| Mishahara sasa juu, Kashfa ya rada yaibuka bungeni |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia Ramadhan Semtawa, Dar na Leon Bahati, Dodoma SERIKALI imetangaza bungeni kuwa itatutumia Sh3.2trilioni katika mwaka wa fedha 2011/12, ambazo pamoja na mambo mengine zitapandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa kuzingatia vigezo maalumu, ikiwamo mfumuko wa bei za bidhaa na huduma. Kauli hiyo ya Serikali imekuja huku kukiwa na kilio cha muda mrefu kutoka Shirikisho la Vyama huru vya Wafanyakazi nchini (Tucta), kutaka nyongeza ya mishahara kwa watumishi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha. Hata hivyo, bila kutoa mchanganuo wa nyongeza ya mishahara kimadaraja kati ya kima cha chini na cha juu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, aliweka bayana bungeni mpango wa Serikali kurekebisha mishahara ya watumishi wake. "Mheshimiwa Spika, Serikali itarekebisha mishahara ya watumishi wake kwa kuzingatia kasi ya mfumuko wa bei, uwezo wa bajeti na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma," alisema Ghasia wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo. Baraza la Majadiliano limeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Sura 105 ya mwaka 2003. Waziri Ghasia akifafanua kwamba, katika mwaka huo wa fedha 11/2012, kiasi hicho cha Sh3.2trilioni mbali ya kurekebisha mishahara ya watumishi pia kitatumika kugharamia upandishwaji vyeo na kulipia madai ya malimbikizo na mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala na Taasisi za Serikali. "Aidha, kiasi hiki kimeongezeka kwa Sh938 bilioni ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 40.2, la fedha zilizotengwa kugharamia malipo hayo katika mwaka wa fedha 2010/2011," alisema. Ajira mpya Kuhusu ajira mpya, alisema katika mwaka wa fedha 2011/12, Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 64,024, huku kipaumbele kikiwa katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na Mifugo. "Aidha, Serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 80,050 wa kada mbalimbali," aliongeza. Kuhusu viongozi wastaafu, Ghasia alisema ofisi yake Itaendelea kuwahudumia Viongozi Wastaafu wa Kitaifa kwa mujibu wa Sheria ya Kuwahudumia Viongozi wastaafu wa Kitaifa Sura 225. Alisema Serikali itafanya upembuzi yakinifu na utafiti wa athari za kimazingira, utakaotokana na ujenzi wa Kituo cha Kuwaenzi Waasisi wa Taifa, kuandaa na kukamilisha michoro kwa ajili ya ujenzi wa jengo husika. Alifafanua kuwa jengo hilo litatumika kwa ajili ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuondokana na gharama kubwa za pango katika majengo ya Taasisi binafsi. Kashfa ya Rada Wakati huohuo, sakata la ufisadi katika ununuzi wa rada ambalo lilikuwa limeanza kuonekana kupoa limeibuka upya Bungeni ambapo Serikali imetakiwa kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha mahakamani watendaji wake ambao wanatuhumiwa kuhusika. “Mheshimiwa Spika, kwanza tunataka wahusika wote waliohusika na kashfa ya rada, akiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, wachukuliwe hatua zote za kinidhamu na kisheria kwa kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” alisema Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Susan Lyimo. Akitoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusu makadirio ya matumizi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Susan alisema kwamba, Serikali haina sababu ya kutafuta ushahidi kwa sababu uchunguzi uliofanywa na Idara ya Upelelezi wa Ufisadi (SFO) ya Uingereza, imeonyesha kuwapo kwa hongo na ukiukwaji wa sheria na taratibu katika mchakato wa ununuzi wa rada. Baadhi yawatuhumiwa katika kashfa hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Miundombinu wakati huo, Andrew Chenge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Johnson Mwanyika. Chenji