali inaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuwekeza katika sekta mbali mbali, miradi ya kiuchumi imekuwa ikiongezeka. Kwa mfano mwaka jana pekee jumla ya miradi sita mipya na programu 18 mpya zilianzishwa. Ni azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushirikiana na sekta binafsi kuzidi mkuleta maendeleo.
Jengine ni kwamba tumeweza kuongeza maslahi ya wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika mwaka 2010/2011 mishahara ya wafanyakazi wa Serikali iliongezwa. Huko nyuma ilikuwa muda mrefu hawajapata nyongeza zao wala kupandishwa vyeo. Kwa kuwa katika mwaka 2011/2012 Serikali ilishughulikia suala la kupanga “Scheme of service”, kwa Wizara na Taasisi zote za Serikali ili kila mmoja ajijue yuko wapi. Lengo la Serikali ni kupandisha tena mishahara katika mwaka huu wa fedha 2013/2014.
Mengine ni Serikali hii kuona umuhimu wa sekta ya mifugo na uvuvi, Mhe. Rais ameunda Wizara Maalum inayoshughulikia Mifugo na Uvuvi. Kwa vile bado tuna changamoto, hatujaendeleza uvuvi katika bahari kuu na bado hatujawaendeleza ipasavyo wakulima wetu na hasa wafugaji, Wizara imepewa jukumu hilo kuona kuwa sekta ya uvuvi inakua sambamba na sekta ya ufugaji.
Pia tumefanya mabadiliko ya hapa na pale, sasa hivi sasa ipo Wizara maalum inayoshughulikia utalii, ambayo inaelekeza azma ya Serikali kuifanya sekta ya utalii kuwa sekta kiongozi katika uchumi wa Zanzibar. Chini ya Uongozi wa Rais Shein Serikali imebuni dhana ya utalii kwa wote, kwa min ajili ya kuwawezesha Wazanzibari wote washiriki katika kuundeleza utalii na kuweza kupata manufaa kutokan na utalii wenyewe.
Mafanikio haya pamoja na juhudi nyengine tunazoendelea kuzichukua, ikiwemo za kuliinua zao la Karafuu kwa kujali zaidi maslahi ya wakulima, yametuwezesha kukuza matumaini ya kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar ambao umeweza kukua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011hadi asilimia 7.0 mwaka jana.
Hayo ni kwa ufupi tu, lakini yapo mafanikio mengine makubwa ambayo yamepatikana katika kipindi hicho na hasa chini ya Serikali hii yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
Changamoto
Lazima tukiri kuwa pamoja na mafanikio hayo makubwa bado tunazo changamoto ambazo tunapaswa tusizifumbie macho.
Kwa mfano ni kweli tumeeneza skuli, lakini kwa sababu yale mahitaji ya elimu au mahitaji ya skuli ni makubwa, ukweli ni kwamba ule ubora wa elimu bado haujafikiwa kwa kiwango cha kuridhisha. Zamani darasa lilikuwa na wanafunzi kati ya 24 na 30, lakini sasa hivi si ajabu kukuta darasa lina wanafunzi 80 hadi 100. Sasa katika hali kama hiyo, ukweli mwalimu anakuwa na kazi pevu. Pia kuna upungufu wa walimu wa Hesabu, Sayansi, Kingereza na Jographia. Halikadhalika tuna upungufu wa zana za kufundishia, hasa kwa masomo ya Sayansi.
Vile vile kwa sababu ya kupanuka kwa huduma, uwezo wetu wa kiuchumi bado ni mdogo, hata huduma za afya hazijawa za kutosheleza. Wakati mwengine tunakabiliwa na upungufu wa dawa hasa dawa ambazo ni muhimu zaidi, upungufu wa wafanyakazi hasa madaktari na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya, kuna upungufu wa zana au vitendea kazi vya kutibia, Hizi ni baadhi ya changamoto ambazo tunapambana nazo.
Serikali katika awamu zote imekuwa zikichukua hatua mbali mbali katika kupunguza matatizo hayo ambayo yanatukabili.
Changamoto nyengine ambayo imejitokeza katika siku za hivi karibuni katika nchi yetu ni hili suala la vitendo vya hujuma, ikiwemo watu kumwagiwa tindikali na hujuma za aina nyengine.
