Sunday, 20 October 2013

CUF kuhakikisha kila Mzanzibari anapata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi


Na Khamis Haji,  OMKR
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama hicho kimedhamiria kuhakikisha kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 anapata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (ZANID) ifikapo mwezi Julai mwakani.
Maalim Seif amesema hayo alipokuwa akihutubia wanachama wa chama hicho katika matawi na Baraza mbali mbali zilizopo katika Wilaya ya Magharibi Unguja, alipokuwa katika ziara ya siku mbili kukagua uhai wa chama.
Hatua hiyo aliitangaza baada ya kujitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wanachama na wapenzi wa CUF kuwa wamekuwa wakinyimwa kwa makusudi vitambulishi hivyo kutokana na kile wanachoamini ni sababu za kisiasa.
Wanachama hao, katika majimbo ya Bububu, Mtoni, Mfenesini, na Dimani wamewatuhumu baadhi ya Masheha kushirikiana na watendaji wa Ofisi ya Vitambulisha vya Mzanzibari Mkaazi, kuwanyima haki hiyo, ikiwemo baadhi yao kuzunguushwa licha ya kuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Walisema uonevu huo unafanyika, licha ya kuwa vitambulisho hivyo vina matumizi mengi muhimu zaidi ya kutumika kwenye kupigia kura, ikiwemo kumuwezesha mwanchi kupata ajira, mikopo, hati ya kusafiria na hata huduma ya kuunga maji na umeme nyumbani.
“Hatukubali tena, lazima iwe mwisho, lakulifanya tutalijua sisi, wala hatutajali mtu ana itikadi gani, awe CCM, awe CUF au Chadema au hana chama, madhali ni Mzanzibari ana sifa tutahakikisha ifikapo Julai mwakani ana ZANID”, alisema Maalim Seif.  
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, wakati kuna Wazanzibari walio wengi wananyimwa vitambulisho hivyo, kuna baadhi ya watu wasiokuwa Wazanzibari mara wanapofika Zanzibar hutafutiwa ZANID na kupelekewa majumbani.
“Mnawanyima wananchi haki yao kwa mujibu wa sheria eti kwasababu tu mnaogopa kushindwa katika uchaguzi, hii ni dhulma … Chama cha Afro Shirazi nchi hii kilifanya Mapinduzi kupinga dhulma, na sisi basi tunasema hatuwezi tena kuvumilia dhulma hii”, alisema Katibu Mkuu wa CUF.
Alisema uvumilivu mara zote una mwisho na kuwaonya wote wanaohusika na utoaji wa vitambulishi hivyo waache tabia hiyo, ili kuiepusha nchi kuingia kwenye matatizo.
“Uvumilivu mara zote una mwisho, msitusukume hadi tukafika ukutani, athari zake zinaweza kuwa mbaya kabisa”, alionya Maalim Seif.  
Malalamiko hayo ya CUF yamekuja, licha ya kutolewa kauli kutoka kwa viongozin wa Serikali ya Zanzibar yenye muundo wa umoja wa Kitaifa, kuahidi kwamba wananchi wote wenye sifa watapatiwa vitambulisho vya ZANID.
Miongoni mwa waliowahi kutoa ahadi hizo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, ambapo pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alitoa kauli kama hizo na kuchukua juhudi kadhaa, ikiwemo kuwakutanisha wadau wa vitambulisho hivyo na viongozi wa CUF.
Hata hivyo, katika ziara hiyo ya Katibu Mkuu wa CUF, baadhi ya wanachama walieleza kuwa wameanza kupatwa na mashaka, huenda kauli hizo zikawa zinatolewa hadharani, lakini nyuma ya pazia kuna maagizo mengine ya kunyimwa vitambulisho hivyo.
Maalim Seif aliwaagiza watendaji wa chama hicho katika ngazi za matawi, majimbo na Wilaya kuorodhesha wanachama wote ambao wamenyimwa vitambulisho hivyo, ili chama kiweze kujua hali halisi ya tatizo hilo na kutafuta njia muafaka za kulitatua.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu wa CUF, pia alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama wa CUF kuzidi kukiimarisha chama chao kwa kuendeleza utaratibu wa vikao na kuepuka makundi, wakati huu ambapo uchaguzi ndani ya chama hicho unakaribia.
Aliwatahadharisha baadhi ya viongozi na wanachama wenye tabia ya kujenga mitandao na makundi ndani ya chama kwa dhamira ya kupitisha watu wao kuwa wagombea Ubunge au Uwakilishi kuacha tabia hiyo haraka, kwa kile alichoeleza kuwa sasa CUF hakitaivumilia.
“Kuna tabia ya kuanzisha mitandao kwa baadhi ya viongozi, kama njia ya kujipanga kupata Ubunge au Uwakilishi, chama kimeagiza kufuatiliwa wenye tabia hiyo, na atakayethibitika kapita kwa njia hizo tutafuta uteuzi wake”, alitahadharisha.
Aidha, alisema kuna tabia ya viongozi wengine kuchaguliwa majimboni, lakini baada ya kushinda hawaonekani tena, amewataka wanachama kuwa macho na kuhakikisha wanawachagua wanachama ambao wako tayari kuwatumikia wanachama na wenye uchungu na chama chao.
Akizungumza huko katika jimbo la Bububu, Mkurugenzi wa Uenezi, Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani alisema chama hicho kina laani kwa nguvu zote hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwavunjia nyumba wananchi wa Bububu Magengeni na Mwanyanya.
Alisema kwamba uvunjwaji wa nyumba hizo umefanywa bila ya kuzingatia taratibu na sheria na huenda umefanyika kutokana na msukumo wa kisiasa, baada ya kuonekana wakaazi wengi wa eneo hilo ni wafuasi wa chama cha CUF.
Alielza kuwa CUF kinataka uchunguzi wa kina ufanywe juu ya hatua ya kuvunjwa nyumba hizo zipatazo 300, kitendo ambacho ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu, kwa vile wananchi wengi wamekosa mafali mwa kuishi na kupata hasara kubwa, bila ya kulipwa fidia.

No comments:

Post a Comment