Tuesday, 1 March 2011

Matapeli waibuka na mbinu mpya Dar

na Betty Kangonga
UTAPELI wa kutumia simu za mikononi umeibuka jijini Dar es Salaam ambapo matapeli huwapigia watu simu huku wakidai wanatoa mikopo na kutafuta wafanyakazi wa kuwaajiri kwenye maduka ya luku.
Matapeli hao hujitambulisha kwa kujifanya watu karibu na baadhi ya watu wenye uhusiano wa karibu na wanayetaka kumtapeli na hivyo kufanikisha uhalifu wao huo bila kutiliwa shaka.
Mbinu hiyo wamekuwa wakiifanikisha kwa kuwaambia wahusika kuwa kuna kazi za kuuza luku zinazohitaji vijana hasa wasichana ambao wamemaliza kidato cha nne wenye uwezo wa kutumia kompyuta.
Matapeli hao pia hutaja kiasi cha mshahara kuwa ni sh 180,000 kwa mwezi, sh 3,000 ya chakula (kila siku), sh 20,000 kwa ajili ya makato ya mifuko ya hifadhi ya jamii na sh 20,000 kwa ajili ya bonasi ya utendaji kazi mzuri.
Aidha tapeli huyo ambaye hujiita Jamal au Hamisi mwenye asili ya Kiasia hupenda kutumia namba za simu tofauti ambazo ni 0753 472119, na 0659 674843 na kujifanya mkarimu pindi anapoongea.
Baadhi ya watu waliokwishatapeliwa walisema kuwa walipokutana na tapeli huyo anakuwa kamili na aina za fomu za ajira hiyo na kuwasainisha huku akimtafuta mwanasheria wa kusaini katika fomu zikishajazwa.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, mmoja aliyewahi kukumbwa na utapeli huo kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema tapeli huyo hupenda kukutana na watu katika vituo vya mafuta vyenye mashine za luku zikiwemo za Victoria, Ilala na Mwenge.
“Yaani ndani ya nusu saa unaweza kujikuta unapoteza simu, fedha pamoja na nakala za fomu zako, tena anataja fedha kulingana na wewe ulivyo; wapo ambao wametajiwa na kutoa sh laki moja na wengine 40,000 pamoja na simu za mkononi,” alisema.
Alisema mwingine hujiita Maganga na kujifanya anafanya kazi ya uanasheria katika mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii akidai anajishughulisha na kutoa mikopo.

No comments:

Post a Comment