Tuesday, 1 March 2011

Kikwete alia na CHADEMA


*Ahofia maandamano yao na mikutano inayoendelea mikoani
*Asema yanachochea ghasia kuiondoa serikali madarakani


Na Edmund Mihale

RAIS Jakaya Kikwete jana kwa mara ya kwanza amezungumzia maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayoendelea
katika mikoa mbalimbali nchini kupinga gharama za maisha akiyaelezea kuwa yenye dhamira ya kutaka kuleta machafuko na uvunjifu wa amani nchini.

Akilihutubia Taifa katika hotuba yake kila mwezi, Ikulu jana, Rais Kikwete alisema kufanya maandamano na mikutano ni haki ya msingi ya vyama vya siasa na raia. Lakini, kuigeuza fursa hiyo kuwa ni jukwaa la kuchochea ghasia na kwa nia ya kuiondoa serikali iliyoko madarakani kwa mabavu ni matumizi mabaya ya fursa hiyo.

"Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila miaka mitano tunafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wetu. Uchaguzi wa mwisho tumefanya Oktoba 31, 2010. Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni zilizochukua karibu miezi mwili na nusu. Kila chama kilielezea jinsi kitakavyokabiliana na matatizo yanayowakabili wananchi wa nchi yetu ikiwa ni pamoja na haya wanayoyazungumza sasa.

"Hatimaye siku ya uchaguzi wananchi walifanya uamuzi wa kuchagua chama walichokiamini, nacho ni Chama Cha Mapinduzi (CCM). Iweje leo, miezi mitatu baadaye kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yale yale waliyoyasema kwenye kampeni.

"Siyo sawa hata kidogo, kuchochea ghasia ati kwa nia ya kuiondoa serikali madarakani ni kinyume cha katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima.

"Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi," alisema Rais Kikwete.

Alisema katika nchi ya kidemokrasia na kwa wanademokrasia wa kweli, wanapomaliza uchaguzi mmoja, wanajiandaa kwa mwingine. Wanajenga upya chama chao, wanaongeza wanachama, wanaboresha sera na hoja zao pamoja na namna ya kuziwasilisha ili watu wawakubali wao na kuwakataa wenzao.

Alisema uwanja muhimu wa kufanya hivyo ni sehemu ya bunge na halmashauri za wilaya kupitia wabunge na madiwani

Alisema kitendo kinachofanywa na Chadema cha kuzunguka nchi nzima na kuchochea ghasia kwa lengo la kuwaondoa walioshinda ili waingie  ni kinyume na misingi ya demokrasia.

"Tutajenga misingi ya hovyo na nchi yetu itakosa amani na utulivu daima. Hebu fikirieni, kama kila atakayeshindwa uchaguzi anafanya hivyo tutakuwa nchi ya namna gani?

"Tanzania yetu hii yenye sifa na heshima ya kuwa nchi ya amani na utulivu itapoteza kabisa sifa hiyo na badala yake umwagaji wa damu na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia vitageuka kuwa maisha ya kawaida. Hatuitendei haki nchi yetu na hatuwatendei haki wananchi tunaodai tunawapenda na kuwatetea.

"Ndugu zetu wa CHADEMA wanayajua yote haya, lakini wanalo lao jambo. Wanataka kuipeleka nchi yetu pabaya kwa kukidhi uchu wao wa madaraka. Kwao sasa demokrasia haina maana, inaweza kusubiri. Wanataka kutumia mabavu. Naomba tuyakatae mambo yao. Tusiwafuate. Waambieni mchezo wao ni hatari na ni mauti yetu. Sisi katika serikali tutajitahidi kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa nchi yetu, watu wake na mali zao," alisema Rais Kikwete.

Akizungmuzia hali ya maisha ya Mtanzania, Rais Kikwete amekiri kuwa kwa sasa hali ni ngumu ya kimaisha, hivyo amewataka kukabiliana nayo.

Alisema kuwa serikali kwa upande wake imeelekeza nguvu na rasilimali zote na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali. hivyo kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, bali kikwazo kikubwa ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi nchini na hivyo uwezo siyo mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo Watanzania wengi wanapenda iwe.

"Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa. Mzee Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii. Wa wale wa umri wangu au kunizidi wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri.

"Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa naye kakaa miaka 10 hakuyamaliza. Mie nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote. Lililo muhimu kuliko yote ni kuwa katika kila awamu nchi yetu imekuwa inapiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo.

"Hali iliyokuwa wakati ule sivyo ilivyokuwa mwaka 1985, wala 1995 au 2005 na ilivyo sasa. Katika miaka mitano hii kuna maendeleo yanayoonekana wazi, pamoja na changamoto nyingi tumefanya juhudi kubwa na mafanikio yanaonekana katika nyanja zote za maisha ya Watanzania. Mwenye macho haambiwi tazama.

"Lakini, pia ni muhimu watu kutambua ukweli kwamba uchumi kama wetu ambao haujajenga uwezo wake wa ndani wa kujitosheleza kwa mahitaji yake, huathirika sana na yale yanayotokea katika uchumi wa dunia. Unapoyumba na sisi tunayumba," alisema Rais Kikwete.

