Tuesday, 8 February 2011

Msafara wa Dk. Kawambwa wapigwa mawe Chuo Kikuu


  Mabomu ya machozi yafurumushwa
  Uporaji bidhaa madukani wakithiri
  Mhadhiri apigwa mawe, ajeruhiwa


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu madai yao mbalimbali likiwemo la nyongeza ya posho ya chakula ambapo wanafunzi hao wanataka iongezwe kutoka Sh. 5,000 hadi Sh. 10,000.

Hali ya amani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kampsi ya Mlimani ni tete, huku zikiripotiwa vurugu za uporaji wa bidhaa madukani kwa kisingizio cha bei kubwa ya chakula na kupiga mawe masafara wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Matukio haya yanatokea siku tatu tu tangu wanafunzi hao wapambane na FFU wakitaka kwenda Ikulu.
Tukio la kuvunja maduka yanayouza mikate, kesi, soda na maji, lilitokea juzi usiku kuanzia saa tatu usiku na lilidumu kwa takribani saa mbili.
Wanafunzi hao wakiimba nyimbo za kuhamasishana walivamia maduka hayo yaliyoko kwenye mabweni namba mbili na tano, na kufanya uporaji huo kwa kile walichosema kuwa na njaa na kwamba bei ya chakula ilikuwa juu kiasi ambacho hawawezi kumudu.
Waliwatuhumu watoa huduma ya chakula chuoni hapo kuwa wamepandisha bei ghafla.
Jana dalili za kutokea rabsha zilianza kuonekana mapema wakati Waziri Kawambwa anawasili, na hali ya usalama iliongezeka kwa kumwagwa polisi wengi, wakiwamo waliomzunguka waziri huyo.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Kawambwa alijikuta katika wakati mgumu chuoni hapo wakati akizungumza na wanafunzi hao, kwani alijikuta akizomewa kila baada ya sentensi moja aliyokuwa akiitoa kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya wazi vya michezo vya chuo hicho.
Waziri Kawambwa alifika chuoni hapo chini ya ulinzi mkali wa Polisi kwa lengo la kuwapoza wanafunzi hao na kuwaeleza mchakato unaofanywa na serikali kutatua matatizo yao, lakini badala yake alijikuta siku yake ikiisha vibaya.
Akiwa chuoni hapo, Waziri Kawambwa alijikuta akikatisha maelezo yake kila wakati kutokana na kuzomewa.
Dk. Kawambwa ambaye alitakiwa kufika chuoni hapo saa 4:00 asubuhi kama alivyoahidi mwishoni mwa wiki iliyopita, aliwasili saa 6:59 mchana baada ya kutokea mtafaruku wa wapi kufanyike mkutano huo.
Awali, mkutano huo ulipangwa kufanyika kwenye ukumbi Nkurumah, lakini wanafunzi waliuzingira ukumbi huo na kuwazuia viongozi wa chuo hicho kuingia.
Hali hiyo ililazimu mkutano huo ukafanyikie kwenye uwanja wa michezo chuoni hapo ili wanafunzi wengi wapate nafasi ya kumsikiliza Waziri Kawambwa na kutoa dukuduku lao.
Wanafunzi hao walisikika wakisema: "Kufanyika mkutano ndani ya ukumbi huo ni kuwahujumu wanafunzi ambao wangependa kusikia kauli ya waziri."
"Hatutaki mashushushu, tunataka kila mwanafunzi asikie kauli ya Waziri, hatutaki kuchakachuliwa, tunataka mkutano ufanyike hadharani uwanjani na sio kwenye ukumbi ambao wanaingia theluthi ya wanafunzi," hayo ni baadhi ya maneno yaliyosikika yakisemwa na wanafunzi hao.
Baada ya mvutano baina ya uongozi wa chuo na serikali ya wanafunzi kudumu takriban saa tatu, msimamo wa wanafunzi uliheshimiwa na mkutano ukahamishiwa kwenye uwanja wa michezo uliopo ndani ya chuo hicho.
Akiwasili kwenye uwanja huo huku amezingirwa na ulinzi wa polisi wa kawaida na wa Kutuliza Ghasia (FFU), Dk. Kawambwa alipokewa kwa nyimbo kadhaa kutoka kwa wanafunzi ukiwemo ule unaosema: "Kama siyo juhudi zako Nyerere, Kawambwa angesoma wapi, hatutaki siasa za majukwaani."
Awali Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, aliwataka wanafunzi kutulia ili kupata fursa ya kumweleza waziri huyo matatizo yao.
Dk. Kawambwa alipochukua kipaza sauti ili kuwasalimia wanafunzi, alizomewa na wanafunzi hao huku wakimwambia : "Njaa inatuuma, siasa hatutaki."
Baada ya Waziri kuwatuliza aliwataka wanafunzi wamweleze matatizo yao, hali iliyosababisha kuibuka upya kelele za kuzomea na baadhi yao kumhoji alifika hapo kufanya nini.
Kero zilizowasilishwa kwa Waziri Kawambwa na wanafunzi hao ni kutaka ongezeko la posho ya kujikumu kutoka Sh. 5,000 hadi Sh. 10,000, wanafunzi 42 waliokamatwa baada ya vurugu za Ijumaa iliyopita wafutiwe kesi zao na kuiomba serikali iwapatie Sh. 100,000 kwa ajili ya kujikimu.
Waziri Kawambwa alisema ameyapokea malalamiko yao kwa hisia na atayafanyia kazi.
Kuhusu ombi la wanafunzi waliokamatwa na kuachiwa kwa dhamana wafutiwe kesi hiyo, Dk. Kawambwa alisema jambo hilo lipo nje ya uwezo wake kwa sababu ni la mhimili mwingine wa dola ambao ni mahakama.
"Nilichokifanya awali ni kuiagiza mamlaka ya polisi kuwaachia kwa dhamana wanafunzi wenzenu, lakini ombi lenu la kutaka kesi yao ifutwe, hili liko nje ya uwezo wangu, lakini nitajaribu kukaa na kuongea na wenzangu wa mhimili wa mahakama," alisema na kuhojiwa na umati huo: "Mbona mafisadi wako huru?"
Akielezea kuhusu ombi la fedha Sh. 100,000, Waziri Kawambwa alisema endapo serikali itaamua kulitekeleza litahusisha vyuo vyote nchini.
"Mmenituma mimi au serikali itoe Sh. 100,000, lakini hapa naongea na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vipi vyuo vingine, natakiwa kujumlisha kiwango hicho mara wanafunzi 94,430 nchini, je, fedha hizo nitazipata wapi leo hii," alisema na kupokelewa na maneno ya wanafunzi yakisema: "Mashangingi yauzwe."
Kuhusu ombi la wanafunzi la kutaka kuongezewa Sh. 5,000 ya chakula na malazi, Waziri Kawambwa alisema serikali itaongeza posho hiyo, lakini Hazina lazima ifanye mahesabu.
Posho hiyo ambayo alikataa kutaja kiwango chake, Waziri Kawambwa alisema itaongezwa kupitia bajeti ya mwaka ujao wa fedha (2011/2012).
"Niseme hivi, bajeti hii itatokana na jinsi mahesabu ya Hazina yatakavyofanyika, lakini malalamiko haya hamjayawasilisha kwangu kimaandishi," alisema na kupokelewa na wimbo unaosema: "Dowans imetengewa bajeti, ongezeko la mishahara ya wafanyakazi lililofanywa na Rais Jakaya Kikwete katikati ya kampeni yake lilitengewa bajeti."
Wakati akitetea hoja hizo za wanafunzi huku akilinganisha kipindi alichosoma chuoni hapo, Dk. Kawambwa alijikuta kwenye wakati mgumu zaidi baada ya wanafunzi kumweleza kuwa, enzi hizo alisoma bure na alichokiongea ni siasa.
Wakati wote wa mkutano huo, FFU na askari wa kawaida walikuwa wamejipanga kiulinzi kukabiliana na chochote kitakachotokea.
Lakini wakati Waziri Kawambwa akiondoka eneo hilo, wanafunzi waliupiga mawe na chupa za maji msafara wake kitu ambacho kiliamsha hasira za askari na kuanza kufyatua mabomu ya machozi.
Kitendo hicho kilichochukua takriban dakika 10, kilisababisha baadhi ya wanafunzi kuzirai na wengine kujeruhiwa wakati wakikimbia kujihami.
Akizungumza na gazeti hili jana jioni, Spika mstaafu, Mwangomango, alisema bado hawajafikia mwafaka kama kesho (leo) wataingia darasani au la.
"Wapo wanaotaka iundwe kamati ambayo itaenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kupeleka madai yao na wengine wanataka waingie madarasani, tumekubaliana tupate mawazo ya wadau wengine kama viongozi wa dini, siasa hivyo tutakutana nao leo usiku (jana)," alisema.
Wakati NIPASHE inaondoka eneo hilo la chuo, baadhi ya wanafunzi walisikika wakisema msimamo wa kutoingia madarasani uko pale pale hadi kieleweke.
Sakata la wanafunzi hao kula chakula na kuchukua baadhi ya vitu lilitokea juzi usiku chuoni hapo kwenye eneo la maduka maarufu kama Kariakoo muda mfupi baada ya kutoka kuangalia mpira.
Vile vile, Mhadhiri Msaidizi wa chuo hicho, ambaye jina lake halijapatikana, naye alipigwa mawe na kujeruhiwa na wanafunzi waliokuwa Hosteli za Mabibo, muda mfupi baada ya kuingia na gari huku taa zake zikiwa na mwanga mkali.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge mstaafu wa chuo hicho, Goodluck Mwangomango, wanafunzi walifikia hatua hiyo kwa madai kuwa walidhani wamevamiwa na polisi.
Mwangomango ambaye alijivua uspika siku mbili baada ya uongozi wa chuo kukataa kutekeleza madai yao, alisema baada ya mhadhiri huyo kuingia huku akiwa hajitambui kutokana na kulewa, alijikuta akipigwa mawe na kujeruhiwa.

