Friday, 28 January 2011

Viongozi Wote Watapekuliwa Isipokuwa Watano tu-Serikali


eurofly


File:Zanzibar International Airport.jpg
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepiga marufuku matumizi mabaya ya uwanja wa ndege utaotumiwa na wafanyabiashara maarufu, mawaziri wastaafu na viongozi mbali mbali wanaotumia sehemu ya wageni mahsusi (VIP) na kukiuka sheria ya kukaguliwa.
Kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar ni viongozi watano pekee ndio waliotajwa katika sheria hiyo kuwa wanaoruhusiwa kupita VIP bila ya kukaguliwa akiwemo rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais, Jaji Mkuu na Spika wa Baraza la Wawakilishi.
Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamad Masoud Hamad aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliyetaka kujuwa kwa nini baadhi ya watu wanakwepa kupekuliwa wakiwemo wafanyabiashara maarufu na watendaji wa serikali.
Hamad alisema watu wote ambao hawajatajwa katika sheria wanapaswa kukaguliwa wakiwemo waziri, wabunge, wawakilishi, mawaziri wastaafu na wafanyabiashara maarufu ambao ndio wakwepaji wakubwa wa kukaguliwa katika viwanja vya ndege vya Zanzibar .
Waziri huo alisema suala la kufnaya kazi kwa mazowea limefikia kikomo na hivi sasa sheria zitakuwa zinafuatwa ambapo kila msafiri atakaguliwa mizigo yake bila ya kujali yeye ni nani kwa kuwa ni haki ya kisheria kukaguliwa mizigo na wasafiri wote wanaosafiri nje ya nchi.
“Mheshimiwa Spika nataka kuwajulisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba Mawaziri,Wabunge na Wawakilishi na wafanyabiashara maarufu wote wanapaswa kupekuliwa wakati wanaposafiri nje ya nchi….nawaomba wakubwa waache vitisho wakati wanapokaguliwa maana wengine huwa wanasema unanijua nani mimi…sasa nasema tufuate sheria zinavyosema na tuache kufanya kazi kwa mazowea” alisisitiza Hamad.
Alisema wapo baadhi ya wakubwa wanatowa vitisho kwa watendaji wa uwanja wa ndege wakati wanapotaka kuwakaguwa kwa madai kwamba hawapaswi kukaguliwa kutokana na vyeo vyao.
“Tatizo letu kubwa Mheshimiwa Spika ni kwamba katika nchi hii kuna kujuwana sana ….umuhali pamoja na uzoefu ndio unaotumika kila sehemu ya kazi kwa hivyo tunasema tunataka kufuata sheria na sheria ifuate mkondo wake kila mwneye haki ya kukaguliwa akaguliwe na kwa nini mtu aogope kukaguliwa jamani…ikiwa wewe huna tatizo unagopa nini?” alihoji Waziri huyo.
Akiongea kwa kujiamini Waziri huyo alisema moja ya kikwazo kikubwa kinachotowa mwanya watu kupita bila ya kukaguliwa ni badhi yao hutumia fursa hiyo na kupitisha madawa ya kulevya kwa kuwa mazowea yaliojengeka baadhi ya wakubwa huwa wanatoa vitisho kwa wafanyakazi kwamba watafukuzwa kazi iwapo watawakagua watu hao jambo ambalo alisema ni kinyume na sheria.
Alisema wapo baadhi ya wakubwa huwatisha watendaji wa uwanja wa ndege wa Zanzibar ikiwemo kuwatisha kuwafukuza kazi wakati wanapokaguliwa.
Aidha Hamad aliwataka wafanyabiashara kuacha kutumia huduma za sehemu ya wageni maarufu VIP kwa sababu hawana hadhi ambapo wafanyabiashara wengi wanaotumia huduma za uwanja wa ndege wakati hawastahiki kutumia fursa hizo.
“Mheshimiwa wapo wafanyabiashara wengi wanaotumia huduma za uwanja wa ndege ikiwemo sehemu ya wageni maarufu VIP na kukwepa kukaguliwa …hali hii imejengeka na baadhi ya wafanyakazi w auwanja wa ndege wamekuwa waoga mno kufanya kazi kwa taratibu za sheria kutokana na mazowea haya mabaya …lakini sasa tunasema yale ya zamani yamekwisha na sasa tunataka sheria ifanye kazi yake” alisema Hamad.
Awali Hamad alisema kwamba uwanja wa ndege za Zanzibar utapatiwa vifaa vya kisasa ikiwemo vya kupaza sauti na kutoa matangazo kwa watu wanaosafiri ili sauti hiyo isikike vyema kwa wasafiri.