Napenda kusema kuwa haya ni mambo ya kusikitisha kabisa, kwa sababu sisi Wazanzibari tumezoweya kuwa nchi yetu ni nchi ya amani.
Haya mambo ya raia kutumia risasi au mashambulizi kwa kutumia tindikali kwa Zanzibar ni mageni. Sisi ustaarabu wetu Wazanzibari, Utamaduni wetu na dini zetu, masuala haya ya ukatili na hujuma sio mambo yetu kabisa.
Mambo haya yananisononesha na kunisikitisha sana, hasa kipindi hiki ambacho tuna maridhiano katika nchi. Kama mambo haya yangetokea wakati ule wa tofauti za kisiasa, tungesema ni hujuma za kisiasa, lakini leo tunayo serikali ya pamoja. Kila chama ambacho kina viti katika Baraza la Wawakilishi kinashirikishwa katika serikali hii ya Umoja wa Kitaifa. Suala la kujiuliza kwanini jambo hili lizuke sasa? Ukweli ni mtihani mkubwa kwetu.
Sisi Wazanzibari tumekuwa ni watu wa dini mbali mbali kwa muda mrefu. Tokea enzi na enzi kiwango cha uvumilivu wa kidini ni kikubwa Zanzibar, mimi nadhani hakuna duniani kuliko Zanzibar. Hapa inajulikana kabisa kwamba asilimia 98 ni Waislamu. Lakini lazima wananchi wajue kwamba Ukristo katika Afrika Mashariki na Kati, mlango wake uliopitia kwenda huko ni Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Jambo jengine zito linalotukabili katika kipindi hichi cha Serikali ya Awamu ya Saba ni mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchakato huo unatokana na dhana na fikra za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Yeye kwa busara zake ameona kwamba sasa hivi miaka 50 imepita tangu Uhuru wa Tanganyika. Hivyo tunahitaji kuandika Katiba Mpya ambayo itawashirikisha wananchi wenyewe.
Kwa hivyo mimi nimpongeze kwa dhati Rais Jakaya Kikwete kuona umuhimu huu wa kuwashirikisha Watanzania wenyewe kuandika Katiba mpya. Yeye alisema wazi kwamba baada ya miaka 50 lazima tuwe na katiba ambayo inakidhi mahitaji ya wakati huu. Katiba ambayo angalau itatuchukua miaka 50 mingine. La msingi zaidi ni kuwa wananchi washirikishwe kikamilifu.
Ni uamuzi mzuri aliochukua Rais ingawa kuna changamoto zake. Hivi sasa tumemaliza hatua ya Tume kukusanya maoni ya wananchi, pamoja na ili hatua ya Mabaraza ya Katiba kuchambua Rasimu ya Kwanza ya Katiba hiyo. Hatua inayoendelea hivi sasa ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuendelea kuchambua maoni ya Mabaraza hayo, na hatimaye iweze kupatikana rasimu ya Pili ambayo ndiyo itapelekwa kwa Rais na yeye Rais kuiwasilisha kwenye Bunge la Katiba.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Hata hivyo, pamoja na azma njema ya kuifanya nchi yetu iwe na Katiba mpya ifikapo mwakani, lazima tukiri kwamba changamoto nyingi zinaendelea kujitokeza katika suala hili.
Waandishi wa habari mnakumbuka mfululizo wa matukio yaliyojiri, hasa baada ya Serikali kuamua kuwasilisha Bungeni mswada wa kurekebisha sheria ya Mabadiliko ya Katiba, pamoja na kadhia nzima ya vurugu zilizojitokeza Bungeni hivi karibuni na kusababisha baadhi ya Wabunge wa Upinzani, wakiwemo viongozi wa Kambi hiyo, kulalamika kutotendewa haki na kuamua kutoka nje.
Baada ya yote yaliyotokea, Rais wa Jamhuri ya Muungano ameona busara ya kukaa meza moja na viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyo sajiliwa, ili kuyajadili kwa upeo wake mambo yanayo lalamikiwa. Kati ya mdai ya msingi ni madai kwamba upande wa Zanzibar haujashirikishwa katika mabadiliko ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mambo mengine mengi, ikiwemo muundo na upatikanaji wa Wabunge wa Bunge Maalum, wasiokuwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Matarajio yangu ni kwamba vikao vilivyofanyika na maazimio ya vikao hivyo, kati ya Rais na Viongozi wa vyama vya siasa yataweza kuzaa maafikiano mema, ili hatua zinazofuata katika suala zima la kuandika Katiba mpya ziweze kuendelea kwa amani na utulkivu na matarajio ya wananchi walio wengi yaweze kufikiwa.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Baada ya kueleza kwa kifupi baadhi ya masuala mabli mbali yanayogusa nchi yetu kwa jumla, sasa naomba niruhusuni kuingia moja kwa moja katika utendaji wa majukumu ya Idara na Tume zilizopo katika Ofisi yangu. Hizo ni Tume ya Ukimwi Zanzibar, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Idara ya Mazingira na Idara ya Watu Wenye Ulemavu.
Tume ya Ukimwi
Tume hii ina umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa ustawi na afya za wananchi wa Zanzibar. Ndiyo maana ikapewa majukumu makuu ya kuhakikisha kwamba Sera na Mikakati ya Taifa ya kupiga vita ukimwi zinaandaliwa na kutekelezwa ipasavyo, nia ikiwa ni wananchi wetu wabaki salama na wasiambukizwe Virusi vya Ukimwi.
Mambo mengine yanayotekelezwa kupitia Tume hii ni kutafuta rasilimali zitakazo tumika katika kutekeleza Muitikio wa Kitaifa wa kupambana na Ukimwi, kuimarisha uwezo wa wadau katika kufanyia kazi program za ukimwi pamoja na kuratibu shughuli zao. Aidha majukumu mengine ya Tume ni kushajiisha utoaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu walioathirika na kuathiriwa, kufuatilia na kutathmini ufanisi wa mapambano dhidi ya ukimwi, pamoja na kutoa taarifa zote zinazohusiana na Ukimwi.
Mafanikio makubwa yameweza kupatikana chini ya utendaji wa Tume hii.
Kwa mfano mwaka jana Tume hii iliweza kusaidia Shehia 22 kuibua Mipango Mkakati ya kukabiliana na Ukimwi. Aidha, katika juhudi za kuongeza uwezo wa program za habari na kuchochea mabadiliko ya tabia katika masuala ya Ukimwi nyumba kadhaa za makaazi ya vijana walioacha dawa za kulevya ‘Sober Houses’ zimesaidiwa kwa kununuliwa televisheni na radio. Dada poa wapatao 307 na kaka poa 38 na vijana 271 wanaojidunga sindano waliweza kufikiwa kupatiwa taaluma kupitia waelimishaji rika.
Pia taasisi za Kidini zinaendelea kuhamasisha waumini wao kupitia katika mikusanyiko ya kidini juu ya mbinu muafaka za kuzuia maambukizi ya ukimwi, kusaidia upatikanaji wa taarifa za afya ya uzazi na usawa wa kijinsia.
Tukiwa tumo katika utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kupambana na Ukimwi, Mapitio ya Sheria ya Tume ya Ukimwi Nam.3 ya mwaka 2002 yamefanyika na rasimu ya mswada wa marekebisho yake yanatarajiwa kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi karibuni.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio katika juhudi hizo, bado changamoto kubwa inatukabili, changamoto hiyo imejitokeza wazi baada ya Utafiti wa mwisho uliofanywa juu ya Virusi vya Ukimwi na Malaria kuonesha kwamba kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Tanzania kwa mwaka 2011/2012, kwa upande wa Zanzibar kimepanda kutoka asilimia 0.6 hadi asilimia 1. Taarifa hizi sio nzuri kwetu na nguvu ya pamoja inahitajika kuhakikisha kwamba maambukizi zaidi yana zibitiwa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya
Kama mnavyoelewa, Zanzibar kama ilivyo kwa nchi nyengine Duniani, miongoni mwa changamoto kubwa zinazojitokeza ni kuwalinda vijana wake wasiathiriwe kwa matumizi ya dawa za kulevya, lakini pia kukomesha uingizwaji na biashara ya dawa hizo kwa jumla.
Suala hili ni changamoto kubwa kwetu. Juhudi kubwa tunazichukua ikiwemo, kuhakikisha Sheria ya Dawa za Kulevya inatekelezeka, mpango wa utekelezaji wa sheria hiyo ‘Road Map’ tayari imeandaliwa. Katika mwaka uliopita jumla ya watu 22 wamekamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya, kati yao wanaume ni 21 na mwanamke mmoja, ambapo jumla ya kesi 22 zipo mahakamani. Wizara yangu tayari imeandaa rasimu ya kanuni ya Sheria ya Dawa za Kelevya, ili kuona sheria hiyo inatekelezwa ipasavyo.
Aidha, vipindi vya redio na televisheni vilivyolenga kuinua mwamko wa jamii juu ya athari za dawa za kulevya vimerushwa hewani kupitia vyombo mbali mbali vya habari. Vile vile kampeni kubwa inafanyika maskulini, ambapo kwa mwaka jana wanafunzi wapatao 6,270 Unguja na Pemba walipatiwa elimu juu ya athari za dawa za kulevya.
Vile vile kwa kutambua mchango wa taasisi zisizokuwa za kiserikali, katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Tume imezipatia ruzuku nyumba tisa za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober Houses), kwa ajili ya kusaidia mahitaji yao mbali mbali.
Jambo muhimu la kuzingatiwa katika kupiga vita dawa za kulevya Zanzibar na kwengineko, ni kuendelea kutoa elimu, ili watu wote wakatae kutumia dawa za kulevya. Kwani itakapofika pahala ambapo hakuna mtu anayetaka kutumia, ni wazi kwamba hata yule muingizaji naye atakuwa haingizi tena kwa sababu hakuna soko.
Waheshimiwa Wana Habari
Idara ya Mazingira
Hii nayo ni Idara muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa wananchi na uendelevu wa nchi yao katika suala zima la kuhakikisha mazingira hayaharibiwi.
Kati ya majukumu makubwa yanayotekelezwa na Ofisi yangu, kupitia Idara hii ni kukusanya na kuhifadhi taarifa za kimazingira, kwa azma ya kusaidia utayarishaji na utekelezaji wa mipango na miradi ya kimazingira. Vile vile kuhamasisha wananchi na wadau wote kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa jamii yetu.
Mbali na hayo majukumu mengine makubwa yanayosimamiwa chini ya Idara hii ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kimaendeleo haziwi chanzo cha uharibifu wa mazingira. Mwaka jana tuliweza kukagua jumla ya miradi 65 ya mahoteli, miradi 15 ya uwekezaji imefanyiwa tathmini ya Athari za Kimazingira. Aidha, kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi Pemba kimefanyiwa ukaguzi wa kimazingira na ripoti yake imekabidhiwa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, ikiwemo mapendekezo yaliyotolewa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya tabia nchi ni eneo jengine ambalo nchi yetu inalipa umuhimu wa kipekee, hasa kwa maumbile ya nchi yetu ikiwa ni ya visiwa vidogo. Kwa kawaida nchi kama hizi huathiriwa sana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Zanzibar imeendelea kuwa mshirika muhimu katika umoja wa nchi za visiwa katika Bahari ya Hindi (ISLANDS), na imekuwa ikinufaika kwa njia mbali mbali na ushiriki huo katika kuandaa na kutekeleza mikakati na program tafauti za kukabiliana na athari hizo na kuhifadhi mazingira kwa jumla, pamoja na kwamba hadi sasa sio mwanachama kamili wa jumuiya hiyo.
Miongoni mwa mikakati yetu Zanzibar katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ni suala hilo kulihusisha moja kwa moja katika ngazi za Shehia, ili wananchi wenyewe wahusike kikamilifu. Kamati 10 za majaribio za usimamizi wa ukanda wa pwani tumezisaidia kuandaa mipango ya utekelezaji ya usimamizi wa mazingira katika maeneo yao. Miongoni ya Shehia hizo ni Nungwi, Chwaka, Nyamanzi na Mtende.
Kazi ya kuyatambua maeneo yaliyoingiliwa na maji ya chumvi na hivyo kuathiri shughuli za kimaendeleo, kijamii na kiuchumi, ikiwemo kilimo kote Zanzibar inaendelea. Hatua hii itatuwezesha kujua ukubwa wa tatizo na hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.
