Nchimbi, Chami wanusurika ajalini |
Habel Chidawali,Dodoma MAWAZIRI Dk Emmanuel Nchimbi wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Dk Cyrill Chami wa Viwanda Biashara na Masoko wamenusurika katika ajali za gari tofauti zilizosababisha magari yao kuharibika vibaya. Nchimbi alipata ajali maeneo ya Kibaigwa, Dodoma wakati akienda kuwahi kikao cha Baraza la Mawaziri ambapo gari yake iligongana na basi la Happy Nation na kuharibika vibaya. Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema mara baada ya ajali hiyo, Nchimbi na dereva walikuwa salama, lakini gari haikuweza kutembea hivyo waziri huyo kulazimika kuomba msaada wa gari ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Charles Kitwanga kuweza kufika Dodoma. Katika ajali ya kwanza, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alisema waziri Chami alipata ajali ya gari juzi katika eneo la kati ya Kibaha na Chalinze mkoani Pwani. Katika ajali hiyo, Waziri Mkuu alisema waziri Chami ambaye hata hivyo, waziri huyo pamoja na msafara wake walitoka salama ingawa gari yao iliharibika upande aliokuwapo Chami. Alisema kuwa asubuhi ya jana aliwasiliana naye na kwamba hali yake ni njema na aliwasili mjini Dodoma salama. Pinda alisema kuwa walikuwa katika mwendo wa kawaida yeye pamoja na msafara wake na mara walipofika katika eneo la tukio magari mawili yalikuwa yakipishana likiwemo lori pamoja na basi. Alisema kuwa katika eneo hilo kuna mlima ambapo gari la nyuma lilijitahidi kufunga breki ili lisigonge kwa nyuma gari la Chami, lakini inavyoonyesha breki za gari hilo zilishindwa kufanya kazi. Kuhusu ajali ya pili ilielezwa kuwa waziri Nchimbi huyo alipata ajali maeneo ya Kibaigwa mkoani Dodoma katika barabara ya Morogoro- Dodoma kwa gari aliyokuwa akisafiria kugongana na basi. Basi hilo lilikuwa likielekea Dar es Salaam. Akizungumza na Mwananchi Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kongwa, OCD Mdimi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, lakini akasema kuwa hali yake inaendelea vizuri na tayari ameshawasili mkoani Dodoma ambapo kwa sasa anapumzika. Aliongeza kwamba ajali hiyo ilikuwa ni ya kawaida japokuwa gari la waziri lilikwaruzana na basi la Happy Nation. Taarifa za tukio zinaonekana gari iliumia vibaya upande wa waziri. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen alisema kuwa hana taarifa zozote zinazohusiana na ajali hiyo. “Kimsingi leo niko nyumbani nimepumzika si unajua mambo mengi, hata hivyo, kupumzika kwangu sio kwamba nsijue nini kinachoendelea bali taarifa za ajali ya waziri sijazipata labda nifuatilie nitawajulisheni,” alisema Zelothe. |
No comments:
Post a Comment