Tuesday, 18 October 2011

Wasomi wataka Muungano usijadiliwe Katiba Mpya

 
Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi, amewatahadharisha Watanzania kuwa wakijadili baadhi ya mambo ya Muungano wakati wa kutoa maoni yao kwenye mjadala wa kuandika katiba mpya wanaweza kuuvunja.
Profesa Kabudi alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mjadala wa maadhimisho ya miaka 50 ya kitivo hicho, ambapo aliwataka wananchi kutogusa suala la Muungano wakati wa mjadala wa katiba mpya kwa kuwa linaweza kusabaisha nyufa au kuuvunja Muungano huo.
“Kuna vitu ambavyo kwa namna yoyote itabidi Watanzania wasivijadili katika mjadala wa kitaifa unaolenga kukusanya mawazo ya wananchi kabla ya kuandikwa kwa katiba mpya,” alisema.
Aliongeza kuwa ikiwa vitu alivyosema vitajadiliwa na wananchi vinaweza kusababisha ufa miongoni mwa pande mbili zilizoungana mwaka 1964 Tanzania Bara zamani Taganyika na Zanzibar.
Akitoa mfano kuhusu Muungano, alisema kuna mambo yaliingizwa na waasisi katika Muungano ambayo yakianza kujadiliwa kwa sasa yanaweza kusababisha nyufa na hata kuuvunja Muungano huo.
Alisema Muungano huo ni wa kuigwa na nchi nyingi za Kiafrika na kwamba ikiwa wananchi wataujadili hali hiyo inaweza kuzua mawazo tofauti ambayo yanaweza kuudhofisha.

MAHAKAMA YA KATIBA
Aidha, Profesa Kabudi alishauri kuundwa Mahakama ya Katiba ambapo wananchi watapata fursa ya kwenda kuhoji miswada mbalimbali ya serikali kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Alisema kazi kubwa ya mahakama hiyo itakuwa ni kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu katiba yao pamoja na kuhoji miswada mbalimbali ya serikali ambayo inawasilishwa bungeni.
Mwanazuoni huyo alisema katiba mpya lazima ilenge kutatua matatizo ya wananchi na kusaidia upatikanaji wa maendeleo na sio inayokidhi matakwa ya wanasiasa kutaka kukaa madarakani.
“Lazima katiba mpya ijayo ilenge kusogeza mbele maendeleo ya wananchi wa mijini na vijijini na isiwe inayolenga kuwalinda watawala na matakwa yao ya kisiasa,” alisema.
Alitaka mambo muhimu ambayo yanawagusa wananchi yajadiliwe kwa kina ili yaweze kuingizwa kwenye katiba mpya ijayo.
Alisema katiba ijayo lazima iwahakikishie watu kuishi vizuri na kwamba ili hilo iweze kufanyika, ni lazima itokane na Watanzania wenyewe.
Profesa Kabudi alisema mijadala ya kubadili katiba sio jambo geni nchini kwa kuwa limewahi kufanyika mara kadhaa.

PROFESA WAMBALI: RAIS ASAIDIWE KUTEUA MAKAMISHNA WA NEC
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi Kitivo hicho, Profesa Michael Wambali, alipendekeza kuwa Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wateuliwe na taasisi maalum zinazojitegemea kwa kushirikiana na Rais ili kuondokana na malalamiko miongoni mwa wanasiasa na wananchi kila baada ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa katiba ya sasa, Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuwateua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na makamishna wa NEC.
Aidha, Profesa Wambali, alisema katiba mpya itenganishe nafasi ya Rais kuingilia utendaji wa Bunge ili kila mhimili ufanye kazi kwa kujitegemea.
“Kila baada ya uchaguzi unapomalizika panakuwa na malalamiko ya kudhulumiwa kura, ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuhusu suala hilo, lakini kuna haja ya makamishna wa NEC kuteuliwa na taasisi zinazojitegemea kwa kushirikiana na Rais badala ya kazi hiyo kufanywa na Rais pekee,” alisema Profesa Wambali.
Alipendekeza kufanyike mkutano maalum kwa ajili ya kuzungumzia namna ya kupata katiba ambapo wananchi wote watapata fursa ya kushiriki na kutoa mawazo yao.

JAJI MANDIA ATAKA WANASHERIA WASAIDIE MJADALA
Akizungumza kwa niaba ya Jaji wa Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othuman Chande, Jaji William Mandia, alisema wanasheria wanachangia maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali.
Aliwataka wanasheria kutumia ujuzi wao wa kisheria kuwaongoza wananchi katika kujadili na kuchangia mawazo yao katika mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya unaoendelea nchini.
Baaadhi ya watu waliohudhuria hafla ya kutimiza miaka 50 ya kitivo hicho ni pamoja na majaji, wahadhiri, majaji wastaafu, wanafunzi wanaosomea sheria na wadau wengine wanaofanya kazi katika taasisi zinazojihusisha na masuala ya sheria.

No comments:

Post a Comment