Alisema kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia zinasababisha gharama za uchukuzi na uzalishaji huongezeka na kusababisha bei za bidhaa kupanda hivyo mfumuko wa bei ukipanda China, nguo na bidhaa zinazonunuliwa kutoka China hupanda navyo hupanda bei.

Hivi sasa mataifa yote makubwa mfumuko wa bei umepanda na kuathiri uchumi wa nchi, kukosekana kwa mvua nako kunasababisha uhaba wa chakula, bei za vyakula hupanda na watu wengine hukosa chakula. Hivyo hivyo lawama kwa serikali au Rais Kikwete inaanzia wapi? aliahoji.

Alisema hata hivyo serikali imekuwa ikitafuta ufumbuzi wa  matatizo yote kwa lengo la kutafuta unafuu kwa kiwango tunachowezekana ikiwemo kutoa unafuu wa kodi kama ilivyofanya kwa sukari na saruji pale. inapobidi.

Jana gazeti la serikali la Daily News lilimkariri Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa akisema kauli  zinazotolewa kwenye maandamano hayo za kumpa muda wa siku tisa Rais Kikwete kutekeleza mahitaji yao ni za kichochezi na zinaweza kuingizwa katika makosa ya uhaini kwa kuwa kinawachichea wananchi waichukie serikali yao.

Hali ya umeme

Akizungumuzia hali ya umeme nchini alisema hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni mbaya kutokana na kupungua kwa maji katika bwawa la Mtera ambayo juzi kina cha bwawa hilo kilishuka hadi kufikia mita 691.25 ambacho ni pungufu kwa mita 7 na kubaki mita 1.25 juu ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme.

Alisema  Februari 15 , 2011, Baraza la Mawaziri lilijadili na kuidhinisha mpango wa dharura wa TANESCO wa kukodi mitambo ya kuzalisha MW 260 za umeme. hivyo baraza hilo liliitaka Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa mchakato huo unakamilika mapema iwezekanavyo ili kupunguza makali na athari za ukosefu mkubwa wa umeme kwa jamii na uchumi wa nchi.

Alisema baraza hilo pia lilisisitizwa kuwa pamoja na udharura uliokuwepo sheria na taratibu za manunuzi ya umma vizingatiwe. Pia, wahakikishe kuwa mkataba watakaoingia uwe ni wenye maslahi kwa taifa na watoa huduma wawe ni kampuni zinazofahamika na zenye sifa stahiki na kuaminika.

"Natambua kuwa Bodi na Mejemienti ya Shirika la Umeme, wanaendelea na mchakato wa kupata umeme huo wa dharura kati ya sasa na Julai, 2011," alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa mwaka 2006/7 serikali iliamua kupunguza kutegemea umeme wa nguvu ya maji kwa kuongeza matumizi ya vyanzo vingine vya nishati.

Alisema mpango umetengenezwa na utekelezaji wake unaendelea na tayari umeme wa MW 145 wa kutokana na gesi asilia umeongezwa kwa kugharamiwa na serikali. na mwisho wa mwaka huu MW 160 zitaongezeka MW 100 Dar es Salaam na MW 60 Mwanza kwa gharama za serikali.

"Bahati mbaya kutokana na matatizo ya fedha ya kimataifa, wawekezaji wa sekta binafsi wa kuzalisha MW 300 za umeme wa gesi asilia pale Mtwara walijiondoa. Umeme huo ungekuwa tayari umeshaingizwa katika gridi ya taifa hivi sasa na kuondoa tatizo la sasa. Wawekezaji wengine wamepatikana na mazungumzo yanaendelea vizuri," alisema Rais Kikwete.

Alisema Mradi wa Kiwira umecheleweshwa na mchakato wa kubadili milki na kupata mkopo wa dola za Marekani milioni 400 za kuwezesha ujenzi wa kituo cha kuzalisha MW 200. Lakini suala la kubadili milki limefikia ukingoni na mchakato wa kupata mkopo unaendelea kwa matumaini.

Hali ya chakula nchini


Rais Kikwete tayari Halmashauri 36 za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Dodoma, Lindi, Mtwara na Iringa imeripotiwa kuwa na upungufu mkubwa.

Alisema serikali imeidhinisha kutolewa kwa tani 13,760 za chakula kutoka Akiba ya Taifa ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kuhudumia watu 423,530 walioathiriwa na upungufu wa chakula katika maeneo hayo.

Alisema kazi ya usambazaji inaendelea. Hadi sasa jumla ya tani 4,822 za chakula cha msaada zimetolewa katika mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Lindi.

Fidia ya Gongolamboto


Alisema serikali imebeba jukumu la kujenga upya nyumba za wakazi wa eneo hilo kwa mujibu wa kiwango cha uharibifu.

"Nimeagiza Jeshi la Kujenga Taifa lifanye kazi hiyo kupitia Shirika lake la Uchumi. Nimeamua hivyo ili kuhakikisha kuwa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na maafa haya yanarejea kuwa ya kawaida mapema iwezekanavyo," alisema Rais Kikwete.

Alisema ameagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kitengo cha Taifa cha Maafa kuhakikisha kuwa utekelezaji unaanza mapema iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment