Tuesday, 25 October 2011

Wabunge kizimbani

 
 
Wabunge wenye kesi za jinai sasa ni 13
10 wa Chadema, CCM wawili, CUF mmoja
Lile wimbi la kufunguliwa kesi za jinai dhidi ya wabunge limezidi kuongezeka, baada ya Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dk. Hamisi Kigwangallah (CCM), kuingia katika orodha hiyo na sasa kufikisha idadi ya wabunge wenye kesi katika mahakama tofauti kufikia 13 tangu Januari mwaka huu.
Jana Dk. Kigwangallah alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, akikabiliwa na makosa sita, likiwamo ya kuvamia kituo cha polisi.
Dk. Kigwangallah akipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza, Mbunge wa Mbarali kupitia (CCM), Modestus Dickson Kilufi, jana alipandishwa tena kizimbani na kuanza kutolewa ushahidi katika kesi ya kutishia kuua kwa maneno inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.
Dk. Kigwangallah alishikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Nzega juzi akiwa na wafuasi wake watatu, Mrisho Hamisi, Methew Dotto na Mwanja Mwandu ambao ni wakazi wa Kata ya Nata. Watu hao ni miongoni mwa wachimbaji wadogo ambao wanahusishwa na vurugu hizo zilizo tokea juzi katika kijiji cha Mwabangu.
Waendesha mashitaka wa Polisi, Merito Ukingoji na Joseph Mbwana, walidai mahakamani kuwa watuhumiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali juzi katika mgodi mdogo wa wachimbaji wadogowadogo uliopo katika kijiji hicho.
Katika kosa la pili na la tatu, wanatuhumiwa wanadaiwa kuingia katika mgodi wa machimbo ya dhahabu wa Resolute bila idhini ya wamiliki na kuvamia kituo cha polisi cha Nzega majira ya saa mmoja jioni.
Waendesha mashitaka hao walidai kuwa, kosa la nne linalowakabili watuhumiwa hao ni kupanga njama katika ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nzega na kufanya maandamano kuvamia kituo cha polisi.
Pamoja na tuhuma hizo, Kigwangallah na Mwanja Mwandu wanatuhumiwa kwa makosa mawili ya kupiga na kujeruhi.
Waendesha mashitaka hao walidai kuwa, Kigwangallah na Mwandu waliwapiga Mosesi Kichambi na Ferdinand Yusuph na kuwajeruhi wakati wa mapambano hayo eneo la mgodi.
Waliiambia mahakama kuwa upelelezi unaendelea kubaini chanzo cha vurugu hizo.
Ukingoji alidai kuwa Kigwangallah amewekewa pingamizi la kutofika eneo hilo la mgodi huo ili kuepusha tafrani ambayo inaweza kujitokeza kati ya wananchi hao na wawekezaji.
Alidai kuwa mahakama inatambua kuwa Kigwangallah ni mbunge wa jimbo hilo na anapaswa kutembelea wananchi wake wa eneo hilo, lakini kwa sababu suala hilo liko mahakamani litatatuliwa na mahakama.
Watuhumiwa wote walikana mashitaka dhidi yao mbele ya Hakimu Mkazi Wilaya, Ajali Milanzi.
Hata hivyo, Dk. Kigwangallah, alipewa dhamana baada ya kujidhamini mwenyewe kupitia nafasi ya ubunge na kuwadhamini washitakiwa wenzake watatu na kutakiwa leo kuwafikisha mahakamani watu watakaowadhamini, vinginevyo mahakama hiyo itawafutia dhamana washitakiwa wote.
Hakimu Milanzi aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 18, mwaka huu,
Dk. Kigwangallah aliomba mahakama hiyo kuwa tarehe iliyopangwa atakuwa katika vikao vya Bunge hivyo hataweza kuhudhuria. Hata hivyo Hakimu Mianzi alimruhusu.
DK. KIGWANGALLAH ANGURUMA
Akizungumuza na waandishi wa habari, baada ya kesi kuahirishwa, Mbunge huyo alisema kitendo hicho cha kumuweka ndani kimemdhalilisha kwa kuzingatia kuwa alikuwa anadai haki ya wananchi wake ambao wamekuwa wakionewa mara kwa mara na wawekezaji hao.
Nimeshangazwa na jeshi la polisi hasa OCD kunibambikia makosa ambayo hayana ukweli pamoja na kunidhalilisha kwa kunipiga vibao kama mtoto mdogo na dhihaka mbalimbali kwa wananchi wangu ambao walikuwa wakidai haki yao ya msingi. Hii si haki, sikutendewa haki katika hili ni uonevu mtupu,” alisema Kigwangallah.
KESI YA WABUNGE CHADEMA YAAHIRISHWA
Katika hatua nyingine, kesi inayowakabili wabunge wawili wa Chadema, Silvester Kasulumbai (Maswa Mashariki) na Suzan Kiwanga (Viti Maalum) ya kumdhalilisha Mkuu wa wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, imeahirishwa hadi Desemba Mosi, mwaka huu, ambapo washitakiwa watasomewa maelezo ya awali. Washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
USHAHIDI DHIDI KILUFI WAANZA KUTOLEWA
Katika kesi dhidi ya Kilufi, Shahidi wa kwanza, Jordan Masweve, ambaye ni mlalamikaji, aliiambia mahakama kuwa Machi 16, mwaka huu aliongozana na Diwani wa kata yake, Alex Paulo, kwenda katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Shahidi huyo ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Rwiwa, alidai kuwa akiwa katika majengo ya halmashauri hiyo, aliingia katika ofisi tatu tofauti na alipomaliza shida zake alirejea kwenye gari kurejea nyumbani.