ya Rada Licha ya kutaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani kambi hiyo ilieleza kupingana matakwa ya Serikali kutaka ipewe fedha za faini kutokana na ununuzi wa rada kutoka kwa kampuni ya BAE System. Kampuni ya BAE ndiyo iliyoiuzia Tanzania rada hiyo na baada ya uchunguzi wa SFO, imeamriwa kulipa fidia ya Sh29.3 milioni, lakini fedha hizo zipitia kwa asasi za kijamii za Uingereza ambazo zinahusika na maendeleo ya Watanzania. Susan alisema wapizani wanaunga mkono mpango wa kutoipatia Serikali ya Tanzania fedha hizo moja kwa moja, lakini wakapinga kitendo cha kupewa asasi za Uingereza zinazosaidia maendeleo ya Watanzania. “Kambi ya Upinzani inaona kuwa bila watuhumiwa hawa kuchukuliwa hatua ni dhahiri kuwa taifa haliwezi kuzilinda vizuri fedha hizo pindi zikilipwa,” alisema Susan. Alisema serikali imekuwa dhaifu katika kulinda fedha za umma kutokana na utamaduni wa kutochukua hatua kwa wahusika wa rushwa kubwa. “…… tunapinga fedha za rada kulipwa serikali yetu kwani haiaminiki, hasa ikitiliwa maanani kuwa fedha hizo zilipotea mikononi mwa serikali hii hii …na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuwawajibisha wahusika,” alisema. Kwa sababu hiyo aliliomba Bunge lijadili na kuazimia kuanzishwa kwa akaunti maalumu ya kuweka fedha hizo na isimamiwe na asasi zote zisizo za kiserikali hapa nchini, sekta binafsi na wawakilishi wa serikali. Alisema lengo la akaunti hiyo liwe ni kuendeleza shughuli za maendeleo kwa maslahi ya umma. Alisema uamuzi wa Uingereza wa kuazimia kutoa fedha hizo kwa asasi zisizokuwa za kiserikali zinazoisaidia Tanzania, ni udhalilishaji mkubwa kwa Watanzania. Kuhusu Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru), kambi hiyo ilitaka serikali kuifuatilia kwa karibu kutokana na hasara ambayo imekuwa ikitokana na usimamizi dhaifu wa kesi. Susan alinukuu ripoti ya uchunguzi ya Taasisi ya Agenda Participation, ambayo ilisema inaweka bayana kwamba Takukuru ni dhaifu katika kuchunguza na kusimamia kesi mahakamani. Alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ilishinda asilimia moja tu ya kesi zote Takukuru ilizofungua mahakamani, wakati asilimia 99 ilishindwa hivyo kulazimika kulipa fidia na malimbikizo ya mshahara kwa washtakiwa. Susan pia alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma pia iwashughulikie watumishi waliotajwa kwenye kashfa za Kagoda, Meremeta, Deep Green, Richmond, IPT na waliohusika katika mikataba mibovu ambayo inaendela kulitia hasara Taifa. Kauli ya Kamati Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana (CCM), aliitupia lawama Ofisi hiyo ya Rais, Menejimenti ya Umma kwa kushindwa kuwasimamia wafanyakazi. “Kuna baadhi ya watumishi katika ofisi za Serikali, wanafanya kazi kwa mazoea bila kuzingatia maadili ya kazi zao kwa kufika kazini kwa muda wanaotaka na kutoka kazini muda wanaotaka bila kufuata kanuni na sheria za kazi,” alisema Pindi. Alisema uzembe katika usimamizi ndio unaofanya wafanyakazi hao kutowajibika ipasavyo, hivyo akaomba kuwepo udhibiti, ufuatiliaji wa utendaji wa mfanyakazi mmoja mmoja na adhabu zitolewe kwa wazembe. Pia aliilaumu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Umma kwa kushindwa kuwa makini katika kuwawajibisha watumishi wake wanaolisababishia taifa hasara. Alitoa mfano kwamba, baadhi ya watumishi wanaoonekana kwenda kinyume na maadili wanajikuta wakihamishwa kutoa idara moja kwenda nyingine au taasisi moja kwenda nyingine. Alielezea kuwa jambo hili limekuwa likisababisha wafanyakazi kuwa wazembe na kutoogopa kufanya makosa, kwa sababu wanajua adhabu yao ni kuhamishwa. Alilaumu pia Ofisi hiyo kutokuwa na kumbukumbu za wafanyakazi jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya waliofukuzwa Serikalini kuajiriwa katika idara nyingine za umma bila kugundulika. |
No comments:
Post a Comment