Tuesday, 1 March 2011

Tuzo ya Martin Luther King yauenzi muafaka Zanzibar  
Mwandishi Wetu

KAMATI ya watu sita walioshughulikia muafaka wa kisiasa Zanzibar baina ya vyama vya CCM na CUF na baadaye kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo, imepata tuzo ya amani ya Dk Martin Luther King Drum.

Tuzo hiyo yenye lengo la kutambua mchango wa wanasiasa hao, ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Lenhardt, alisema tume hiyo imetolewa kutambua mchango wa watu hao katika kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliodumu kwa miaka mingi.

“Sisi tunaunga mkono hatua ya kamati hiyo ambayo ni ya ujasiri na inaonyesha kutia moyo kwa ahadi mpya ya Umoja wa Serikali," alisema Lenhardt.

Wajumbe wa kamati hiyo iliyoundwa Machi mwaka 2010 baada ya Baraza la Wawakilishi kuridhia hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni Ali Mzee Ali (CCM), Abubakar Khamis A.Mazrui (CUF), Jaji Omar Kheri (CCM), Zakiya Omar Juma (CUF) na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee Ibrahim.

"Walionyesha busara, maono, na uongozi kwa kusaidia kuweka muundo wa uchaguzi huru na wa haki na hatimaye Serikali iliyotokana na mapenzi ya Wazanzibari wote," ilisema taarifa ya balozi Lenhardt.

Mwafaka baina ya CCM na CUF ndiyo iliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein wa CCM huku akiwa na makamu wawili ambao ni Makamu wa Kwanza, Seif Shariff Hamad wa CUF, wakati Makamu wa Pili ni Balozi Seif Ali Iddi wa CCM.

Kadhalika, Dk Shein katika Serikali aliyoiunda aliwateua baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CUF kuwa mawaziri na naibu mawaziri.

Jana katika taarifa yake, Balozi Lenhardt alisema wao wanatambua kwamba hayo ni matokeo ya kazi nzuri ya kundi la kujitolea la wazalendo hao ambao waliamua kuweka kando itikadi zao za siasa za vyama na kufanya kazi ngumu ya kuleta maridhiano.

Taarifa hiyo pia ilisema "Kwa kuutambua mchango wa watu hao sita, tunaunga mkono hatua madhubuti za kuundwa kwa Serikali hiyo ya umoja wa Kitaifa, tukitambua kuwa hilo halikufikiwa kwa mahasimu wawili wa kisiasa visiwani humo, kuvutana mkono wa kumaliza tofauti zao bali ni jitihada za Wazanzibari wote."

Balozi Lenhardt alisema kuwa kitendo  kamati hiyo kinaionyesha ni namna gani siasa inavyoweza kutumika kuleta amani  nchini.

Kabla ya kufariki dunia kwa kuuawa kikatili mwaka 1968, Dk Martin Luther King alikuwa akitumia muda wake mwingi kuhakikisha jamii inaishi kwa amani, usawa na utulivu.

Na katika kutambua mchango huo Dk Martin Luther, Ubalozi wa Marekani nchini umekuwa ukitoa tuzo kwa wapigania haki, amani na usawa kila mwaka nchini.

Baadhi ya Watanzania ambao wamewahi kupata tuzo ya amani ya Dk Martin Luther King na miaka waliopata tuzo hizo kwenye mabano ni Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, (1999) na rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere (2000).

Wengine ni Jaji Mkuu Mstaafu, Marehemu Francis Nyalali (2002), Profesa Geoffrey Mmari – (2003), Mama Justa Mwaituka (2004), Balozi Gertrude Mongella (2005), Dk Salim A. Salim (2006), Hayati Rashid Kawawa (2007) na Reginald Mengi (2008).

Pia wamo watu wa jamii ya Albino (2009) na Dk Marina Alois Njelekela ambayeni, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), 2010.

No comments:

Post a Comment