Na Mauwa Mohammed, Zanzibar |
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, imekiri kwamba historia ya Zanzibar imepotoshwa na baadhi ya waandishi wakiwemo wataalam wanaoandika historia za Zanzibar ili kukidhi maslahi yao binafsi. Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Bihindi Hamad Khamis alipokuwa akijibu swali la msingi aliloulizwa na mwakilishi wa Kiwani Hija Hassan Hija, aliyetaka kujua hatua itakayochukuliwa na serikali kwa waandishi wenye kupotosha ukweli wa historia ya Zanzibar . Mwakilishi huyo alitaka kujua ni eneo gani la kihistoria kati ya Zanzibar na Bagamoyo ambapo kulikuwa ni kitovu cha utumwa. Akijibu swali hilo Bihindi alisema serikali itawachukulia hatua wale waandishi wa historia wenye lengo la kuipotosha jamii kwa makusudi. Aidha alisema kwa mnasaba huo ipo haja ya kutayarisha wataalam wenye uwezo na kupewa jukumu la kuandika historia sahihi ya Zanzibar. Alisema hatua za awali za kuandika vitabu na vijarida zimeanza pamoja na kuwapeleka wafanyakazi masomoni katika vyuo mbali mbali ili wafanye kazi kwa ufanisi na ufasaha zaidi. Hata hivyo alifahamisha kuwa eneo lililokuwa ni soko kuu na kitovu cha biashara ya watumwa ni Zanzibar, Bagamoyo ilikuwa ni sehemu ya kupitia kabla ya kusafirishwa kupelekwa Zanzibar ambako kulikuwa na soko kuu. Watumwa walikuwa wakisafirishwa kupelekwa nchi mbali mbali ikiwemo Visiwa vya Bahari ya Hindi, kama Maurishasi, Shelisheli na nchi za Kiarabu, Umoja wa Nchi za Kiarabu na wengine walibaki Zanzibar kufanya kazi za kilimo cha mikarafuu na minazi na wengine wakitumika katika kazi za majumbani. |
No comments:
Post a Comment