Dr. Shein afanya Uteuzi
Rais wa Zanzibar Dr. Shein amteua Ali Mzee kuwa mjumbe wa Baraza La Wawakilishi Zanzibar.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein amemteua Ali Mzee Ali kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,Dk Abdulhamid Yahya Mzee imesema Rais amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa kifungu 66 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Ali Mzee aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kipindi kilichopita ambapo pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi. Uteuzi huo unaanza leo Julai 8 mwaka huu.
Pia Rais Dk Shein amemteua Abdulrahman Mwinyi Jumbe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Watu wa Zanzibar(PBZ). Jumbe amekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya PBZ katika kipindi kilichopita.
Aidha, Dk Shein amemteua Ali Abdalla Suleiman kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa barabara Zanzibar kuchukua nafasi ya Masauni Yussuf Masauni. Kabla ya uteuzi huo, Ali Abdalla aliwahi kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Kiongozi.
Pia Rais amemteua Abdulnassir Ahmed Mohammed Abdulraman kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Bima Zanzibar.
Rais Dk Shein amemteua Salum Khamis Nassor kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Vitega Uchumi Zanzibar(ZIPA) Mkurugenzi huyo anaendelea na nafasi yake hiyo.
Pia Rais amemteua Mohammed Hafidh Rajab kuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Uteuzi huo uliofanywa na Rais Dk Shein wote umeanza leo Julai 8 mwaka huu.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO)
08/07/2011

No comments:
Post a Comment