Tuesday, 18 October 2011

Wanasheria wataka Mahakama ya Katiba  
Ellen Manyangu
WATAALAMU wa sheria wameshauri Katiba mpya inayotarajiwa kuundwa, iwe na kipengele cha kuanzishwa kwa Mahakama ya Katiba yenye uwezo wa kutatua migogoro ya kikatiba.Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam, walisema uundwaji wa mahakama hiyo, utasaidia kupata ushauri wa mambo mbalimbali ya kisheria kuhusu masuala ya kikatiba.

Walisema hayo wakati wa ufunguzi wa sherehe za miaka 50 ya uhuru katika Kitivo cha Sheria cha Chuo kikuu cha Dar es Salaam.Akiwasilisha mada yake kwenye hafla hiyo, Mkuu wa kitivo hicho cha sheria,  Profesa  Palamagamba Kabudi,  aliwataka watanzania kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kupata Katiba mpya.

“Uundaji wa Katiba usiwe wa makabatini bali uwe wa wananchi na uzingatie yanayolengwa kufanywa. Wananchi watunge na kutoa maoni wenyewe na sio kujengewa Katiba na watu wengine au kulishwa maneno,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema wanasheria wameamua kulisemea jambo hilo kwa kuwa uundaji wa Katiba ni jambo nyeti kwa mustakabali wa taifa na maendeleo yake.Mwanansheria Tom Nyanduga kutoka nchini Kenya aliishauri serikali kuwa kuongoza kwa makini mchakato huo wa Katiba mpya badala ya kuwaachia wanaharakati.

“Kila mtu kwa ngazi yake na majukumu yake katika serikali afanye wajibu wake katika kuhakikisha katiba mpya inakuwa na mahitaji  muhimu na ya kutosha,” alisema Nyanduga.

Awali akizindua sherehe hizo kwa niaba ya Jaji mkuu wa Tanzania Jaji Williamu Mandia, alisema kitivo hicho cha sheria kimekuwa na msaada mkubwa kwani matunda yake yanaonekana nchini na nje ya nchi.

“Kitivo hiki kina haki ya kujivuna kwa kutimiza mika 50 kwani kina matunda ambayo  yamekuwa ni msaada mkubwa kwa serikali,jamii,wanasiasa na hata katika hoja na maoni mbalimbali katika uudwaji wa Katiba”alisema Mandia.

No comments:

Post a Comment