Mitalaa ya msingi na sekondari haiwezi kutoa wahitimu mahiri |
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia akizungumza katika uzinduzi wa ripoti kuhusu uhusiano wa ubora wa mitalaa na utoaji wa elimu bora uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Na Elizabeth Sulayman KATIKA dunia ya leo, ili binadamu aweze kuboresha maisha yake kwa ufanisi, lazima awe na elimu. Elimu ndiyo inayomwezesha kujitambua, kujimiliki yeye mwenyewe, kuzikabili changamoto zinanazomsonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wazazi, serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia kuhusu kushuka kwa ubora wa elimu nchini. nchini Tanzania. Kuna vigezo viwili vinavyotumika kupima kiwango cha ubora wa elimu. Kwanza,wasomi hutazama ufaulu wa wanafunzi katika stadi za msingi kama vile kuandika, kusoma na kuhesabu na pili, wasomi hutazama kiwango ambacho wanafunzi wameweza kupata stadi za msingi zitakazowawezesha kukabiliana na ulimwengu wa ajira. Lakini msingi mkuu wa utoaji elimu bora unajengwa na ubora wa mitalaa pamoja na ubora wa mbinu, mikakati na jitihada za kutekeleza mtalaa huo. Maana ya mtalaa na athari yake katika elimu Waandishi wengi wanakariri kuhusu ugumu uliopo katika kuelezea maana ya dhana ‘mtalaa’. Neno hili linatokana na lugha ya Kilatini, likimaanisha ‘kuendesha kozi’. Kwa kuzingatia maana ya asili ya neno lenyewe, mwandishi wa masuala kuhusu mitalaa Peter. F Oliva anaelezea maana ya neno hilo kwa kuzingatia mambo 12 yafuatayo: Kile kinachofundishwa shuleni, seti ya masomo, maarifa, programu ya masomo, seti ya vitu vya kujifunza, seti ya malengo ya ufanyaji kitu, kozi ya kujifunza na kila kitu kinachoendelea shuleni yakiwemo mambo yanayofanyika nje ya darasa, usimamizi na uhusiano kati ya mtu mmoja na mwingine. Mambo mengine ni kila kitu kinachopangwa na wafanyakazi shuleni, mjumuiko wa uzoefu mbalimbali anaoupata mwanafunzi awapo shuleni na kile ambacho mwanafunzi hukipata kikiwa ni matokeo ya kuwa shuleni. Ufanisi wa mitalaa ya elimu ya Tanzania Agosti 2010, asasi ya HakiElimu ilifanya utafiti kuhusu uhusiano kati ya ubora wa mitalaa na utoaji wa elimu bora uliofanyika katika wilaya sita nchini ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kutathmini ubora wa mtalaa wa elimu ya msingi na sekondari. Walimu na wanafunzi waliombwa kuonyesha ni kwa kiwango gani mtalaa wa elimu wa Tanzania unafaa katika kutoa wahitimu mahiri, wenye kujiamini, wanaowajibika na wenye ujuzi unaohitajika. Matokeo yanaonyesha idadi kubwa ya washiriki, walimu na wanafunzi walisema kwamba mtalaa wa elimu wa Tanzania hauna uwezo wa kutoa wahitimu mahiri katika nyanja mbalimbali. Kwa mfano, ni asilimia 35 tu ya walimu na asilimia 26 ya wanafunzi ndiyo walioripoti kwamba mtalaa unafaa katika kuandaa wahitimu mahiri na wenye kujiamini. Kibaya zaidi, ripoti inasema walimu kama wadau muhimu, hawahusishwi pale yanapotokea mabadiliko ya mitalaa. Hii imewafanya wawe nyuma katika utekelezaji wa mitalaa kwani wao ndio watekelezaji wakuu wa mitalaa. Mabadiliko mengi yanavuruga utoaji elimu. Walimu waliikosoa serikali kwa kuanzisha mtalaa ambao hauendani