Alidai kuwa alipofika kwenye gari, alikuta simu ya Diwani Paulo ikiita wakati mwenyewe akiwa umbali mfupi wakizungumza na Kilufi.
Alidai kuwa aliichukua simu ya Paulo kwa ajili ya kumpelekea, lakini kabla hajafika katika eneo ambalo Paulo alikuwa akizungumza na mshitakiwa, Kilufi alimtahadharisha kuwa asifike kwenye eneo hilo na kumtaka aende akajisalimishe kwake ndani ya wiki mbili, huku mbunge huyo akijisifu kuwa asipojisalimisha atamuonyesha kwa kuwa ana marafiki wengi ambao ni watu wakubwa serikalini, akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria.
Alidai kuwa baada ya kuambiwa hivyo, aliamua kuondoka, lakini Kilufi alianza kumrushia matusi kwa kumwambia kuwa yeye (Masweve) ni mpumbavu.
Alidai kuwa baada ya kitendo hicho, aliamua kwenda moja kwa moja katika kituo cha Polisi kwa ajili ya kufungua jalada dhidi ya Mbunge Kilufi.
Baada ya kumaliza utetezi wake, Wakili wa Serikali, Apimak Mabrouk, alimuuliza maswali kama baada ya kutokea tukio hilo alimwarifu mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Baada ya kubabaika kidogo, Masweve alijibu kuwa alitoa taarifa kabla ya kwenda Polisi, maelezo ambayo yalipingana na yale aliyoyatoa wakati wa akitoa ushahidi wake.
Wakili Mabrouk alimuuliza tena kama wakati tukio hilo likitokea walikuwepo watu wengine. Masweve alidai kuwa walikuwepo wao wenyewe.
Shahidi wa pili, Alex Paulo ambaye ni Diwani wa Kata ya Rwiwa, akitoa ushahidi wake, alidai wakati wakiendelea na maongezi na Mbunge Kilufi, alisikia Mbunge huyo akijibizana na Masweve, akimtaka aondoe kesi mahakamani na kama asipofanya hivyo atamtoa roho.
Alidai kuwa baada ya kutolewa vitisho hivyo, aliongozana na Masweve kwenda kumweleza Mkurugenzi wa Wilaya, George Kagomba, ambaye aliwashauri kwenda kuripoti suala hilo Polisi.
Wakili Mabrouk alimuuliza maswali kadhaa ambayo shahidi huyo aliyajibu kwa ufasaha na ndipo Hakimu Michael Mteite alipomwita shahidi wa tatu kuendelea na ushahidi.
Askari wa Jeshi la Polisi namba PC 5I03 Koplo Andrew wa Idara ya Upelelezi katika kituo cha Polisi cha Rujewa, alidai kuwa alipewa kazi ya kupeleleza kesi hiyo na alipoanza kuifuatilia aligundua kuwa inamuhusu Mbunge na ndipo alipoipeleka kwa bosi wake ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mbarali ambaye pia alimrudishia ili aifanyie kazi.
Alidai kuwa baada ya kurudishiwa kesi hiyo alimwita Mbunge kwa kumpigia simu, lakini alimjibu kuwa alikuwa bungeni na aliporudi kutoka bungeni alikwenda moja kwa moja kituo cha Polisi Rujewa kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo ya awali.
Baada ya maelezo hayo, Wakili Mabrouk alimuuliza shahidi huyo kuwa ilikuwa vipi kesi hiyo ikapelekwa Mahakama ya Mkoa badala ya Mahakama ya Wilaya ya Mbarali. Shahidi huyo alijibu kwa kudai kuwa kwa kuwa mahakama zote zinatumia sheria sawa, waliamua kuipeleka kwenye mahakama hiyo.
Wakili Mabrouk pia alitaka kujua sababu za kesi hiyo kuchelewa kufikishwa mahakamani, na PC Andrew alidai kuwa upelelezi wa suala hilo ulikuwa haujakamilika.
Baada ya upande wa mashahidi kumaliza kutoa ushahidi, Hakimu Mteite alimtaka Mbunge Kilufi aanze kujitetea, lakini mawakili wa Serikali walipinga kwa madai kuwa walikuwa hawajajiandaa kwa ajili ya kusikiliza upande wa utetezi.
Hakimu Mteite aliamua kuiahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo Kilufi ataanza kujitetea na kujibu hoja za upande wa mashtaka.
Mbali ya kesi zinazowakabili Kasulumbai, Kiwanga, Kigwangala na Kilufi, wabunge wengine tisa wanakabiliwa pia na kesi za jinai.
Wabunge hao ni pamoja na wa Chadema Freeman Mbowe (Hai), Joseph Selasini (Rombo), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini) walioshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha kwa kuandamana bila kibali jijini Arusha Januari 5, mwaka huu.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), anashitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mbeya kwa kosa la kufanya mkutano bila kibali cha polisi Mei mwaka huu.
Naye Mbunge wa Meatu (Chadema), Meshack Opurukwa, anashitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mwa kufanya mkutano zaidi ya muda unaotakiwa kisheria katika jimbo lake mapema mwaka huu.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Ester Matiko, wanashitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara kwa kosa la kuzuia uchukuaji wa maiti za watu waliouawa katika uvamizi wa mgodi wa North Mara Februari mwaka huu.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Magladena Sakaya na wenzake kadhaa, wana kesi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora kwa kufanya mkutano bila kibali.
Imeandikwa Lucas Macha, Nzega; Furaha Eliab na Emmanuel Lengwa, Mbeya.

No comments:

Post a Comment