Mabadiliko makubwa ndani ya CCM yaja
Mchakato katiba mpya umeanza
CCM
Rais Jakaya Kikwete, ameahidi kufanya mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho na kuwekeza nguvu kubwa kwa vijana ili kukinusuru. Pia amesema mchakato wa Katiba mpya umeanza.
Kuhusu mabadiliko ndani ya CCM, Rais aliwataka wanaCCM kutofanya ajizi katika suala la kuwatazama viongozi na watendaji wanaokipaka matope chama hicho ili kuepuka kushindwa ghafla.
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho, aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akizungumza katika maadhimisho ya miaka 34 tangu kuzaliwa kwa CCM na kueleza kwamba hakina budi kufanya hivyo"wakati wa Kamati Kuu (CC) na Halmaashauri Kuu (NEC) tutalijadili pia suala hili la mageuzi ndani ya chama."
“Nitapenda nijadiliane na wenzangu namna tutakavyotekeleza agenda muhimu kwa uhai na maendeleo ya chama hili ndugu zangu haliepukiki,”alisema.
“Tuutazame uongozi wetu na muundo wetu kama unakidhi haja na kama sio mzigo unaokipaka matope chama chetu wale tunaoweza kuachana nao sasa tuachane nao wale tutakaofuatana nao baadaye tufuatane nao,”alisema.
Alisisitiza kuwa wanachama wa chama hicho wasilionee haya jambo hilo na wala wasilifanyie ajizi hata kidogo tutashindwa ghafla.
Alisema kuwa athari zitakuwa kubwa zaidi pale chama kitakaposhindwa kuwaridhisha watu pamoja na matendo na tabia zisizoridhisha za viongozi na wanachama wa chama hicho.
Alisema kwa maana nyingine chama lazima kiinge tabia ya nyoka kwa maana wakati mwingine nyoka kutoa gamba lake na kupata gamba jipya.
Alisema kuwa hali ya kifedha ya chama hicho si nzuri na kuwataka kutafuta vyanzo vipya vya mapato.
Alisema kuwa ruzuku katikak chama hicho imeshukuka kwa sh. milioni 200 baada ya vyama vya upinzani kuongeza viti vya ubunge na udiwani.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amesema matayarisho ya mchakato wa kuandika Katiba mpya yameanza.
Kikwete alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikisherehekea miaka 34 tangu kianzishwe mwaka 1977.
Alisema muswada kwa ajili ya kuandika katiba mpya utatoa taratibu za kuongoza, kuendesha, kusimamia na kuhitimisha mchakato wa suala hilo.
“Kiserikali matayarisho yanaendelea kupeleka muswada bungeni wa kuanzisha mchakato rasmi utakaotuelekeza kwenye Katiba Mpya na taratibu zake za kuongoza, za taratibu zake za kuendelesha, taratibu zake za kuusimamia na taratibu za kuhitimisha,” alisema.
Alisema kuwa Katiba ni mali ya Watanzania na kwamba washiriki katika kuizungumza kwa uwazi bila ya vikwazo. Alisema kwa wale wenye mijadala wavumiliane kwa sababu kutakuwa na mawazo tofauti.
“Usiwazomee mwenye wazo tofauti, usijifanye wewe unahaki zaidi ya mwenzako, usifanye mawazo yako wewe ni bora kuliko ya mtu mwingine na bado unajiita wewe ni mwana demokrasia, hujui demokrasia wewe ni dikteta lazima uwe tayari kupokea mawazo tofauti, mbona sisi tunapokea mawazo tofauti na hatujapiga watu virungu,”alisema.
Alisema serikali na chama chake ni wadau wanaohitaji Katiba ihusishwe kukidhi mahitaji na wakati tulionao na matarajio yetu ya baadaye.
Alisema hata kama kusingekuwepo mapendekezo ya watu mbalimbali ni dhamira yao kufanya hivyo na kukumbusha miaka miwili ya maadhimisho ya chama hicho alizungumza haja ya kuwa na katiba mpya.
“Sikubaliani hata kidogo na wale wanaosema katiba hii mbaya, katiba mbaya haizai taifa lenye umoja, katiba mbaya hazai taifa lenye amani na utulivu, haizai taifa ambalo maendeleo yanaonekana, tungekuwa hatushughuliki na maendeleo tungeuana tu kama katiba ni mbaya,”alisema na kuongeza,
“Miaka 50 ni mingi Katiba iliyotufikisha hapa tulipo itazamwe na yapo mambo yatakayohitaji kurekebishwa, kuondolewa na mengine yaliyofikiriwa kuwepo,” alisema.
Rais alisema hatma ya hayo yote ni mchakato utakaowezesha kuzaliwa kwa Katiba Mpya.
Alisema wanataka kufanya mabadiliko makubwa ya msingi ambayo yatafanana na sura ya taifa la sasa lengo likiwa ni kulipeleka mbele miaka mingi.
“Baada ya tukio lile la Arusha mji wa kimataifa kumekuwa na maswali mengi tuendelee kuwepo Arusha ama tusiwepo kwa mgogoro ambao hauna sababu ya kuwepo,”alisema.
No comments:
Post a Comment