Sunday, 3 July 2011

SEMINA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA KWA WAWAKILISHI




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifungua semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Utambuzi na usajili wa Vitambulisho vya Taifa,katika ukumbi wa Ocean View Hotel Kilimani Zanzibar leo.(03/07/2011)
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipata hasara nyingi kwa kushindwa kuwatambua watu waishio nchini kutokana na kutokuwa na mfumo wa utambuzi na usajili wa watu Kitaifa.
.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa semina elekezi kuhusu Utambuzi na Usajili wa Watanzania kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi huko katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani mjini Unguja.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Dk. Shein alisema kuwa kutokuwepo kwa mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu kumeiathiri Tanzania kwa kiasi kikubwa sana katika uchumi, masuala ya jamii na usalama.
Alisema kuwa athari hizo zinaweza kuwa kubwa zaidi hasa pale Tanzania inapoingia kwenye soko huria la Afrika Mashariki ambapo kwa upande wa Zanzibar nayo inaguswa na kuhusika sana na atahari hizo.
Akizitaja baadhi ya hasara hizo Dk. Shein alisema ni pamoja na wananchi kuendelea kuwa katika umasikini kwa kushindwa kupata mikopo katika benki na taasisi za fedha ambapo alisema faida ya zoezi hilo litawasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Dk. Shein alisema kuwa baadhi ya benki zinatoza riba kubwa kufidia hasara wanayoipata kutokana na baadhi ya watu kutorudisha mikopo kwa sababu hawatambuliki.
Alisisitiza kuwa Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikipata matatizo na malalamiko mengi kwa kushindwa kumtambua mwanafunzi yupi anastahili mkopo na kwa kiasi gani pia, urudishaji wa mikopo hii umekuwa mgumu kwa kushindwa kuwapata wadaiwa mara baada ya kumaliza vyuo na hivyo serikali kupata hasara.
Kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na hasara unaofanywa na raia kutoka nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa msamaha wa Rais, ni wazi kuwa udhibiti wao umekuwa mgumu kutokana na kushindwa kuwatambua.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali imeendelea kubeba mzigo mkubwa wa gharama wakati wa zoezi la kupiga kura ikiwa ni pamoja na kupoteza fedha nyingi kila mwaka kwa kulipa watumishi hewa katika mfumo wa mishahara ya watumishhi wa serikali na kuwatoa hofu Watanzania na Taasisi za Haki za Binaadamu kwa kueleza kuwa zoezi hilo halina nia ya kuvunja au kukiuka haki ya mtu yoyote.
Alisema kuwa serikali imekuwa inapata matatizo na kuingia migogoro na wananchi wakati wa mazoezi ya kuwalipa fidia kutokana na kuchukuliwa ardhi au kubomolewa nyumba zao kwa sababu ya kushindwa kumtambua mmiliki sahihi na anachokimiliki.
Kutokana na hayo alisema kuwa imegunduliwa umuhimu wa kutoa vitambulisho hivyo utaratibu ambao tayari umeshaundiwa mamlaka na kuipongeza mamlaka hiyo kwa hatua iliyofikia ya kupata Mkandarasi wa kutengeneza Vitambulisho vya Taifa.
Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kwa Wajumbe hao kuwa semina hiyo itawaongeza ari ya kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi, katika Majimbo na maeneo yao wanayoishi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vitaendelea kuwepo na kutumika kwa madhumuni yaloe yale yaliyokusudiwa.
Alisema kuwa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vimesaidia sana katika mambo kadhaa, kama vile kufanya uchaguzi ulio haki na huru, jambo ambalo limeipatia sifa kubwa Zanzibar kwa Jumuiya za Kimataifa.
Alisema kuwa Vitambulisho hivyo vya Mzanzibari Mkaazi vimesaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na hata katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu ambapo pia, vimezisaidia Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutengeneza vitambulisho vya watumishi kazi ambayo inaendelea.
Sambamba na hayo Dk. Shein alitoa wito kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kutumia uzoefu wa miaka sita walionao Ofisi ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ili kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa Tanzania. Na kueleza kuwa taasisi hiyo imetunukiwa cheti cha ubora kutoka ‘International Standard Organisation’, kutokana na ubora wake.
Mapema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Shamsi Vuai Nahodha alitoa wito kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuitumia vizuri fursa ya maelekezo na ushauri wake katika kutekeleza mradi huo mkubwa.
Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho, akitoa neno la shukurani kwa Mhe. Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa niaba ya Wajumbe hao kwa kupata semina hiyo muhimu.




 PICHA ZAIDI ZA UFUNGUZI WA SEMINA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifungua semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Utambuzi wa usajili na Vitambulisho vya Taifa,katika ukumbi wa Ocean View Hotel Kilimani Zanzibar jana,(kulia) Makamo wa Pili wa Rais Balozi Sei Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya utambuzi na usajili wa Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maina,akizungumza akitoa taarifa kuhusiana na mamlaka ya vitambulisho wakati wa ufunguzi wa Semina kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein

Baadhi ya watendaji wa Mamlaka ya utambuzi na usajili wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakisikiliza kwa makini hotuba iliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifungua semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Utambuzi wa usajili wa Vitmbulisho vya Taifa,katika ukumbi wa Ocean View Hotel Kilimani Zanzibar jana

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,wakimsikiliza Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akitoa hotuba yake katika ufunguzi wa Semina ya wajumbe hao inayohusu usajili wa vitambulisho vya Taifa,iliyoandaliwa na Mamlaka ya Utambuzi na Usajili vitambulisho vya Taifa,(NIDA) katika ukumbi wa Ocean View Hoteli Kilimani Zanzibar.


No comments:

Post a Comment