Monday, 7 February 2011

Wizi kimafia wazidikutikisa mabenki TZ

Ramadhan Semtawa
 
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Profesa Ndulu.



MTANDAO wa uhalifu wa kutumia mawasiliano ya intaneti (Cyber Crime), umezidi kutikisa mabeki nchini baada ya kubainika mpango mkakati wa kuhamisha fedha kidogo kidogo kwa njia ya manunuzi kutoka kwenye akaunti ya mfanyabiashara maarufu nchini.

Tukio hilo jipya limebainika baada ya duru za kiuchunguzi kuonyesha limeratibiwa na mtandao huo kuanzia ndani ya mabenki, maduka ya kuuza bidhaa na makao makuu ya mabenki ambako hutoa idhini ya kuhamisha fedha moja kwa moja kwa njia ya mawasiliano ya intaneti baada ya kuthibitisha namba ya kadi ya mteja na maelezo mengine muhimu ya siri.

Kwa mujibu wa nyaraka za kiuchunguzi, tukio hilo la kuibiwa fedha kwenye akaunti ya mfanyabiashara huyo (jina linahifadhiwa) lilitekelezwa Januari 4, mwaka huu baada ya mtandao huo kuhamisha Sh 4,586,740, zikionekana zilifanya manunuzi kwenye duka la Shoprite, Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Tayari wafanyakazi kadhaa wa Shoprite na kijana mmoja ambaye ndiye aliyekuwa na kadi ya benki yenye jina la mfanyabiashara huyo wamenaswa na polisi na huenda wakati wowote wakafikishwa kortini kujibu mashtaka hayo.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambaye taasisi yake ina dhamana ya kusimamia sekta ya mabenki nchini, alikiri kuwepo tukio hilo huku akisisitiza, "Hilo ni jambo linalofahamika na linafanyiwa kazi kwa pamoja na vyombo vya usalama.

"Mkuu huyo wa BoT, alifafanua kwamba taasisi hiyo, vyombo vya usalama na wadau wengine wakiwemo wa taasisi za fedha wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu kwa kutumia taratibu zao za kazi kuhakikisha tatizo hilo halitikisi nchi kwa kasi."Tumekuwa tukijitahidi sana na wenzetu wa vyombo vya usalama kuhakikisha jambo hili halikui kwa kasi kubwa. Zipo hatua nyingi zinafanyika, lakini hatuwezi kuzieleza kwa uwazi hadharani," alisisitiza Profesa Ndulu.

Gavana Ndulu akifafanua hayo, duru hizo zaidi za kiuchunguzi zinaweka bayana kwamba tayari tukio hilo limetua mezani kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, tangu siku ya Jumapili ya Januari 9, mwaka 2011.DCI Kamishna Manumba alipoulizwa jana kwa njia ya simu, alisema alikuwa likizo na kushauri atafutwe msemaji wa jeshi hilo, lakini alipopigiwa simu yake ya kiganjani iliitia bila kupokelewa.Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, sakata hilo limekuwa likifanyiwa upelelezi na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Samson Kasala, ambaye naye hata hivyo, kila alipotafutwa hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa ikiita tangu mwishoni mwa wiki.

Hata hivyo, duru hizo za kiuchunguzi zinaonyesha kwamba mfanyabiashara huyo alibaini kufanyiwa wizi huo wa kimafia  Jumamosi jioni ya Januari 8, baada ya kufanya ukaguzi wake wa kawaida kwa kuangalia taarifa za moja ya akaunti yake kwenye mtandao wa kompyuta nyumbani kwake.Kwa mujibu wa taarifa hizo za kiuchunguzi, baada ya kupata taarifa hiyo mfanyabiashara huyo alipatwa na wasiwasi na ndipo baadaye akathibitisha kulikuwa na aina ya kughushi kulikoratibiwa na wezi wanaotumia kadi za kuchukulia fedha hapa nchini.

Taarifa hizo za kiuchunguzi zilionyesha kwamba mtu mmoja (jina linahifadhiwa kwa sasa), alikwenda katika duka la Shoprite Mlimani City na kununua bidhaa kwa kutumia kadi ya zamani ya mfanyabiashara huyo, ambaye hata hivyo, ilikuwa imeisha muda wake siku nyingine na kwamba alikwishapewa kadi nyingine.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba siku ya tukio mfanyabiashara huyo alikuwa na kadi yake nyumbani na hakuwahi kutembelea duka la Shoprite Mlimani City na kufanya manunuzi, hali iliyomfanya azidi kuthibitisha alikuwa kaibiwa fedha hizo ndipo alipoamua kuwasiliana na makao makuu ya benki yake kwa upande wa Uingereza.

Uchunguzi zaidi unaonyesha mtandao huo ulifanikisha mpango mkakati wake baada ya kutumia namba ya kadi ya mfanyabiashara huyo iliyokwisha muda tangu mwaka 2009, lakini mwenyewe alishangaa na hajui jinsi ilivyopatikana kwani aliiteketeza kadi hiyo tangu ilipokwisha muda.Uchunguzi zaidi umebaini kwamba, siku hiyo ya tukio kundi la vijana wa kiume na kike akiwemo mmoja aliyeonekana kama Mhindi au Mwarabu, walifanya manunuzi na kutoa kadi ya akaunti ya mfanyabiashara huyo kwa ajili ya malipo.

Nyaraka hizo zinaonyesha, manunuzi hayo yalifanyika baada ya kufanyika mawasiliano ya moja kwa moja (Offline) kati ya wahudumu wa Shoprite na makao makuu ya benki hiyo yalipo Uingereza, ambako walipotajiwa namba za kadi hiyo walitihibitisha  ni ya mfanyabiashara huyo ndipo waliporuhusu malipo ya fedha kutoka akaunti hiyo.'Offline' katika huduma za kibenki kwa mtandao, huwezesha wezi kuhamisha fedha moja kwa moja kutoka kwenye akaunti fulani kwenda nyingine baada ya kubaini namba za kadi maalumu yenye namba za siri za mteja kisha kufanya mawasiliano  na makao makuu ya benki ambayo baada ya kuthibitisha huweza kutoa fedha.

Katika tukio hilo, mawasiliano ya kuhamisha fedha hizo kutoka makao makuu kwenda Shoprite Mlimani City, yalifanyika kwa muda wa dakika 25 kwa kutumia kadi hiyo na kwamba, hadi sasa baadhi ya watu wanahojiwa na polisi na huenda wakafikishwa mahakamani wakati wowote.Taarifa kutoka Jeshi la Polisi zilisema kwamba sasa kuna watu wengi wa mikoa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam ambao wanashikiliwa na polisi kwa kuhusika kuamisha fedha kwenye akaunti za watu.

Hata hivyo, polisi wanatupia lawama mabenki kwamba huenda yanafaidika na wizi huo wa mtandao kwa kuwa mara vijana hao wanaojihusisha kazi hiyo chafu, kunaswa wao wamekuwa wagumu kwenda kutoa ushahidi mahakamani na hata polisi. “Sisi tunawashika, lakini baadhi ya benki hazitaki taarifa zao ziwe hadharani, lakini wananchi wanaendelea kuibiwa, tunaomba BoT ilazimishe benki ziwe wazi ile kuzuia matendo haya ya kimafia,” alisema polisi mmoja kutoka wa makao makuu ya Polisi.

Ofisa mmoja wa benki ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kwamba wao wamekuwa hawapati hasara kwa kuwa benki zina bima, hata mteja anayeibiwa naye hurejeshewa fedha zake.

No comments:

Post a Comment