Makamba aacha zigo zito nyuma
.jpg)
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyejiuzulu, Yusuf Makamba
Lile agizo la Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyejiuzulu, Yusuf Makamba, la kuwachochea wanachama wake wote walioshindwa ubunge na udiwani kufungua kesi za kupinga matokeo, kwa kuwa ccmhama kingebeba gharama za kesi, imethibitika ilikuwa ni geresha na ulaghai mtupu.
Chama hicho kupitia kwa Makamba kilitoa maelekezo kwa makada hao kikiwataka kufungua kesi za kupinga matokeo hayo na kuwaahidi kwamba gharama zote za kesi zingelipwa na chama, lakini ahadi hiyo imeshindwa kutekelezwa.
Katika barua ya maelekezo ya Novemba 9, mwaka jana kwa makatibu wa CCM wa mikoa, Makamba aliwaelekeza maagizo hayo ikiwa ni pamoja na kuwapa kazi hiyo mawakili makada wa CCM.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba CCM/OND//636/VOL11/122 yenye kichwa cha habari: Wagombea ubunge/udiwani CCM kufungua malalamiko kupinga matokeo, Makamba alisema wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho walioshindwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010 wanatakiwa kufungua malalamiko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi (Madiwani) au Mahakama Kuu (Wabunge) ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya kutangaza matokeo (31/10/2010).
“Chama Cha Mapinduzi Makao Makuu kitachangia gharama za mawakili kwa wagombea ambao hawana uwezo wa kifedha,” alieleza Makamba katika barua hiyo na kuongeza:
“Kwa barua hii, mshirikishe Makatibu wa CCM wilaya/kata na wagombea husika kuandaa hoja za malalamiko na vielelezo/ushahidi na kuwasilisha CCM ofisi Ndogo Dar es Salaam au kuwasiliana na mawakili ambao ni makada wetu moja kwa moja ili kuandaa hati za malalamiko ndani ya muda huo.”
Hata hivyo, maelekezo hayo hayajatekelezwa hali ambayo imewaathiri wagombea kadhaa wa chama hicho ambao walifungua kesi za kupinga matokeo ya ubunge.
Aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini kupitia CCM, Justin Salakana, aliyefungua kesi ya kupinga ushindi wa Philemon Ndesamburo (Chadema), amesema kuwa ameelemewa na gharama za kuendesha kesi hiyo.
Aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa uwezekano wa kuendelea na kesi hiyo ni mdogo kutokana na ukata.
Salakana alisema kuwa kutokana na sheria kumtaka alipe Sh. milioni 10, kiasi hicho ni kikubwa na ni vigumu kukilipa.
“Nilifungua kesi namba mbili ya mwaka 2010, gharama za kuwalipa mawakili na ukizingatia kwamba patahitajika fedha zaidi hapo mbeleni (siku za usoni) kesi itakapoanza, kwa maana ya gharama za mashahidi na za mawakili hivyo uwezekano wa kuendelea na kesi ni mdogo,” alisema Salakana ingawa hakuwa tayari kuthibitisha kama ataifuta kesi hiyo leo.
Alisema kuwa wanachama wa CCM mjini Moshi na wapenzi wote waliowapigia kura wanafahamu juu ya kesi aliyoifungua baada ya matokeo kutangazwa na Ndesamburo kuibuka mshindi.
“Baada ya matokeo hayo tulikaa pamoja na uongozi wa CCM na baadhi ya wapiga kura wengine na kuyapitia matukio yote yaliyojitokeza na kuorodheshwa wakati kampeni zikiendelea na kulikuwa na kuridhika kuwa kulikuwepo na ukiukwaji wa sheria na kasoro nyingi ambazo zilifanya chama chetu kishindwe,” alisema.
Alisema uamuzi ulifikiwa kwamba wafungue kesi ya malalamiko. Hata hivyo, alisema pamoja na kufikia maamuzi hayo suala la gharama za kesi lilizungumzwa na kueleweka kwamba ni kubwa hasa kwa kuzingatia sheria mpya ambayo inamtaka mdai atoe Sh. milioni tano.
Alisema pia kuna gharama za mawakili na za mashahidi baada ya kesi kuanza.
Alisema baada ya kuwasilisha kesi wakili aliwaambia kuwa walitakiwa kulipa Sh. milioni tano ili kesi ianze. “Juhudi zilifanyika kuzipata hizo shilingi milioni tano na wiki iliyopita zilikamilika na akapewa wakili kuziwasilisha mahakamani,” alisema.
Mgombea mwingine wa CCM aliyelalamikia gharama za kupinga gharama za kupinga matokeo ni Hawa Ng’umbi, ambaye anapinga matokeo ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema).
Ng’umbi aliiomba Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kufuta gharama hizo au kuzipunguza ili kesi yake dhidi ya Mnyika ianze kusikilizwa.
Hata hivyo, mahakama ilikubali kumpunguzia gharama hizo hadi Sh. milioni tatu kwa kila aliyemlalamikia.
Nao wanachama watatu wa CCM katika Jimbo la Singida Mashariki waliojaribu kufungua kesi ya kupinga ushindi wa Tundu Lissu, walikwama na mahakama kutupa kesi yao baada ya kushindwa kutekeleza taratibu za kupunguziwa gharama.
No comments:
Post a Comment