Wakili ataka mawaziri warudi darasani |
Rais Jakaya Kikwete, akijibu maswali mbali mbali aliyoulizwa wakati wa Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji kwa nchi za Afrika lililoanza jana, jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi Raymond Kaminyoge WAKILI wa Kampuni ya FB Attorneys, Fayaz Bhojani jana alitoa mpya katika Jukwaa la Uwekezaji Afrika, lililoanza jijini Dar es Salaam, baada ya kueleza kuwa Mawaziri wa Serikali za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, hawana uelewa wa kutosha hivyo wanatakiwa kusoma. Akichangia hoja katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na marais wa nchi hizo, Bhojani alisema mawaziri hao wameshindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi. Viongozi waliohudhuria jukwaa hilo ni pamoja na Marais Jakaya Kikwete, Mwai Kibaki wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Piere Nkurunzinza wa Burundi, Dk Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Rwanda, Bernard Makuza aliyemwakilisha Rais Paul Kagame. “Mawaziri wetu wanatakiwa kurudi shuleni wakasome kwa sababu wanayoyaahidi hawayatekelezi na wakirudi siku nyingine, wanarudia tena kuahidi. Nadhani wanahitaji kwenda shule. Serikali ziwapeleke shule,” alisisitiza Bhojani. Kauli hiyo iliwafanya washiriki wa Jukwaa hilo kuangua kicheko huku baadhi wakimuunga mkono. Bhojani alisema hayo muda mfupi baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola lililoandaa Jukwaa hilo, Dk Mohan Kaul kukaribisha maswali na michango ya mawazo kutoka kwa washiriki. Rais Nkurunzinza ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo alikuwa wa kwanza kuwajibia mawaziri wake tuhuma hizo kwa kusema: “Mawaziri hawawezi kupelekwa tena shuleni kwa sababu walishamaliza masomo yao.” Kauli hiyo ya Rais Nkurunzinza iliungwa mkono na Rais Kikwete aliyesisitiza kuwa mawaziri hawawezi kurudishwa shuleni. Akizungumza na Mwananchi nje ya mkutano huo, wakili alisema: “Wengi wanapenda kuwaacha wananchi wakiwa wana furaha kwa ahadi zao zisizotekelezeka huku wakifahamu kwamba wanadanganya.” Hata hivyo, Bhojani hakutoa mifano. Mapema Rais Kikwete akizungumza kwenye ufunguzi wa jukwaa hilo aliwatoa hofu wawekezaji kwamba Serikali yake haitataifisha mali wanazowekeza nchini. Kikwete alilazimika kuwatoa hofu baada ya mmoja wao kutoka Kenya, Tito Wambui kuhoji usalama wa rasilimali zinazowekezwa nchini hasa baada ya Tanzania kufanya operesheni ya utaifishaji mwaka 1967. Alisema Serikali haiwezi kutaifisha mali za wawekezaji kwa kuwa sasa kuna sheria inayohusu uwekezaji, ambayo pamoja na mambo mengine, inawalinda wawekezaji na mali zao. “Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki zinafahamu umuhimu wa wawekezaji katika kukuza uchumi wa nchi. Ili kuvutia wawekezaji, sheria mbalimbali zimetungwa ili kutoa haki sawa kwa wawekezaji na serikali,” alisema Rais Kikwete. Rais Nkurunzinza aliwataka wawekezaji duniani kuwekeza katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akisema eneo hilo lina miradi mingi. Alisema ukanda huo kwa sasa una amani hivyo kuna fursa kwa wawekezaji kuchagua maeneo ya kuwekeza. Waziri Mkuu wa Rwanda, Makuza alizitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kusimamia amani na utulivu uliopo hivi sasa… “Bila amani na utulivu, hatuwezi kuzungumzia masuala ya uwekezaji. Tusimamie amani.” Mkutano huo unaotarajiwa kumalizika leo, umeandaliwa na Baraza la Biashara la Jumuiya ya nchi za Madola kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC). |
No comments:
Post a Comment