Alisema jana asubuhi baadhi ya wanafunzi waliuvamia mgahawa (Cafeteria One) uliopo chuoni hapo na kuchukua vyakula vyote walivyovikuta.
Alisema baada ya Waziri Kawambwa kuondoka chuoni hapo, wanafunzi walifanya kitendo hicho katika mgahawa huo na wa jirani kisha kupiga mawe na kuharibu baadhi ya mali.
Alisema vitendo hivyo vimefanywa na wanafunzi wa jinsia zote kwa maelezo kuwa hawana fedha za kununua chakula.
Baadhi ya wanafunzi ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini walisema hayo yote yanatokea kwa sababu ya serikali kutokubali kuwaongezea fedha za kujikimu.
Walisema baada ya kufika kwenye migahawa hiyo walikuta baadhi ya vitu vimepandishwa bei huku wao wakiwa hawana fedha.
"Hali hii ilitufanya wanafunzi kushikwa na hasira na kuvunja baadhi ya vitu vilivyopo humo pamoja na kula chakula kwa sababu tulikuwa na njaa," alisema mmoja wa wanafunzi hao.
NIPASHE ilishuhudia migahawa iliyovamiwa na wanafunzi hao ikiwa imefungwa na baadhi ya vitu vikiwa vimeharibiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo, lakini hakubainisha thamani ya mali zilizoharibiwa na wanafunzi hao.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment