Sunday, 30 January 2011

Na Salma Said Zanzibar
KUANZIA sasa wasafiri wote wanaoingia Zanzibar watalaazimika kuwa na cheti kinachoonyesha wamepata chanjo dhidi ya ugonjwa wa manjano.
Nabu Waziri wa Afya wa Zanzibar , Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema jana kuwa uamuzi huo ni hatua ya kujikinga na tishio la kukumbwa na aina fulani ya ugonjwa wa homa ya manjano uliolipuka nchini Uganda.
Dk. Sira alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa kikao cha nane cha Baraza la Wawakilishi kilichomalizika jana huko Mbweni nje kidogo kutoka mjini hapa.
Kikao hicho, pamoja na mambo mengine kilipitisha muswada wa sheria mpya ya muundo wa utumishi wa umma uliowasilishwa na Waziri wa Nchi na Utawala Bora, Haji Omar Kheri.
Akitoa taarifa hiyo, Dk. Sira alisema kwa watu wanaokusudia kusafiri kwenda nje ya Zanzibar pia wanashauriwa kupata chanjo kabla ya kusafiri.
Alisema taarifa juu ya wasafiri kutakiwa kuwa na cheti cha chanjo dhidi ya ugonjwa huo, imesababzwa katika balozi zote za Tanzania na kwamba wanaotakiwa kuonyesha vyeti hivyo ni pamoja na watalii.
Dk Sira alifafanua kuwa aina ya ugonjwa huo tayari umeua watu 50 kati ya watu wote 256 walioambukizwa nchini Uganda.
Haikuelezwa ulizuka lini nchini Uganda, lakini Dk. Sira alisema ugonjwa huo unaenezwa na mbu na kwamba mpaka sasa tiba ya kupambana na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo haijapatikana.
Alishauri watu wanaposikia dalili ya mafua, uchovu, homa za vipindi na macho kuwa na rangi ya njano, waenda hospitali.
Alisema ingawa taarifa hazionyeshi kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo, wananchi wanatakiwa kuzingatia masharti ya usafi wa mazingira ili kuzuia uchafu kuibua mazalio ya mbu.


No comments:

Post a Comment