Nape aendeleza mashambulizi

.jpg)
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesisitiza kuwa Rais Jakaya Kikwete ni msafi na kwamba hahusiki katika kashfa yoyote ya kifisadi inayohusisha baadhi ya makada wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi usiku, Nape alisema kama kuna watu wanadai kwamba Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa ni mchafu, wajitokeze hadharani na kuonyesha uchafu wake.
“Rais wetu hayuko kwenye nyumba ya vioo hata kidogo na ndiyo maana amekuwa wa kwanza kurusha mawe kwa watuhumiwa wa ufisadi,” alisema akimaanisha kuwa kama Kikwete angekuwa ni fisadi asingekuwa wa kwanza kuwanyooshea kidole mafisadi na kuwataka waondoke kwenye nyadhifa zao ndani ya chama.
Nape aliwataja kwa majina baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusishwa na tuhuma za ufisadi na hivyo kuchafua taswira ya CCM kwa wanachama na wananchi.
“Jamani siyo kwamba tunaogopa kuwataja, hawa watu wametajwa kwenye vikao vya chama chetu ndiyo maana nawataja hata hapa, nimewataja huko nyuma na nitaendelea kuwataja,” alisema na kuongeza:
“Tumewaomba wapime wenyewe na baada ya hizo siku tisini wajiondoe kwenye nafasi za uongozi wote ndani ya chama vinginevyo tutawaondoa na ikiwezekana tutawanyang’anya kadi za uanachama kwa sababu watakuwa wamekaidi uamuzi halali wa kikao halali.”
Aidha, alisema operesheni vua gamba inayoendelea haiwahusu tu watuhumiwa hao bali wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki kwenye vitendo vya ufisadi ikiwemo kwenye miradi ya chama hicho kama shule za sekondari na majengo mbalimbali.
“Kwenye miradi yetu ya CCM nako kuna ufisadi kweli, tumefika sehemu tumekuta mwanachama mwenzetu wa CCM amesaini mkataba na wawekezaji wa kuwapangisha kwa muda wa zaidi ya miaka 200, unaweza ukaona mwenyewe kama ni upangishaji au ni uuzaji,” alisema.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati, aliwataka viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali ambao wanafahamu kuwa siyo wasafi kuanza kuondoka wenyewe kabla hawajaondolewa kwa kudhalilishwa.
Chiligati alisema hayo wakati akizungumza na wana-CCM pamoja na wananchi wa Manispaa ya Iringa kwenye viwanja vya ofisi za CCM Mkoa wa Iringa juzi jioni.
Chiligati na Nape wapo mkoani Iringa katika ziara yao ya kujitambulisha kwa wanachama kufuatia Sekretarieti ya CCM kuundwa upya baada ya kuvunjwa kukamilisha falsafa ya Mwenyekiti wake ya kujivua gamba.
JUKWAA LAO LAANGUKA
Wakati huo huo, Chiligati na Nape wamejikuta wakipigwa butwaa baada ya wao na viongozi wengine wa Chama hicho Mkoa wa Iringa kudondoka chini baada ya jukwaa walilokuwa wamekaa kuanguka.
Mkasa huo ulitokea katika Kata ya Mgama Iringa Vijijini majira ya saa 7:10 jana mchana wakati viongozi hao walipokwenda kukagua ujenzi wa chuo cha makada wa chama hicho katika eneo la Ihemi.
Haikueleweka mara moja kama jukwaa hilo lilikaguliwa na oganaizesheni ya Chama hicho kabla ya kukaliwa na viongozi hao.
Ujumbe wa viongozi hao ukiwa katika harakati za kutia saini kitabu cha wageni, jukwaa hilo liliachia sehemu ya chini na kuanguka jambo ambalo lilisababisha kizaazaa cha nani ajiokoe na nani aokolewe.
Baadhi ya viongozi waliokuwepo katika jukwaa hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Asery Masangi; Mbunge wa Kalenga, William Mgimwa na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Iringa, Abed Kiponza.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, wanachama wa CCM na watu wengine waliokuwepo walishuhudia viongozi hao wakiamka na kuhutubia bila kutumia jukwaa.
Inadaiwa kuwa ujenzi wa jukwa hilo uligharimu Sh. 800,000.
Katika tukio lingine, baada ya mkutano huo kumalizika na viongozi hao kuanza kuondoka, ghafla Diwani wa Kata ya Mgama, Denis Lupala, aliusimamisha msafara akilalamika kuwa yeye ni kiongozi wa wananchi na alitakiwa kupata nafasi ya kufikisha kero za wananchi wake katika mkutano huo, lakini hakupewa nafasi ya kufanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Chiligati alilazimika kwenye gari na kuzungumza naye faragha na baadaye kuondoka.
Lakini baadaye Diwani huyo alimshukia Chiligati akimweleza kwamba yeye ni miongoni mwa wanaotakiwa kuvuliwa gamba ili kukisafisha chama hicho huku akisisitiza kuwa hakuhusishwa na ugeni huo.
Hali hiyo ilimlazimisha Nape kuingilia kati kuhoji kuhusiana na madai ya diwani huyo.
Alijibiwa na Mwenyekiti wa Chama Wilaya ya Iringa, Kiponza, kuwa suala hilo litashughulikiwa ndani ya chama kwa kuwa taarifa zimeshafika ofisini.
Imeandikwa na Mawazo Malembeka, Godfrey Mushi na Vicky Macha, Iringa.
No comments:
Post a Comment