Monday, 16 April 2012

Picture
Mwezi Februari mwaka huu, habari zilichapishwa kuhusu "ushindi" wa Serikali katika al maarufu ‘Kesi ya Samaki wa Magufuli’ iliyokuwa ikiwakabili wavuvi raia wa China wamiliki wa meli ya Tawariq 1 waliofanya uvuvi haramu katika pwani ya Bahari ya Hindi, kwenye maji yaliyo katika eneo la Tanzania.

Mwezi huo huo wa Februari, gazeti la Nipashe likachapisha habari kutahadharisha kuwa meli hiyo inazama si tu kutokana na kile mlinzi wa eneo hilo alichosema ni kupigwa na mawimbi makubwa ya maji ya bahari, bali pia kuwepo kwa tuhuma kuwa mali na vifaa vya meli hiyo vinahujumiwa na baadhi ya watu ambao ni maafisaa wa bandari.
  • Alipotaarifiwa na wanahabari walioshuhudia meli hiyo ikiwa imeegama upande na kuulizwa ikiwa analifahamu hilo, Mkuu wa Kikosi cha Polisi cha Wanamaji, ASP Mboje Kanga naye aliuliza, “Sasa kukaa upande ni kuzama?” ... “Wewe umeiona?” halafu, “Maana unafanya kazi ukiwa ofisini hilo ndilo tatizo lenu!”
  • Alipotakiwa kueleza sababu za meli hiyo kukaa upande alijibu, “Mimi si msemaji; hiyo meli ipo chini ya Mahakama, kawaulize wao wanaweza kusema chochote. Mimi sihusiki.”
  • Alipotakiwa kueleza jitihada zinazofanyika ili kuhakikisha haizami akasema, “Tayari watu wanahangaika kuiokoa ili isizame, tunafanya kila jitihada kuiokoa na tumeshaanza kufanya hivyo.”


    Serikali/Tanzania imeshinda kesi; Ndiyo, ni sawa na haki kabisa kuonesha 'hatuna utani'; Ninachojiuliza ni je, Hasara ya meli hii ikiwa ni mali ya Wachina, ikizaa kesi nyingine, tunao uhakika kweli wa kushinda tena kesi? au ndiyo tutaingia kwenye deni la gharama kubwa zaidi? Serikali yenyewe kila leo inalia na ukata, bajeti za Wizara kila mwaka wa fedha ni kuhemea kwa wafadhili na mikopo ya riba za kupaa, itazikamua wapi fedha za kutetea tena kesi nyingine mahakamani?

    Ikiwa meli hii ni mali ya Serikali baada ya kushinda kesi, hujuma iliyofanyiwa na hasara inayopatikana kwa kuzama au kuja kuikarabati, tutakuwa tumetia adabu au tumetiwa adabu? Inanikubusha kesi ya Mpare na Mchagga, Mpare anakwenda kuuza ng'ombe ili apate fedha ya kumshinda Mchagga kwenye kesi ya kuku! (ni utani wa watani hao wanajuana).

    Hii nchi kweli ya watu makini sana (sigh). Ukisema kinyume utaambiwa macho yako hakuna lolote zuri linayoona; Kazi ni kutafuta, kuona na kuhesabu mabaya na kukosoa tu!

    Haya bana, kula uliwe! fanyeni mtakavyo, si mnaweza? Endeleeni!
Picture
 

No comments:

Post a Comment