Tuesday, 22 October 2013

Busara za JK zimefufua matumaini ya Wananchi


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Ireland nchini, Fionnula Gislen katika hoteli ya Serena Dar es Salaam (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Ireland nchini, Fionnula Gislen katika hoteli ya Serena Dar es Salaam (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema busara za Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete zimefufua matumaini ya wananchi wengi kuweza kupatikana Katiba mpya, baada ya kujitokeza changamoto ambazo ziliwafanya kuanza kuvunjika moyo.
Maalim Seif ameyasema hayo leo 22/10/2013 huko hoteli ya Serena Dar es Salaam alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Fionnuala Gilsenan yaliyohusu mambo mbali mbali, ikiwemo maendeleo ya mchakato wa kupatikana Katiba mpya Tanzania.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema baada ya kujitokeza malalamiko yaliyotokana na kuletwa mswada wa mabadiliko ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais Kikwete Oktoba 14 mwaka huu aliamua kukutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini.  
Amesema katika mazungumzo ya Rais na viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini, walikubaliana viongozi wa vyama hivyo wawasilishe mapendekezo yao yatakayosaidia kupatikana Katiba nzuri na kumaliza malalamiko na mivutano iliyojitokeza.


Maalim Seif alisema pande hizo zilikubaliana kwamba mazungumzo hayo yataendelea na yatakuwa chini ya Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), ambapo vyama vyote vya siasa vitakuwa na fursa ya kutoa na kuwasilisha yale wanayoona yanapaswa kuwemo au kutolewa ili baadaye yafikishwe bungeni kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
“Ni kwa uamuzi wa busara kama aliouonesha Rais Kikwete hali ya kukosekana mafahamiano itaweza kuepukwa na nchi yetu itaweza kupata Katiba itakayokidhi mahitaji ya wananchi” alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alieleza kuwa baada ya hatua hiyo ya Rais Kikwete kuweza kukaa pamoja na wadau muhimu katika zoezi la kutafuta Katiba Mpya, viongozi wa vyama wamefurahi na wako tayari kushiriki kikamilifu kufanikisha lengo lililokusudiwa.


Akizungumzia Muungano, Maalim Seif amesema wananchi walio wengi wanataka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uendelee kutokana na mahusiano na maingiliano ya miaka mingi, hata kabla ya nchi mbili hizo kupata uhuru, lakini pia alisema Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ya kujiamulia mambo yake, ndiyo itakayoweza kuufanya Muungano huo imara zaidi.

“Hata katika maoni ya wananchi hakuna Mzanzibari aliyetaka Muungano huu uvunjwe, lakini kwa upande wa Tanzania Bara walikuwepo asilimi nane, hali hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani Wazanzibari wanavyopenda Muungano uwepo”, amesema.
 
Aidha, Balozi huyo wa Ireland akizungumzia haja ya kudumishwa amani na utulivu, alikubaliana na ushauri wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, juu ya haja ya mataifa kushirikiana katika kupiga vita matukio ya uvunjifu wa amani pamoja na ugaidi.
 
Balozi Gislenan alisema vitendo vya ugaidi havina mipaka na nchi yoyote ile inaweza ikalengwa, kama ilivyojitokeza hivi karibuni nchini Kenya kwenye eingo la maduka la West Gate.
 
Amesema ni wajibu wa mataifa yote kushirikiana na kuwa na mikakati ya pamoja kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayatokei, pamoja na kuwasaka wale wote wanaojihusisha ili waweze kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

No comments:

Post a Comment