Kambi ndogo yataka `kambi rasmi` ya upinzani bungeni iondolewe
Kambi isiyo rasmi ya upinzani, imekusudia kuwasilisha hoja binafsi kuomba kutengua kanuni namba 131 ili kuondoa neno ‘kambi rasmi’ bungeni kwa nia ya kupewa nafasi ya uwenyekiti kwenye kamati za kudumu.
Mwenyekiti wa kambi hiyo, Hamad Rashid Mohamed, alisema jana kuwa lengo lao sio kupata marupurupu, bali ni kushirikishwa kwenye kamati.
Hamad, ambaye pia ni Mbunge wa Wawi (CUF), alisema tayari wameshajipanga kuwasilisha hoja hiyo ili vyama vingine vya upinzani viruhusiwe kuongoza baadhi ya kamati za bunge.
Hamad alimlaumu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa kuishutumu CUF kwamba, inawasiliana na chama hicho kupitia vyombo vya habari wakati na wao (Chadema) hufanya hivyo akitolea mfano taarifa ya Kamati Kuu ya Chadema.
Hata hivyo, alisema walipokea barua kutoka Chadema inayosema kuwa chama hicho kitaunda serikali kivuli ndani ya Bunge bila kushirikisha vyama vingine.
“Sisi tulifahamu mapema. Tangu siku ya mdahalo, nilimwambia Mbowe, baada ya kusema kwamba, sisi tuna ushirikiano Zanzibar. Tulidhani Chadema wangeheshimu maamuzi ya wananchi kuhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja Kitaifa kwa sababu haya hayakuwa maamuzi ya CUF,” alisema. Alisema wamesikitika kwa hatua ya Chadema kuwatenga Wazanzibari kwa madai kuwa CUF sio chama cha upinzani tena.
“Tunataka kuwahakikishia Watanzania kwamba, CUF ni chama cha upinzani na tutaendelea kutetea maslahi yao kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa, tofauti yetu na wao itakuwa moja tu tutaangalia zaidi maslahi ya taifa,” alisema.
Hamad alisema wataheshimu sheria na katiba ya nchi na kuchambua hoja zenye maslahi ya taifa.
Kuhusu Katiba mpya, Hamad alisema chama hicho kinataka rasilimali za nchi, ikiwamo ardhi, zisimamiwe na wananchi sio serikali.
Pia Katiba itamke wazi juu ya udhibiti wa malighafi za viwandani, yakiwamo madini ya uranium, mipaka ya raia, tume huru ya uchaguzi, mahakama ya kikatiba na kupunguza madaraka ya Rais.
Kuhusu tume huru, alisema rasimu, ambayo wameshaiwasilisha, inaeleza bayana kuhusu muundo wa tume hiyo kwa kupendekeza makamishna wawe wanaomba nafasi hizo na kuthibitishwa na Bunge.
No comments:
Post a Comment