Alisema kwamba ni kweli hadi sasa hakuna vipaza sauti viliopo katika uwanja wa ndege wa Zanzibar ambavyo ni muhimu kwa ajili ya watu wanaosafiri hasa wakati ndege inapotaka kuondoka hutakiwa vipaza sauti ziwe vinatoa taarifa maalumu za uwanja wa ndege ili wasafiri waweze kusikia iwapo ndege yao inataka kuondoka.
“Yupo mtaalamu hivi karibuni atakuja nchini kwa ajili ya kufanya utafiti na kuweka vipaza sauti pamoja na bodi la ratiba za safari za ndege zinazosafiri katika viwanja vyetu hivi”aliongeza Waziri huyo ambaye ni Engineer.
Alisema huduma hizo ni muhimu sana kwa sababu ndiyo zitakazoufanya uwanja huo kufikia vigezo vyote vinavyotakiwa kuwa wa kimataifa na kusisitiza mashirikiano kati ya wananchi na wafanyakazi ili sheria na taratibu za usafiri zifuatwe.
Hamad ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Ole (CUF) alisema tayari benki ya Exim kutoka China itajenga jengo la kisasa la kusafiria abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume na ujenzi huo utahakikisha unaondowa tatizo la uhaba wa nafasi katika uwanja wa ndege wa Zanzibar kwa abiria.
Wakati huo huo serikali imetangaza kubadilisha majina ya viwanja wa ndege vya Unguja na Pemba ambapo uwanja wa Pemba uliokuwa ukiitwa kiwanja cha Karume hivi sasa utaitwa uwanja wa ndege wa Pemba wakati uwanja wa Unguja utaitwa Abeid Amani Karume Internation airport
“Mheshimiwa Spika kiwanja cha ndege cha Zanzibar kimebadilishwa jina na kuitwa Abeid Amani Karume Internation Airport ili kulikuza na kulienzi jina la muasisi wa mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na rais wa kwanza wa visiwa vya Unguja na Pemba” alisema Issa Haji Ussi Naibu Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano.
Ussi alisema kwamba kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho kilikuwa kikijulikana kwa jina la kiwanja cha ndege cha Karume, hivi sasa kinaitwa kiwanja cha ndege cha Pemba baada ya mabadiliko hayo.
“Mheshimiwa Spika hivi sasa serikali haijafikiria jina hilo la kiwanja cha ndege cha Pemba kuitwa kiwanja cha ndege cha Thabit Kombo lakini hata hivyo wizara yangu itafikiria suala hilo na kufanya hivyo inapowezekana: alisema Naibu huyo.
Mwakililishi wa Jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija alitaka kujua sababu zipi zilizopelekea viwanja hivyo vya ndege kubadilishwa majina badala ya kuachwa yale majina yake ya awali.
“Kwa kujua viwanja vyote viwili vimepewa jina kubwa la kiongozi wa kwanza na mkombozi wa Zanzibar na kwa kuwa hadhi ya viwanja hivyo ni tofauti, jee kuna mpango gani wa karibu wa kukifanya kiwanja cha Pemba kuwa na hadhi inayokwenda sambamba na jina la kiongozi wetu huyo” alihoji Mwkailishi huyo na kuongeza kwamba..
“Kwa kuwa miongoni mwa majina makubwa na yenye historia muhimu kwa uhuru wa Zanzibar ni pamoja na Mzee Thabit Kombo, kwa nini kiwanja cha Pemba hakipewi jina la kiongozi huyo” alihoji Hija.
Naye Mwakilishi wa Ziwani (CUF), Rashid Seif Suleiman alitaka kujua kiwanja cha ndege cha Pemba kipo katika hadhi gani na serikali ina mpango gani wa kukipandisha daraja kiwanja hicho.
Akijibu swali hilo Naibu waziri wa wizara hiyo alisema kw akuzingatia viwnago vya viwanja vya ndege vya kitaifa na kimataifa na viwango vyengine vinavyotambulika kiwanja cha ndege cha Pemba kwa kuzingatia daraja au viwango vya ndege, ni kiwanja cha kitaifa.
Aidha alisema serikali ina mpango wa kukipandisha daraja kiwanja hicho kwa kurejesha taa za kuongozea ndege kuruka na kutua nyakati za usiku na wakati wowote hali ya hewa inapochafuka pamoja na kufanya ukarabati wa jengo la abiria

No comments:

Post a Comment