Sunday, 30 January 2011

Na Salma Said

TRA Waicheza Shere Serikali ya Zanziba

MAMLAKA ya kodi ya Mapato Tanzania (TRA) inaidangaya serikali kwa kuendelea kutekeleza utaratibu wa kodi kwa waagizaji bidhaa wa Zanzibar .
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema hapa jana kuwa kitendo cha kutoza kodi mara mbili kwa bidhaa zinazoingia Zanzibar ni ukosefu wa uamunifu wa TRA kwa wafanyabiashara.
Mazrui alikuwa anajibu malalamiko ya Abdallah Juma Abdallah (Chonga) na Makame Msimba Mbarouk (Kitope) katika Baraza la Wawakilishi juu ya utaratibu wa TRA kuendelea kutoza kodi mara mbili kwa bidhaa ambazo tayari zimelipiwa kodi katika mojawapo ya bandari za Tanzania .
Waziri Mazrui alisema kwa kuendelea kufanya hivyo, wafanyakazi wa TRA wakiuka sheria katika utekelezaji wa taratibu za kodi kwa bidhaa zinazoingia nchini kupitia bandari za Dar es Salaam na Zanzibar .
“Sheria inasema, bidhaa ikilipiwa kodi katika moja ya bandari nchini, isilipiwe tena katika bandari nyingine kwa vitu vinavyoingizwa katika pande mbili za muungano,” alisema.
Alisema pamoja na wawakilishi hao kutoa malalamiko ndani ya kikao cha baraza, anashangaa pia kuona bado anaendelea kupata malalamiko ya wadau wengine wa sekta ya biashara juu ya mwenendo wa TRA.
“Wapo watu wameniletea malalamiko wakisema jana (juzi) wamelipa kodi mara mbili,…bara na Zanzibar,” alisema Mazrui na kuongeza kuwa ili kusaidia juhudi za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, wanaofanyiwa vitendo hivyo watoe ushahidi kwa kuonyesha risiti wanazopewa baada ya kulipa kodi.
Alisema anachojua ni kwamba TRA imetoa barua rasmi kusisitiza kwamba bidhaa ilipiwa kodi katika moja ya bandari nchini, isilipiwe kodi tena inaposafirishwa kwenda sehemu nyingine ya eneo la muungano.
Katika swali la msingi, Mbarouk Wadi Mussa (Mkwajuni) alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kuwaondolea kero inayosababishwa na TRA kuwatoza kodi wafanyabiashara wa Zanzibar wanapoingiza bidhaa Tanzania bara ambazo tayari zimelipiwa Zanzibar .
Akijbu swali hilo , Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko alisema ni kweli kuna malalamiko ya muda mrefu ya wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kwenda Tanzania bara kutozwa kodi kwa bidhaa zilizolipiwa wakati wa kuingia nchini kupitia Zanzibar . 

No comments:

Post a Comment