Thursday, 3 February 2011

Maandamano makubwa yaja nchini





*Kupinga mabilioni ya DOWANS
Stella Aron na Christina Gauluhanga, jijini

WAKATI Jeshi la Polisi likiyabariki kwa masharti kufanyika kwa maandamano ya Chama Cha Wananchi (CUF), viongozi wa chama hicho wameibuka na kusema hawakubaliani na masharti hayo.Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, ameliambia Dar Leo leo asubuhi kuwa wamekubali maandamano hayo yafanyike lakini kinachotakiwa ni kufanya mabadiliko ya uwanja ambapo wao walipanga kukitumia cha Kidongo Chekundu.

Wakati Kova akitoa sharti hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, amesema hawapo tayari kubadili uwanja kwa kuwa wana imani kuwa uwanja huo upo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii.

Amesema viongozi wa CUF wana akili timamu na wana imani kuwa wenye njama hizo ni Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa vile pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, naye ni CCM na uwanja huo upo chini yake.

“Sisi tunafahamu kiwanja hicho kinatumika kwa shughuli mbalimbali na mwaka jana tumefanya mikutano miwili hivyo haiwezekani kipindi cha mwezi mmoja tuambiwe kuwa kiwanja hicho hakitumiki kwa mambo ya kisiasa,” amesema Mtatiro.

Mtatiro amesema maandamano hayo ya kupinga ulipaji bilioni 94 kwa kampuni ya Dowans yatafanyika Februari 7, mwaka huu, na yataanzia Buguruni Sheli na kumalizia Kidongo Chekundu.

Akisisitiza kuwa maandalizi ya maandamano hayo yamekamilika, Mtatiro ameiomba Polisi kufika tu kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, lakini masuala ya uwanja waachiwe wenyewe CUF.

Kamanda Kova amesema wamewaruhusu waandamanaji hao isipokuwa wafuate masharti watakayokubaliana ili kusitokee rabsha zozote zenye kusababisha uvunjifu wa amani.

No comments:

Post a Comment