Friday, 8 July 2011

Waziri wa Ardhi Maakazi Maji na Nishati Ali Juma Shamhuna awasilisha bajeti ya wizara yake

Waziri wa Ardhi Makaazi Maji na Nishati Ali Juma Shamhuna amepumzika kabla ya kusoma hotuba ya bajeti ya wizara yake katika Baraza kla Wawakilis
Mbweni Zanzibar
Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) imesema Dhamira ya kulitoa suala la Mafuta na Gesi Asilia katika Orodha ya Muungano iko palepale. Akisilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Maji na Nishati,Waziri wa Wizara hiyo, Ali Juma Shamuhuna alisema suala la utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia limepewa kipaumbele. “Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wajumbe bado msisitizo umewekwa katika kuihuisha Nishati hii kuwa ni muhimili mkubwa wa Uchumi wetu” Alisema Waziri Shamuhuna. Waziri huyo ameliambia Baraza la Wawakilishi kwamba Mpango wa utekelezaji wa Sera ya Nishati umeshaandaliwa na kupelekwa katika Ubalozi wa Sweden kwa kuomba ufadhili katika kipindi cha awamu ya pili ya mradi wa Sera ya Nishati ambacho kiko katika matayarisho. Akizungumzia Sera ya Nishati, Waziri huyo alisema Sera ya Nishati ya Zanzibar ilikamilika na kupitishwa rasmi na Baraza la Mapinduzi Disemba 2009. ”Mheshimiwa Spika, Baadae Sera hiyo ililetwa katika Baraza lako Tukufu Januari 2010 kwa kupata baraka za Wajumbe” Alisema Waziri huyo. Waziri Shamuhuna ameongeza kwamba kwa kuwa Uchumi sio suala la Muungano, ushughulikiaji wa rasilimali ya Nishati ya Mafuta na Gesi Asilia haupaswi kuwa suala la Muungano. Akizungumzia Mradi wa Maji safi na salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Waziri Shamuhuna alisema Kazi inayoendelea sasa ni majaribio ya mradi kwa kuyapeleka maji kwa wananchi, katika maeneo mbalimbali ya mji. Waziri huyo alisema mradi huo uliogharimu Tsh Bilioni 32 ambao umekamilisha ujenzi wa awamu ya pili kwa ufadhili wa serikali ya Japani kwa thamani ya Tsh Bilioni 20. Mradi huo umejenga matangi makubwa mawili (yenye ujazo wa lita 1, 200,000 na 2, 700,000), visima vitano (5) na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 21 kwa sasa umekamilika. Hata hivyo, Waziri huyo alisema kutokana na uchakavu wa mabomba, mafanikio ya mradi huo hayajaonekana sana kwa baadhi ya maeneo, kwa sababu maji mengi yanapotea ardhini kabla ya kuwafikia watumiaji. Waziri Shamuhuna ameongeza kuwa pamoja na kuendelea na majaribio, hivi sasa Mamlaka ya Maji Zanzibar inaendelea na kazi za kubadilisha mabomba yaliyochakaa na kuweka mapya, kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa mradi huo.

No comments:

Post a Comment