Thursday, 21 April 2011

Ubalozi Marekani wampa Kanyamala `Tuzo ya Mwanamke Jasiri`

 
Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt

Mwanzilishi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la Kivulini lililoko jijini Mwanza, Maimuna Kanyamala, amepata “Tuzo ya Mwanamke Jasiri” inayotolewa kila mwaka na Ubalozi wa Marekani nchini.
Kanyamala, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, alikabidhiwa tuzo hiyo jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, kwenye sherehe, iliyohudhuriwa na wageni kutoka makundi mbalimbali.
Mwaka jana mshindi wa tuzo hiyo, alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya.
Akizungumza kwenye sherehe hizo, Balozi Lenhardt, alisema ubalozi na wananchi wa Marekani, wametoa tuzo hiyo kwa Kanyamala, kama njia ya kutambua juhudi zake za muda mrefu za kupigania haki za wanawake.
Alisema Kanyamala alitilia mkazo maalum wa kuzihamasisha jamii kuzuia ukatili dhidi ya akinamama na wasichana katika eneo la Kanda ya Ziwa.
“Juhudi zake zimeleta changamoto kubwa kutoka kwa jamii. Kutokana na kampeni zilizofanywa na Shirika lake la Kivulini za kupinga ukatili, amejikuta katika lawama kali kutoka kwa wapinzani wake wa Kanda ya Ziwa wakimtuhumu kwa kuwafanya wanawake ‘wavimbe vichwa’,” alisema.
Alisema Serikali ya Marekani ipo pamoja na shujaa huyo kuhakikisha malengo yake ya kuwakomboa wanawake yanafikiwa.
Balozi huyo alisema serikali yake imetenga zaidi ya dola milioni saba mwaka huu kusaidia mipango inayolenga kuondoa ukatili dhidi ya wanawake.
Kwa upande wake, Kanyamala alisema tatizo la ukatili dhidi ya wanawake katika eneo la Kanda ya Ziwa, limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi za wakazi wake na Tanzania kwa jumla, ambazo hazithamini hadhi ya mwanamke.
“Ndiyo maana asilimia 48 ya wanawake wamekutana na ukatili dhidi yao katika kipindi chao cha maisha na asilimia 60 kati yao hawakuweza kuuripoti rasmi katika mamlaka zinazohusika, sababu ikiwa ni woga wa kunyang’anywa watoto, mali au kutokuwa na nyenzo za kuwawezesha kufika kwenye ofisi zinazohusika,” alisema.
Alisema asilimia 50 ya wanawake wanaona kufanyiwa vitendo vya ukatili ni kitu cha kawaida kisichohitaji kuchukua hatua zozote, hivyo, akaitaka jamii kuwathamini kinamama kwa kuwa ni dada zao, watoto wao na pia ni mama zao.

No comments:

Post a Comment