na mahitaji ya watu. Pia waliokosoa mwenendo wa serikali katika miaka ya hivi karibuni kufanya mabadiliko ya mtalaa bila ya kuwahusisha wadau ukijumuisha walimu na wanafunzi. Kwa mfano, Ofisa Elimu wa wilaya moja alisema: “Nadhani tumekuwa tukifanya mabadiliko ya mtalaa kiasi cha kuwachanganya walimu wetu. Kabla ya walimu hawajauzoea mtalaa mpya, mabadilikio yanafanyika.” Mfumo wa kitabu kimoja Katika utafiti huu, walimu walitoa mawazo yao kama wanapendelea matumizi ya vitabu vya aina moja vya kiada au vitabu vya aina nyingi. Kimsingi, walimu na wanafunzi wanataka mfumo wa kitabu kimoja uendelee. Matokeo ya utafiti yanaonyesha, asilimia 79.9 ya walimu wanapenda kutumia vitabu vya kiada vya aina moja katika shule zote huku asilimia 20.5 ikitaka vitabu vya aina mbalimbali. Ushiriki wa jamii katika mitalaa Wazazi wengi hawana uelewa kuhusu mitalaa ya elimu ya Tanzania. Wengi waliohojiwa walisema wanafahamu kidogo sana kuhusu mitalaa na sera za elimu za Tanzania. Hii imewapa ugumu kufuatilia mchakato wa kujifunza na kufundisha. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba wazazi na jamii kwa ujumla wanahusishwa kwa kiwango kidogo kwenye michakato ya utunzaji wa mtalaa, na hii imeathiri elimu nchini. Vitabu na makosa Utafiti umebaini baadhi ya vitabu haviendani na muhtasari rasmi wa wizara huku mada zikiwa zimeandikwa bila kufuata maelekezo ya mtalaa, hivyo kuwapotosha wanafunzi. Aidha, baadhi ya vitabu vina makosa makubwa ya kimaudhui kiasi cha kuwafanya wanafunzi washindwe kuunganisha kinachofundishwa na kile wanachotarajia kupata. Pia vitabu vina makosa mengi ya lugha. Mwanafunzi anashindwa kuelewa nini kinazungumziwa kwa manufaa yapi. Mapendekezo Pamoja na mambo mengine, ripoti inaishauri serikali kufuata maoni ya wazazi, walimu na wanafunzi waliopendekeza matumizi ya vitabu vya aina moja na kudhibiti ubora wa vitabu hivyo, ili kuhakikisha kuwa vile vinavyopendekezwa kutumika shuleni vinakuwa na ubora unaohitajika. Kuna haja kwa wasimamizi katika sekta ya elimu kutilia mkazo suala la upatikanaji wa nyenzo za kutosha za kufundishia na kujifunzia katika shule zetu. Hatua madhubuti zichukuliwe na wadau wa elimu kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto, ili wajifunze na wafanikiwe kitaaluma na kijamii. Walimu wafahamishwe kuhusu sera hizi pamoja na kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili kupanua uelewa wao. Pia kuna haja ya kuboresha mbinu za ufundishaji, ili zilenge kuwafanya wanafunzi wapate ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa na serikali kuboresha maslahi ya walimu pamoja na kuwapatia mafunzo, jambo ambalo ni muhimu katika upatikanaji wa elimu bora. Kwa kuwa Kamati ya Uidhinishaji wa Vifaa vya Elimu (EMAC), ndicho chombo kikuu katika kuhakikisha ubora wa vitabu shuleni unakwepo, kamati hiyo inapaswa ifanyiwe uboreshaji kwani vitabu vingi vya kiada vilivyopitishwa na kamati hiyo vina makosa yanayowapotosha walimu na wanafunzi. Makala haya ni rejea ya ufupisho wa ripoti ya ya utafiti kuhusu uhusiano kati ya ubora wa mitalaa na utoaji elimu iliyoandaliwa na Haki Elimu |
No comments:
Post a Comment