Saturday, 29 January 2011

Kigogo mwingine wa CHADEMA kortini




Na Ratifa Baranyikwa


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, anayefanya kazi katika shirika la Umoja wa Mataifa jana amefikishwa mahakamani kwa kosa la kuandamana kinyume cha sheria.
Polisi wanamhusisha Mwigamba na vurugu zilizotokea Arusha Januari 5, mwaka huu; lakini iliwachukua muda kumtia mbaroni kutokana na mazingira ya kazi yake katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia mauaji ya Rwanda (ICTR).
Kufikishwa kwake mahakamani jana kunamfanya mwenyekiti huyo wa Arusha kuungana na watuhumiwa wengine 27, wakiwamo viongozi wakuu wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi ya kufanya kusanyiko kinyume cha sheria.
Miongoni mwao ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa; wabunge Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini); Godbless Lema (Arusha Mjini); Joseph Selasini (Rombo); na wengine.
Habari toka mahakamani hapo zinaeleza kuwa Mwigamba alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana majira ya saa tano asubuhi, baada ya kuwekwa ndani kwa takriban masaa mawili.
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Charles Magesa, mwenyekiti huyo wa mkoa wa Arusha alidaiwa kuandamana kinyume cha sheria na hivyo kesi yake kuunganishwa na ile inayowakabili kina Mbowe na wengine.
Hata hivyo Mwigamba alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 22 mwaka huu ambapo kesi kama hiyo inayowakabili kina Mbowe na wengine itatajwa tena.
Akizungumza kwa njia ya simu mara baada ya kutoka mahakamani, Mwigamba ambaye alikuwa nje kwa dhamana hadi jana baada ya kukamatwa wiki moja iliyopita kwa madai hayo alisema kuwa aliamriwa na Jeshi la Polisi kuripoti ofisini kwao jana.
Alisema jana majira ya saa mbili asubuhi, aliripoti kituoni hapo lakini ghafla wakamueleza kuwa anakwenda mahakamani.
UN makao makuu wamesema maofisa wao watakuwa wakimfuatilia kuhakikisha anatendewa haki kama mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment