Saturday, 26 October 2013

Serikali ya China yatoa msaada wa fedha kwa SMZ 


Waziri wa Fedha  Omar Yussuf Mzee
Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana Saini mkataba wa makubaliano na Serikali ya China  ambapo nchi hiyo itaipatia Zanzibar msaada wa zaidi ya  Dola milioni sita za Marekani ikiwa ni uendelezaji wa misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa Zanzibar katika nyanja mbali mbali za Uchumi.
Sherehe za utiaji saini makubaliano hayo  zilifanyika leo  katika Wizara ya Fedha, Vuga  ambapo Waziri wa Wizara hiyo  Omar Yussuf Mzee aliiwakilisha Zanzibar na Balozi mdogo wa China hapa Zanzibar Xie Yunliang aliiwakilisha nchi yake.
Akizungumza baada ya utiaji saini, Waziri wa Fedha alisema kua msaada huo utalenga katika nyanja mbali mbali ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, Uchimbaji wa visima vya maji safi na salama na kupambana na mbu wa malaria  katika maeneo ambayo maradhi hayo bado yapo.
Alisema kazi iliobakia hivi sasa ni kwa Idara ya  Hazina kuwasiliana na wahusika  ili utekelezaji wa makusudio hayo yaweze kufikiwa kwa haraka.
Nae Balozi Xie Yunliang alisema kuwa  Zanzibar na China ni nchi mbili zenye uhusiano mzuri  wa muda mrefu hali ambayo imeifanya kua ni rafiki wa karibu.
Alisema  makubaliano hayo ni muendelezo wa misaada wanayoitowa ili kuona Zanzibar inapiga hatua katika juhudi zake za kukuza Uchumi na Maendeleo ya wananchi.
Utiaji saini makubaliano hayo ulikwenda  sambamba na  kukabidhiwa hati za Taa za Barabarani zinazo tumia nishati ya jua katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar ambapo mradi huo ulifadhiliwa na Serikali ya China.

No comments:

Post a Comment