Thursday, 21 April 2011

Mvua yaleta balaa Dar

*Wananchi watembea usiku kucha
*Mwingine afa kwa kunaswa na umeme
*Magari kibao yafia kwenye foleni

Na Waandishi Wetu, jijini

WANANCHI wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam jana walikumbwa na adha ya pekee kutokana na mvua kunyesha siku nzima hali iliyosababisha wengi kutumia usafiri wa pikipiki huku wengine wakihama makazi yao kutokana na maji kufurika katika makazi yao.

Dar Leo lilishuhudia kero zaidi ya usafiri ambapo wananchi wengi walitumia nauli zaidi ya mara tatu tofauti na viwango halisi ili mradi waweze kufika majumbani mwao.

Adha hiyo iliwakumbusha wakazi wa Gongo la Mboto na Mbagala yale yaliyowatokea kipindi cha mabomu huku wengine wakisikika kujutia hali hiyo kuwa hawaelewi itaisha lini kwani wao kila siku ni kiguu na njia kutokana na kutembea mwendo mrefu tena kama ambavyo walifanya wakati wa mabomu.

Kutokana na hali hiyo wenye daladala wengi waliamua kuzipaki gari zao huku zile zilizokuwa barabarani zilikuwa zikitoza kiwango kikubwa kwa madai kuwa wanafidia ruti chache watakazofanya kutokana na foleni iliyopo katika barabara mbalimbali.

Baadhi ya wakazi wa Keko, Vingunguti, Mwananyamala na maeneo mengine walilazimika kuhamishia familia zao kwa ndugu na jamaa zao kutokana na nyumba zao kujaa maji.

Wakizungumza na Dar Leo kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi hao wameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuboresha miundombinu ya barabara ambayo ndiyo ilikuwa kikwazo kikubwa cha usafiri.

Wamesema barabara nyingi ni mbonu na hazina mifereji jambo ambalo limekuwa likisababisha maji kushindwa kupita kwa urahisi na kujaa barabarani.

Wametolea mfano barabara ya Vingunguti kwenda Tabata ambayo wamesema kuwa, mkandarasi ameshindwa kuikamilisha na kusababisha adha kwa wananchi kushindwa kupita huku magari mengi yakinasa barabara.

Adha hiyo haikuwakumba raia tu wa Tanzania bali hata wageni na viongozi mbalimbali wa nchi walionja joto ya jiwe ambao walikuwa wakitumia barabara ya Nyerere kwa ajili ya kwenda au kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.

Hali hiyo ilisababisha wageni kushuka na kutembea kwa miguu umbali mrefu huku wakiwakodi vijana wawabebee mizigo yao ili mradi tu wawahi safari zao za ndege.

Hatua hiyo ilitokana na foleni kubwa iliyosababisha magari kushindwa kutembea katika mataa ya Tazara na maeneo mengineyo.

Pia wananchi wamelalamikia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushindwa kufuatilia miundombinu yao ambapo baadhi ya wananchi walijikuta wakikumbwa na ajali ya kunaswa na umeme kutokana na nguzo za umeme kukatika katikati ya barabara.

No comments:

Post a Comment