Ofisi yangu imejikita zaidi kuhakikisha kwamba, Sera, Sheria na Kanuni za Mazingira zinatekelezwa. Kwa mfano kwa mwaka jana jumla ya operesheni 117 zimefanyika Unguja na Pemba na watu 33 walikamatwa na kuhukumiwa kwa faini ya TZS 3,280,000 kwa jumla. Operesheni za kudhibiti mifuko ya plastiki zinaendelea. Mwaka jana kilo 670 za mifuko ya plastiki ziliteketezwa katika eneo la Maruhubi.
Matarajio yetu ni kupata mafanikio makubwa zaidi katika utekelezaji wa majukumu yetu, hasa baada ya Serikali kuidhinisha Sera mpya ya Mazingira na Mpango wa Utekelezaji wa Usimamizi wa Mazingira kuandaliwa kwa mujibu wa Sera hiyo Mpya ya Mazingira.
Waheshimiwa Wana Habari
Idara ya Watu Wenye Ulemavu
Idara hii yenye majukumu ya kuratibu masuala mbali mbali ya watu wenye ulemavu Zanzibar, pia ina umuhimu mkubwa na wa kipekee katika kuhakikisha haki sawa inapatikana miongoni mwa wananchi wote wa Zanzibar bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote ile.
Katika kuhakikisha tunafanikisha hilo la kuleta usawa na kuona watu wenye ulemavu wanapata fursa zote, ikiwemo za kielimu, kiuchumi na kushirikishwa kikamilifu katika mambo yote yanayohusu nchi na jamii, mkazo mkubwa tumeuweka katika kufanya kazi kwa pamoja na jumuiya zote zilizopo za Watu Wenye Ulemavu.
Miongoni mwa Jumuiya hizo ni Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), Chama cha Viziwi (CHAVIZA), Umoja wa Watu Wenye Ulemavu (UWZ), Jumuiya ya Maalbino Zanzibar (JMZ), Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu (JUWAUZA), Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (ZADA), Chama Maalum cha Olympic kwa Watu Wenye Ulemavu (SOZ) na jumuiya nyenginezo.
Hata hivyo lazima tukiri kwamba tuna changamoto kubwa ya uhaba wa fedha, visaidizi na nyenzo nyengine kwa ajili ya kuweza kutosheleza mahitaji yote kwa wenzetu Wenye Ulemavu.
Kutokana na hali hiyo, Serikali, taasisi zisizokuwa za kiserikali na jamii kwa jumla, hatuna budi tushirikiane kwa pamoja katika kuwaandalia mazingira mazuri zaidi ya kujiletea maendeleo na kuwarahisishia maisha yao, na hatimaye tuweze kuondoa vikwazo vya aina zote na tujenge jamii Jumuishi kwa Wote.
Kati ya mikakati yetu pia ni kuhakikisha Watu wote Wenye Ulemavu Zanzibar wanatambuliwa. Katika kuendeleza usajili wa Watu Wenye Ulemavu jumla ya Wilaya tisa zimefanyiwa usajili, zikiwemo tano Unguja na nne Pemba, kwa azma ya kuweza kupata takwimu sahihi na kurahisisha upangaji wa Sera na Mipango ya Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ofisi yangu kupitia Idara hii imeendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya jumuiya za watu wenye ulemavu, pamoja na kuandaa njia mbali mbali zitakazowezesha kupunguza changamoto zinazojitokeza. Kati ya juhudi hizo ni kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu, ambapo kila mwenye moyo wa kusaidia anaweza kutumia Mfuko huo kusaidia shughuli za kimaendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu wanapata fursa na haki zote kama ilivyo kwa wananchi wote. Aidha, Ofisi inatoa shukuruni nyingi na za dhati kabisa kwa wananchi wote waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kusaidia Watu Wenye Ulemavu kwa njia mbali mbali.
Njia hizo ni misaada ya kifedha, matibabu na visaidizi. Miongoni mwa watu waliotoa misaada hiyo ni pamoja na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, mtu mmoja mmoja ndani nchi, pamoja na jumuiya na taasisi mbali mbali.
Kwa ufupi kabisa hayo ndiyo mambo tunayoyatekeleza.
Ahsanteni.

No comments:

Post a Comment