Thursday, 3 February 2011

Jaji Mkuu asema hali ni mbaya

 
Jaji Mkuu, Mohamed Othman

Mahakama za Mwanzo nchini zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa majengo na kulazimika kuendeshea shughuli zake kwenye maghala, masoko, na vilabu vya pombe kutokana na ufinyu wa bajeti.
Kadhalika, mahakama inakabiliwa na upungufu wa mahakimu ambapo hakimu mmoja hulazimika kutoa huduma katika mahakama tatu hadi nne kwa wakati mmoja ambazo zina umbali mrefu huku wakijitegemea kwa usafiri.
Hayo yalielezwa jana na Jaji Mkuu, Mohamed Othman, mbele ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Mheshimiwa Rais majengo mengi ya Mahakama ya Mwanzo hayana staha, mahakama ya Kate, Sumbawanga iko kwenye jengo lililokuwa ghala la kijiji, za Katoro, Geita na Mugeta Bunda, ziko kwenye ghala la mazao, Chikundi, Mtwara iko kwenye jengo la soko la kijiji, Nachingwea iko kwenye jengo la klabu ya pombe huku zile za Kilimarondo na Ndomoni, Lindi zikiwa kwenye gulio,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza: “Mahakimu wa mahakama za mwanzo wanafanyakazi katika hali ngumu kutokana na baadhi yao kuhudumia mahakama zaidi tatu hadi nne kwa wakati mmoja huku wakitumia fedha zao kuzunguka umbali mrefu na mahakama ikishindwa kuwalipa posho za kazi hizo.”
Alisema mbali na hilo, majengo ya mahakama yamechakaa, lakini serikali katika bajeti yake ya mwaka 2010/2011 ilitoa bajeti ya kujenga mahakama za mwanzo tano tu.
Jaji Chande alisema kwa upande wa utendaji na utoaji haki wa mahakama bado kuna mrundikano wa kesi kutokana na bajeti kuwa ndogo kwa ajili ya kuendesha vikao hasa katika kesi za mauaji.
Naye Rais Kikwete alisema dhamira ya serikali kuendeleza mhimili wa Mahakama iko pale pale kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma na utendaji haki kwa wananchi.
Rais Kikwete alisema mchakato wa kuanzisha mfuko wa mahakama unaendelea ambapo muswada wake utawasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Aprili mwaka huu ili uingizwe kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012.
Nawapongeza kwa kutambua umuhimu wa elimu kuhusu mahakama kama hatua ya msingi ya utatazi wa migogoro katika jamii, utasaidia wananchi kuelewa maamuzi yanayotolewa mahakamani, Rais hana mamlaka ya kuyaingilia,” alisema.
Aliongeza: “Watanzania wanatakiwa kuamini kwamba lililoamriwa na mahakama Rais hana mamlaka nalo na kwamba maamuzi yake yataheshimiwa…Pia, mtakuwa mmenisaidia watu watapata ufahamu kwamba mahakama ikitoa uamuzi Rais sina tena mamlaka ya kuingilia maamuzi hayo yatabaki kuheshimiwa.”
Rais alisema serikali ina dhamira kubwa ya kuendeleza mhimili wa Mahakama nia ni kufika hatua ya kila mkoa nchini kuwa na jengo lake la mahakama kuu.
Katika miaka mitano iliyopita tumefanya mambo mengi mazuri na nawaahidi kufanya vizuri zaidi katika miaka ijayo. Tumejenga majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kagera na Shinyanga. Tutaendelea kutenga fedha ili ujenzi ufanyike katika mikoa iliyobakia hatua kwa hatua mpaka kila mkoa uwe na Mahakama Kuu yake.
Sina kipingamizi kwa upande wa kuongeza Majaji ili mmalize kiu yenu. Nileteeni mapendekezo yenu nitafanya uteuzi kama nilivyofanya miaka iliyopita,” alisema.
WAKILI WA SERIKALI ATAKA KATIBA MPYA
Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kanda ya Iringa, Okoka Mgavilenzi, amesema kuwa katiba mpya ni muhimu na kwamba madai hayo hayaepukiki kwa sasa kwa kuwa katiba iliyopo imejaa vipengele vilivyopitwa na wakati.

Wakili huyo alisema licha ya katiba ya sasa kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili, bado haiwafikii wanajamii kwa kuwa inauzwa na walio wengi hawaifahamu.

Wakili Mgavilenzi alikuwa akisoma hotuba yake katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya mahakama mjini Iringa.

Mgavilenzi alisema ni muhimu katiba ipatikane bure au kwa gharama ndogo na nafuu kwa kila mwananchi na kwamba hilo litahitaji ligharimiwe na serikali ili wananchi waipate na kuifahamu vyema.

UPUNGUFU WA VYUMBA ARUSHA
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, inakabiliwa na ukosefu wa vyumba kwa ajili ya kuhifadhia mahabusu wanawake wakati wanapokuwa wakisubiri mashauri yao, hali inayowakosesha wenye watoto haki ya kunyonyesha vizuri.
Hayo yalisemwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Aisha Nyerere, alipokuwa akitoa hotuba yake, kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Arusha.
Jaji Nyerere alisema hilo ni tatizo kubwa linalowalazimisha Mahakama, kuwaweka nje ya Mahakama mahabusu hao ili waweze kunyonyesha watoto wao vizuri, huku wakiwa chini ya ulinzi mkali.
Hali hii ni hatari kwani mahabusu anakosa haki yake ya msingi kama hiyo ya kunyonyesha kwa uhuru na kulazimika kunyonyesha hadharani,” alisema.
Aidha, alitaja kero ya kutokuwepo ukumbi kubwa za kufanyia mashauri, ambapo alisema kwa sasa kuna ukumbi mmoja wa wazi, hali ambayo inaathiri usikilizwaji wa mashauri.
Upungufu huu unalazimisha wakati mwingi kupanga zamu za mahakimu kuingia kazini kwa kupokezana nusu siku, wengine asubuhi na wengine mchana, jambo linalolazimisha kusikiliza kesi chache kwa siku na kusababisha malalamiko kwa jamii, kuwa tunaandaa mazingira ya rushwa,” alisema Jaji Nyerere.
Alimshukuru Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, kwa uamuzi wake wa kuahidi ujenzi wa mahakama 20 za mwanzo, nchini kote na Arusha ikiwa mojawapo.
Hii itatupunguzia mrundikano wa mahabusu na kesi zisizo na lazima katika Mahakama zetu chache zilizopo, na kuupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya jamii kuhusu ucheleweshawaji wa kesi zao,” alisisitiza Jaji Nyerere.
JAJI SHANGALI ATAHADHARISHA
Jaji Mfawidhi wa Mhakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mary Shangali, amesema uelewa mdogo wa elimu kwa wananchi kuhusu mahakama inavyofanya kazi zake ni mmojawapo ya vikwanzo vinavyowanyima fursa ya kutafuta haki, muda na mahali mwafaka.
Alisema katika maadhimisho hayo mjini Dodoma jana kuwa hali hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa mahakama kwa kuwa kutojua haki inasababisha jamii kuwa na mtizamo hasi. Aliviomba vyombo husika kuendelea kueelimisha jamii.
MAHAKAMA ZAFUNGWA KWA UCHAKAVU
Imeandikwa na Hellen Mwango (Dar), Godfrey Mushi (Iringa), Peter Mkwavila (Dodoma), Cynthia Mwilolezi (Arusha) na Renatus Masuguliko (Geita).
 

No comments:

Post a Comment