Posho za wabunge balaa
Wakati wabunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakitangaza kufuta posho za vikao kwa wabunge na watumishi wengine wa serikali, ofisi ya Bunge imejiweka kando kwa kueleza kwamba haiwezi kuziondoa.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha na Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, alisema kutokana na msimamo huo wa Bunge, ameazimia kutosaini fomu ya mahudhurio anapongia kwenye vikao vya Bunge ili kuepuka kulipwa posho hizo.
Alisema msimamo wake kwa sasa ni kutotaka kabisa posho hizo “Nimekataa kwamba wala zisiingizwe kwenye mfuko wa maendeleo ya jimbo la Kigoma, wala zisiingizwe kwenye akaunti yangu.”
Zitto alifafanua kuwa “sitosaini fomu za mahudhurio kwa sababu ndizo zinazohalalisha malipo.”
Alisema ofisi ya Spika imemwandikia barua na kumweleza kuwa haitoweza kuacha kumlipa posho ya kikao kwa kuwa kufanya hivyo sio utaratibu wa Bunge.
“Pamoja na maelezo hayo, mimi bado naona ni makosa kwa wabunge kuendelea kulipwa posho kwa sababu tunalipwa mshahara kwa kazi hiyo…nimeshawasilisha barua kuelezea nia yangu ya kukataa kabisa posho za vikao kwa sababu ninalipwa mshahara,” alisema Zitto.
Alifafanua kuwa katika bajeti ya kambi hiyo, watapendekeza ukaguzi wa kina ufanyike kwenye taasisi 22 za umma ili kuthibitisha madeni yake. Hata hivyo, hakuzitaja taasisi hizo.
Kwa upande wake, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lisu, alisema “hoja yetu ni kuondoa huu utamaduni wa posho, unaangamiza taifa tuuondoe.”
Alisema ni jukumu la viongozi kupigania maisha ya Watanzania kwa ajili ya taifa lijalo.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alisema posho za vikao ni suala la sera. “Sijui itakuwaje lakini wenyewe (wabunge) wakae na kukubaliana…kama unavyoona wamegawanyika, sasa wakae wakubaliane.”
Hata hivyo, Dk. Kashilillah hakueleza kama msimamo wa wabunge wa Chadema utaweza kutekelezwa ama la.
No comments:
Post a Comment