Wednesday, 2 February 2011

Serikali Yadizi Kusisitiza Chanjo


Na Salma Said Zbar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kuanzia sasa wasafiri wote wanaoingia Zanzibar watalaazimika kuwa na cheti kinachoonyesha wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano ambayo imeenea katika baadhi ya nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini.
Nabu Waziri wa Afya wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya aliwaambia waandishi wa habari katika jana ofisini kwake jana Mnazi Mmoja Mjini Unguja kwamba serikali imeamua kutoa agizo hilo kufuatia tishio la ugonjwa huo hatari kutokea katika baadhi ya nchi.
Alisema baadhi ya nchi za kiafrika ikiwemo Uganda na nchi za kusini mwa Amerika ndio kuna ugonjwa huo wa homa ya manjano ambapo yatari nchi ya Uganda jumla ya watu hamsini (50) wameshapoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Naibu huyo alisema kutokana na hali hiyo wageni wote watakaoingia Zanzibar wanaotoka katika nchi hizo watalazimika waoneshe chanjo dhidi ya ugonjwa huo na wasipoonesha watachanjwa kwa nguvu sambamba na kupigwa faini ya kulipa dola za kimarekani 40 kwa kila mmoja.
Dk Mwamboya alisema watu wanaotoka Tanzania Bara hawahusiki na udhibiti huo na kusisitiza kwamba dhana hiyo isipotoshwe kwani wizara ya afya na Tanzania Bara na Zanzibar yatari zimeshakubaliana kukutana leo kwa ajili ya kukaa pamoja na kuweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo kwa pamoja.
Vifo vilivyotokea huko Uganda ndio vilivyoishitua serikali na kuchukua hatua na uamuzi huo ambapo hatua ya kujikinga na tishio la kukumbwa na aina fulani ya ugonjwa wa homa ya manjano uliolipuka nchini Uganda.
Hivi karibuni Dk. Mwamboya alitoa taarifa kuwahamasisha wananchi mwishoni mwa kikao cha nane cha Baraza la Wawakilishi kilichomalizika hivi karibuni huko Mbweni nje kidogo kutoka mjini wa Unguja na kuwataka wawakilishi kutoa elimu juu ya suala hilo kwa kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao.
Akitoa taarifa hiyo, Dk. Sira alisema kwa watu wanaokusudia kusafiri kwenda nje ya Zanzibar pia wanashauriwa kupata chanjo kabla ya kusafiri.
Alisema taarifa juu ya wasafiri kutakiwa kuwa na cheti cha chanjo dhidi ya ugonjwa huo, imeshasambazwa katika balozi zote za Tanzania na taasisi mbali mbali na kwamba wanaotakiwa kuonyesha vyeti hivyo ni pamoja na watalii wanaoingia nchini.
Dk. Sira alifafanua kuwa aina ya ugonjwa huo tayari umeua watu 50 kati ya watu wote 256 walioambukizwa nchini Uganda hivyo wananchi wanapaswa kuzingatia agizo hilo kwani ugonjwa huo ni hatari na unaambikiza kwa haraka.
Hata hivyo Dk Mwamboya hakueleza ulizuka lini nchini Uganda, lakini alisema ugonjwa huo unaenezwa na mbu na kwamba mpaka sasa tiba ya kupambana na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo haijapatikana.
Alishauri watu wanaposikia dalili ya mafua, uchovu, homa za vipindi na macho kuwa na rangi ya njano, waenda hospitali kuangalia afya zao pamoja na kupima kwani athari hizo zikijulikana mapema ni vizuri kwa kupata tiba yake.
Alisema ingawa taarifa hazionyeshi kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo, wananchi wanatakiwa kuzingatia masharti ya usafi wa mazingira ili kuzuia uchafu kuibua mazalio ya mbu.
Naibu Waziri huyo alisema katika hatua za mwanzo za kukabiliana na tishio la ugonjwa huo tayari wameshafungua vituo katika maeneo ya bandarini Malindi na Uwanja wa Ndege Zanzibar na kuwataka taasisi zinazohusika na kuleta wageni kuwaelimisha wageni na kuchukua hatua wageni wanaoingia nchini.

No comments:

Post a Comment