Friday, 25 October 2013

Mageuzi tena Katiba Mpya


Mwandishi Wetu
23 Oct 2013
RASIMU ya awali ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imekwishajadiliwa katika Mabaraza ya Katiba na sasa inafanyiwa uchambuzi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inafanyiwa mabadiliko kadhaa ya msingi huku mfumo wa Serikali Tatu ukiendelea kubaki kama ilivyopendekezwa, Raia Mwema limeelezwa.
Kati ya mambo ya msingi ambayo yataingizwa katika awamu ya pili ya rasimu ya Katiba Mpya ikakayowasilishwa kwa Rais na kisha katika Bunge la Katiba mara baada ya kukamilika ni pamoja na mipaka kati ya Tanganyika na Zanzibar, kuongozwa kwa mambo ya Muungano kutoka saba yaliyopendekezwa awali hadi 10, kinga dhidi ya mashitaka ya Rais, majimbo ya ubunge kwa Bunge la Muungano, ulinzi na usalama pamoja na vyama vya siasa kuweza kufukuza wabunge walioshinda kwa ridhaa ya vyama hivyo.
Mipaka ya Tanganyika na Zanzibar
Mipaka ya Tanganyika na Zanzibar ni lazima iwekwe ndani ya Katiba ili kila mamlaka ya nchi washirika iendeshe shughuli zake bila kuingiliana. Uchimbaji wa mafuta au uvuvi wa samaki, Tanganyika ijue iishie wapi na Zanzibar iishie wapi.
Kwa sasa katika rasimu ya Katiba Mpya, sura ya kwanza inayozungumzia mipaka, alama, lugha, utamaduni na tunu za taifa, ibara yake ya pili inaeleza kuhusu eneo la Jamhuri ya Muungano kuwa ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari.
Mambo ya Muungano kutoka saba hadi 10
Kwa sasa, katika rasimu ya kwanza ya Katiba mpya, mambo ya Muungano yanatajwa kuwa saba ambayo ni mosi, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pili, ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; tatu, uraia na uhamiaji; nne, sarafu na benki kuu; tano, mambo ya nje; sita, usajili wa vyama vya siasa na saba; ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Katika mambo hayo saba, yatanatarajiwa kuongezwa matatu kwa mujibu wa maoni yaliyotolewa wakati wa Mabaraza ya Katiba. Yanayoweza kuongezwa ni Haki za Binadamu, Tume Huru ya Uchaguzi, Maadili na Miiko ya Uongozi.
Kinga dhidi ya mashitaka ya Rais
Rasimu ya kwanza ya Katiba mpya iliyojadiliwa katika Mabaraza ya Katiba ilipendekeza katika Ibara ya 83(1) na (2) kuhusu kinga dhidi ya mashitaka ya Rais. Katika ibara hiyo ya 83 (1) inaeleza; Wakati Rais akiwa madarakani, hatashitakiwa wala mtu yeyote hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai.
Ibara ya 83(2) inaeleza; wakati Rais ameshika madaraka kwa mujibu wa Katiba hii, haitaruhusiwa kufungua mahakamani shauri la madai kuhusu jambo lolote alilolitenda au alilokosa kulitenda yeye binafsi kama raia ama kabla au baada ya kushika madaraka ya Rais, ila tu kama angalau siku thelathini kabla ya shauri kufunguliwa mahakamani, Rais atapewa au ametumiwa taarifa ya madai kwa maandishi kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na taarifa hiyo ikiwa inatoa maelekezo kuhusu chanzo cha shauri hilo, kiini cha madai yenyewe, jina lake na anwani ya mahali anapoishi huyo mdai na jambo hasa analodai.
83 (3) inaeleza; isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na kura ya kutokuwa na imani na Rais, haitakuwa halali kwa mtu kumshitaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo alilofanya wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais.
Katika eneo hili kuhusu kinga dhidi ya mashitaka ya Rais, maoni mengi ambayo yanapewa nafasi kubwa kuwekwa katika rasimu ijayo ya Katiba mpya itakayowasilishwa katika Bunge la Katiba ni kutaka kuwapo na mwanya wa kumshitaki Rais baada ya kuondoka madarakani, hasa kwa makosa ambayo atakuwa amefanya yasiyohusiana na madaraka yake ya urais.
“Huwezi kuwa na kinga ya jumla katika kumshitaki Rais ambaye amekwishaondoka madarakani, tunaweza kuwa na kinga ya kutomshitaki kwa mambo ambayo ameyafanya kama Rais na lakini lazima kuwe na nafasi ya kumshitaki kwa mambo ambayo ameyafanya akiwa madarakani ambayo si sehemu ya majukumu ya Rais. Kwa mfano, ikitokea Rais amehusishwa na matukio ya hovyo kama ubakaji. Jiulize, ubakaji ni kazi za Rais…kama siyo kwa nini asishtakiwe baada ya kuondoka madarakani?” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Majimbo ya Bunge la Muungano utata
Kwa kuzingatia maoni ya wadau wengi wa Mabaraza ya Katiba, kumekuwa na hali ya kupaki njia panda katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo katika rasimu yake ya awali ilipendekeza katika Ibara ya 105 (2) kuhusu aina za wabunge ambao ni (a) waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi (b) wabunge watano watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuchaguliwa kuwa waunge kuwakilisha watu wenye ulemavu kwa kuzingatia uwiano wa Washirika wa Muungano.
Lakini sehemu inayoiweka njia panda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sasa, hasa baada ya kukusanywa kwa maoni ya Mabaraza ya Katiba ni kuhusu muundo wa majimbo ya ubunge, kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika rasimu ya awali, ilipendekezwa katika Ibara ya 105 (3) kwamba;…kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa jimbo la uchaguzi.
Hoja inayoibua utata hapo ni kwamba, kwa sababu, kwa mfano, Rais wa Tanganyika (Tanzania Bara) anaweza kugeuza wilaya kuwa mkoa na kwa hiyo akaweza kuongeza idadi ya majimbo ya ubunge na kwa sababu, Rais wa Zanzibar anaweza kubadilisha shehia kuwa wilaya ili kuwa na idadi kubwa ya majimbo na hatimaye idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Muungano, kwa sababu zozote zile ikiwamo kuwa na idadi kubwa ya wabunge kwa ajili ya kulinda maslahi ya upande anaoongoza, kigezo cha mkoa au wilaya kuwa jimbo la uchaguzi kinapoteza mantiki.
Sasa inaweza kupendekezwa, kuwapo kwa idadi mahsusi ya majimbo ya uchaguzi na hasa kwa kigezo cha idadi ya usawa kati ya Bara na Zanzibar, yaani asilimia 50 ya wabunge wa Bunge la Jamhuri watoke Bara na wengine asilimia 50 ya idadi ya wabunge wa Bunge hilo watoke Zanzibar, bila kujali ukubwa wa nchi hizo Washirika.
Ulinzi na Usalama
Katika rasimu ya sasa, kwa mfano Ibara ya 224, inaeleza; kutakuwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ambaye atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama wa Taifa. Baraza hilo la Ulinzi na Usalama wa Taifa linatajwa katika 221(1) kuundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano; Makamu wa Rais; Rais wa Tanzania Bara; Rais wa Zanzibar; Waziri mwenye dhamana na ulinzi; Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi, Waziri mwenye dhamana na mambo ya nje; Waziri mwenye dhamana na usalama wa taifa; waziri mwenye dhamana ya fedha; Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania; Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na mapendekezo ya Mabaraza ya Katiba, eneo hili linaweza kufanyiwa mabadiliko ili wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini wateuliwe na Rais lakini wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfano unaopendekezwa hapa ni kama wa sasa wa namna Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyopatikana, ambaye jina huteuliwa na Rais, kisha jina lake kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa au hata kukataliwa.
Chama kuweza kufukuza mbunge
Kwenye rasimu ya awali, kuhusu uwajibikaji wa wabunge katika Ibara ya 123(2) na (3) zinagongana kimantiki. Wakati ibara ya 123(2) ikieleza; Mbunge aliyependekezwa na chama cha siasa, hatapoteza ubunge wake ikiwa mbunge huyo atafukuzwa au kuvuliwa uanachama wa chama chake na Ibara ya 123(3) inaeleza; endapo mbunge, kwa ridhaa yake atajiondoa au kujivua uanachama kutoka chama chake cha siasa, mbunge huyo atapoteza sifa za kuwa mbunge na atasita kuwa mbunge.
Kutokana na mgongano huo wa kimantiki, mabadiliko yanatajwa kuweza kufanyika kwamba chama kinapomvua uanachama mbunge husika basi na ubunge wake ukomee hapo. Katika hili, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, inaelezwa vyama vyote vikubwa vya siasa nchini vimekubaliana na kuna nafasi kubwa ya kupitishwa.
Eneo jingine ambalo litafanyiwa marekebisho kwa mujibu wa vyanzo vyetu hivyo vya habari ni namna ya kumwondoa mbunge asiyejali maslahi ya wananchi wake kabla ya muda wake wa muhula kuhitimishwa.
Katika rasimu ya awali, ibara ya 124 (1) inaeleza, bila kuathiri masharti ya Ibara ya 123 ya Katiba hii, wananchi watakuwa na haki ya kumwondoa mbunge wao madarakani, endapo mbunge atafanya mojawapo ya yafuatayo; (a) kuunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume cha maslahi ya wapiga kura au kinyume cha maslahi ya taifa.
Katika kipengele hiki, uzoefu wa ushindani wa uvunaji, usafirishaji na matumizi ya gesi ya Mtwara unatumika kujenga hoja ya kuondoa kipengele hiki. Chanzo chetu cha habari kinaeleza; “Kwa mfano, Mtwara maslahi ya taifa yanaonyesha gesi hiyo isafirishwe na kuhudumia taifa zima lakini wananchi wa jimbo mojawapo kwa mfano walikuwa wanasema gesi hiyo isisafirishwe, kama mbunge wa jimbo husika atasema isafirishwe maana yake hazingatii maslahi ya wananchi wake kwa hiyo afukuzwe….hii haijakaa sawa.
“Kwa hiyo, kipengele hiki kinaweza kufanyiwa marekebisho bila kupora haki ya wananchi kumwondoa mbunge wao. Kwa mfano, inaweza kuelezwa katika Katiba wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kwa mujibu wa sheria itakayotungwa na Mbunge,” anaeleza mtoa habari wetu kutoka serikalini.
Mchakato unaendelea
Kwa sasa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ipo katika hatua ya uchambuzi wa maoni yaliyotokana na mikutano ya Mabaraza ya Katiba na baada ya hapo, itaandika rasimu ya Katiba Mpya awamu ya pili ambayo itakabidhiwa kwa Rais ambaye ataitisha Bunge la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na baada ya hapo, rasimu hiyo itawasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Bunge la Katiba linaweza kurekebisha au kuongeza masuala mbalimbali katika rasimu hiyo y awamu ya pili itakayowasilishwa kwao na baada ya kuridhika, na rasimu hiyo kuwasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa hizo kura za maoni, wananchi watapiga kura ya maoni kwa njia ya kujibu swali la ndiyo kama wanaikubali au hapana kama hawaitaki rasimu hiyo.
Mchakato wa upigaji na usimamizi wa kura ya maoni utaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo kwa sasa inaongozwa na Jaji Damian Lubuva.
..- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/mageuzi-tena-katiba-mpya#sthash.kX75XLfW.dpuf

No comments:

Post a Comment