Saturday, 29 January 2011

Serikali yaahidi kurejesha posho walizokatwa polisi







Midraji Ibrahim
SERIKALI imekiri kukatwa kwa posho za upelelezi na nyumba kwa askari polisi kwa miezi ya Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu, huku ikitoa taarifa zinazokanganya kuhusu suala hilo.Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Khamis Kagasheki aliliambia Mwananchi jana kuwa, uamuzi wa kuondoa posho za watumishi umechukuliwa ili kubana matumizi yake, lakini haukutakiwa kuhusisha watumishi wa jeshi la polisi.
Lakini jana jioni msemaji mkuu wa Wizara  ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga aliliambia mwananchi  kwamba kukatwa kwa malipo ya polisi kulitokana na mfumo wa malipo ya mishahara kuruka vipengele viwili ambavyo ni posho ya upelelezi na ile ya pango.
Kwa upande wake Kagasheki alisema uamuzi wa kuondoa posho ulichukuliwa na serikali katika kubana matumizi yake, lakini haukutakiwa kugusa polisi au majeshi.

Balozi Kagasheki alisema posho ya upelelezi na nyumba kwa polisi zimeondolewa pengine kwa hasira za watumishi wa hazina kwa sababu wanazozijua, lakini sio maelekezo ya serikali. Inakadiriwa zaidi ya polisi 16,000 wameathirika mpango huo.Mwananchi jana liliripoti taarifa za kufyekwa kwa  mishahara ya polisi, huku mamlaka zinazohusika zikirushiana mpira kuhusu suala hilo.
Lakini jana Balozi Kagasheki alisema kabla ya uchaguzi mwaka jana, Baraza la Mawaziri lilikubaliana kuondoa posho ambazo alidai zimekuwa kubwa kuliko bajeti ya mishahara na maendeleo, lakini uamuzi huo haukutakiwa kugusa majeshi.“Fungu la posho limekuwa kubwa linatisha linazidi fungu la mishahara na maendeleo.
Ndio maana Baraza la Mawaziri likamwambia PM (Waziri Mkuu) kwamba kwa hali hii hatuwezi kufika lazima posho zikatwe, lakini uamuzi huo haukutakiwa kuhusisha majeshi yetu,”  alisema Balozi Kagasheki na kuongeza:“PM aliahidi kusimamia hilo mara moja. Lakini pengine naweza kusema watu wa Hazina kwa hasira bila kufanya utafiti wakaamua kufyeka hata posho za polisi.
"Nasema hivyo kwa sababu Hazina ndio wanufaika wakubwa wa posho hizo wanajipangia vikao wenyewe wanavyotaka, posho zinazolipwa zinatisha!”Naibu waziri huyo alisema haingii akilini kwamba posho walizopewa polisi kuanzia Julai mwaka jana, tena kwa kusimamiwa na Rais Jakaya Kikwete, ziondolewe leo bila maelezo yoyote kwa wahusika.“Mimi kama mimi nasema this is unfair (hii sio haki) zirudishwe haraka,” alisema Balozi Kagasheki na kuongeza kuwa, posho hizo zililenga kuwapunguzia makali na kuwaepusha na vishawishi vya kuingia kwenye mitego ya rushwa.
Alisema mishahara na posho za polisi bado ziko chini, ukilinganisha na nchi jirani na kwamba, anasikitika kwa taarifa za kufyekwa posho hizo  kutofikishwa ngazi za juu.Kuhusu suala la polisi kutupiana mpira na Hazina, Balozi Kagasheki alisema sio kweli kwamba, jeshi hilo halina taarifa hizo kwa sababu takribani kwa siku tatu wamekuwa wakikutana na wenzao wa hazina kuhakikisha posho hizo zinarejeshwa haraka tangu makato ya Desemba mwaka jana.
Kwa upande wake Nantanga alisema inasadikiwa kulikuwa na hitilafu katika mfumo wa malipo uliosababisha kurukwa kwa vipengele viwili ambavyo ni posho ya nyumba na posho ya upelelezi.
“Bado hatujafahaumu kilichotokea, lakini sauala hilo linafanyiwa kazi,”alisema Nantanga alipozungumza na Mwananchi kwa simu jana jioni na kuongeza:

“Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Ndani, zimeundwa task force (kikundi kazi) kwa ajili ya kulifanyia kazi tatizo hilo, mambo yatakuwa mazuri muda si mrefu”.

Kwa mujibu wa Nantanga, kikundi kazi hicho kina wajibu wa kufuatilia na kubaini chanzo cha tatizo hilo, kushughulikia mfumo wa malipo kusoma vipengele vyote vya mishahara ya polisi na kuhakisha askari wote waliokatwa fedha zao zinarejeshwa.

Alisema makamanda wa polisi wa mikoa yote nchini tayari wamejulishwa kuhusu matatizo hayo ili waweze kufikisha ujumbe kwa askari polisi zaidi ya 16,000 ambao walikumbwa na tatizo hilo.

Hata hivyo Natanga hakuweza kutaja kiasi cha fedha kilichokatwa kwa makosa kwa maelezo kwamba ilikuwa ni mapema kutokana na kuwepo kwa viwango tofauti vya malipo ya posho kwa polisi husika.

Waziri wa Fedha na Uchumi, Muspha Mkullo akizungumza na gazeti la The Citizen ambalo ni dada na gazeti hili alikiri kuwepo kwa matatizo ya malipo lakini akasema Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye anayepaswa kutoa ufafanuzi.

“Ndiyo kuna tatizo lakini tumekubaliana kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye anayepaswa kuzungumzia suala hilo,”alisema Mkullo.

Taarifa za kukatwa kwa mishahara ya polisi zilianza kusikika katikati ya wiki hii, na juzi baadhi ya polisi walifika Mwananchi kulalamikia suala hilo.
Malalamiko hayo pia yaliripotiwa katika mikoa mingine nchini ikiwemo Dodoma na Ruvuma.

No comments:

Post a Comment