Sunday, 6 February 2011

Dk. Shein asema CCM bado ni imara

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema CCM bado kipo imara na kwamba ni mawazo potofu kusema kimepoteza dira.
Alisema kinachotakiwa kufanywa na viongozi wa chama hicho ni kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kukipa sura ya ushindani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Dk. Shein alisema hayo alipokuwa akihutubia wanachama wa CCM baada ya kuongoza matembezi ya mshikamano ya kuadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa kwa chama hicho mwaka 1977 baada ya vyama vya TANU na ASP kuungana.
Matembezi hayo yalianzia ofisi ya CCM ya Mkoa wa Mjini Magharibu hadi viwanja vya Mwembekisonge mjini hapa ambako ulifanyika mkutano wa hadhara.
Dk. Shein alisema watu wanaosema CCM imepoteza mwelekeo, wao ndio wamepoteza dira kwa vile CCM bado kina viongozi bora na ndio maana wananchi wanaendelea kukipa ridhaa ya kuongoza dola.
“Chama chetu katika kipindi chote kimeendelea kuwa imara na kina viongozi bora, ndo maana wananchi wanakipenda na kukithamini…watu wanadhani kimepoteza mwelekeo, wao ndio wamepoteza mwelekeo na dira,” alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema maendeleo ya demokrasia yanaoonekana nchini ndio kipimo cha uongozi bora wa CCM ambacho sasa kinaadhimisha miaka 34 kikiwa imara.
“Chama chetu kinaadhimisha miaka 34, kikiwa imara sana na ushindi tulioupata Zanzibar na Tanzania bara…ushindi wa asilimia moja tuliopata Zanzibar sio mdogo,” alisema Dk. Shein.
Kuhusu mwenedo wa serikali ya awamu ya saba yenye muundo wa umoja wa kitaifa, Dk. Shein alisema iko katika mwelekeo mzuri wa kusogeza maendeleo kwa wananchi bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Saleh Ferouz, aliwataka wanachama wa CCM kuwa makini katika uchaguzi ndani ya chama hicho utaofanyika mwakani.
Katika risala yao wanachama wa CCM wa Mkoa wa Mjini Magharibi, walilalamikia ugumu wa maisha wakisema chanzo cha hali hiyo ni mfumuko wa bei na kutaka serikali ichukue hatua.

No comments:

Post a Comment