Sunday, 3 July 2011

BARAZA LAWAWAKILISHI LATANGAZA BEI MPYA ZA KARAFUU

                                     

                                                 

Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepandisha bei ya zao la karafuu kwa
asilimia 80 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa miaka 10 kufufua zao hilo.
Akitangaza bei mpya kwa waandishi wa habari jana katika ukumbi wa
Idara ya Habari(MAELEZO), Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko, Nassor
Ahmed Mazrui,alisema “Ili kulifanya zao la karafuu na biashara yake
iwanufaishe zaidi wakulima,Serikali imeamua kuanzia sasa kuwalipa
wakulima wa karafuu asilimia 80 ya bei ya kuuzia katika soko la
kimataifa”
Waziri Mazrui alisema katika msimu wa mwaka huu karafuu daraja la
kwanza itanunuliwa na Shirika la Biashara la Taifa(ZSTC) kwa kg
shilingi 10,000 wakati pishi yennye kiwango hicho itanunuliwa kwa
shilingi 15,000.
Karafuu daraja la pili itanunuliwa kwa kg shilingi 9,500 na pishi
shilingi 14,250 ambapo karafuu daraja la tatu itanunuliwa kwa shilingi
9,000 wakati pishi itanunuliwa kwa shilingi 13,500.
Alisema kuanzia mwezi Januari mwaka huu,Serikali ilianza kufuatilia
mwenendo wa bei ya karafuu katika masoko ya dunia kwa madhumuni ya
kuandaa bei mwafaka ya kununulia karafuu kulingana na soko la duania
la zao hilo.
“Utafiti huo wa mwenendo wa bei katika soko la dunia ulikusudiwa pia
kuiwezesha Serikali kuandaa Sera mwafaka ya bei kwa ajili ya
kuendeleza zao la karafuu…Kwa hayo yote mawili, Serikali imefanikiwa
vizuri sana” Alisema Waziri Mazrui.
Waziri huyo alisema ili kutekekeleza azma ya Rais Dk Ali Mohammed
Shein ya kuimarisha zao la karafuu, Serikali imeandaa na kuanza
kutekeleza mkakati maalim wa kuendeleza zao hilo kwa kipindi cha miaka
10.Alisema katika utekelezaji wa mkakati huo, Serikali itajielekeza
katika maeneo makubwa matatu ambayo ni kurekebisha muundo wa ZSTC kwa
kubainisha majukumu yake mapya,kuweka sheria mpya kwa ajili hiyo na
kuimarisha kiutendaji kwa kuajiri wafanyakazi wenye uwezo zaidi na
mbinu mpya za kibiashara.
Waziri Mazrui ameutaja mkakati wa pili ni kuimarisha mfumo na taratibu
za uendeshaji wa biashara ya karafuu kimataifa ikiwa ni pamoja na
kuipatia karafuu ya Zanzibar utambulisho maalim wa kimataifa ili
kudhibiti magendo na uuzaji holela wa karafuu za Zanzibar.
Mkakati wa mwisho umetajwa kuwa ni kuanzisha mfuko wa maendeleo ya
karafuu ambao pamoja na mambo mengine, utashughulikia kilimo cha zao
hilo,pamoja na kutoa huduma za kitaalam za kuendeleza karafuu.

No comments:

Post a Comment