Ufisadi: CCM�Dar hapatoshi



Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan
Hamkani si shwari tena ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, na sasa Halmashauri Kuu ya Mkoa huo imetakiwa kung'oka yenyewe kabla ya kung'olewa katika kipindi cha siku 10 kutokana na kugubikwa na kila aina ya uchafu.
Jemedari wa mapambano hayo mapya akiwa amepashwa moto na maamuzi ya NEC Taifa iliyowapa miezi mitatu mafisadi wote ndani ya chama hicho wang'oke ni Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, ambaye amesema halmashauri hiyo imechafuka kwa ufisadi uliopindukia.
Kutokana na hali hiyo, Azzan ameipa siku 10 kuitisha kikao kwa ajili ya kujadili tathmini ya mwenendo mzima wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka jana vinginevyo atawalipua kwa kuanika madudu yanayofanywa na watendaji wake.
Kadhalika, Azzan amedai kuwa anatishiwa maisha na watu wasiofahamika baada ya kuitaka sekretarieti ya mkoa huo ijivue gamba.
Mbunge huyo aliitaka sekretarieti ya mkoa kujivua gamba mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa vikao vya CCM vya Kamati Kuu (CC) na NEC na kuamua kujivua gamba ili kukirejesha haiba ya chama ambayo imechafuka mno kutokana na tuhuma za kukumbatia watu wenye tuhuma za ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Azzan alisema kuwa mpaka sasa Halmashauri ya mkoa haijafanya kikao chochote na hakuna matarajio ya kuitisha kikao licha ya katiba kuwataka kufanya hivyo.
Azzan alikwenda mbali zaidi kwa kuitaka sekretarieti hiyo ijiuzulu, vinginevyo aliahidi kuanika uozo unaofanywa na wajumbe hao baada ya siku 10.
Alisema viongozi wa mkoa wamekuwa na utendaji mbovu hali ambayo ilisababisha kuwepo na makundi ndani ya CCM tangu mwaka 2007 ulipofanyika uchaguzi wa ndani wa chama.
“Kuna makundi mawili yamegawanyika ndani ya chama hali ambayo ilisababisha kuchukuliwa kwa majimbo yetu kwani walikuwa wanafanya ufisadi mkubwa wa kuwaweka watu wao wagombee wakati hawakuwa chaguo la wananchi,” alisema.
Alisema kitendo hicho cha kujichagulia watu wao kimesababisha kwa asilimia kubwa kura nyingi kwenda upinzani kutokana na wanachama wa CCM kuwapigia kura wagombea wa upinzani baada ya kuwekewa wagombea ambao hawakubaliki.
“Kwa upande wangu walinifanyia uchakachuaji, lakini walishindwa tena sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam ilitaka nianguke katika Uchaguzi Mkuu ila nashukuru wananchi waliniokoa kwa kunipitisha kwa asilimia kubwa,” alisema Azzan.
Azzan alisema alinyimwa hata vifaa vya uchaguzi katika jimbo lake, hali ambayo ilimsikitisha na kwamba hata alipojaribu kuulizia suala hilo alikuwa akipatiwa taarifa za vitisho.
“Majimbo ya wenzangu kama la Kawe, Ubungo na mengineyo walipatiwa fulana 5,000 pamoja na kofia, lakini mimi hawakunipatia. Nikasikia kuwa zimepelekwa katika Jimbo la Kilwa wakati mgombea wa huko alishapatiwa...yapo mambo mengi na nitayaanika wasipofanya kikao hicho,” alisema.
Alisema sekretarieti ya mkoa inatakiwa kujivua gamba kwani wajumbe wake wamekuwa wakifanya ufisadi mkubwa wa kukiangamiza chama kutokana na kujali maslahi yao binafsi.
Azzan alisema amelazimika kusisitiza msimamo wake kwa kuwa amekuwa akipigiwa simu za vitisho pamoja na ujumbe mfupi (SMS) kutoka kwa watu asiowajua baada kauli yake ya hivi karibuni aliyoitoa mjini Dodoma na kuitaka CCM Mkoa wa Dar es Salaam nayo ijivue gamba.
“Mimi siogopi vitisho wanaogopa kuitisha hicho kikao kutokana na kwamba wanayajua waliyoyafanya katika Uchaguzi Mkuu, lakini wasipoitisha kikao mwezi ujao nitaanika hadharani mambo yote waliyoyafanya,” alisema.
CHILIGATI, NAPE WAENDELEZA MAKOMBORA
Wakati huo huo, viongozi wa sekretarieti mpya ya CCM taifa jana waliendelea na ziara yao kujitambulisha kwa wanachama katika mkoa wa Iringa.
Viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Chiligati, na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, waliendelea kuwarushia makombora viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Katika mkutano uliofanyika ofisi za CCM mkoa wa Iringa jana jioni, Nape alisema wanaotuhumiwa kwa ufisadi waache siasa watafute kazi nyingine za kufanya.
Alisema watu hao waliigeuza CCM kama kichaka cha kufanya biashara na mambo yao na kuongeza kuwa mtu mzima akikupa muda hunabudi kujipima mwenyewe.
Kwa upande wake, Chiligati alisema chama hicho kimeagiza kufanyika kwa tathmini katika ngazi zote ili wanachama wawataje watuhumiwa wanaopaswa kuvuliwa nafasi za uongozi kwa aibu kama hawatajiwajibisha ndani ya siku 90.
No comments:
Post a Comment