Askari aliyempiga risasi dereva teksi mbaroni
Hatimaye Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, limesema uchunguzi wake wa awali, umebaini kuwa askari mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mwenye namba G.6825 PC Elias Matiku, alihusika katika tukio la kumpiga risasi dereva teksi, Jamal Abdul (32).
Limesema kuwa kutokana na uchunguzi huo, Matiku amewekwa rumande kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi, mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema jana kuwa, kushikiliwa kwa askari huyo, kumetokana na uchunguzi wa awali kwa watu waliohusika na siku ya tukio, kutaja baadhi ya umbo na vitu mbalimbali alivyokuwanavyo askari huyo.
Alisema jeshi lake pia limebaini kuwa ndiye aliyehusika.
“Hivyo tumeamua kumshikilia hadi hapo na watu wengine kama yule mgonjwa (majeruhi) akiweza kuja kumtambua, hatua zaidi za kipolisi zitachukuliwa dhidi yake,” alisema Kamanda Andengenye.
Alisema kuwa siku ya tukio, Januari 16 mwaka huu, majira ya saa 11.00 alfajiri, eneo la Ngarenaro, Dereva mwenye gari namba T. 976 AJZ aina ya Toyota Mark 11, akiwa amepaki eneo la Shiaz Kaloleni, alitokea mtu mmoja, aliyevaa koti kubwa jeusi, na viatu vyeusi na mkononi akiwa na silaha na kuomba kupelekwa kituo cha polisi Ngarenaro.
Alisema koti hilo lilikuwa la kuzuia baridi, lakini silaha aliyokuwa ameshika haikujulikana ya aina gani, hivyo baada ya makubaliano ya kumlipa Sh. 3,000 waliondoka hadi eneo la standi ya mabasi ya Kimotco, ndipo mtu huyo alipompiga risasi mkono wa kulia na kasha kuondoka teksi hiyo.
“Huyu mtu aliondoka na gari hadi kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Suleman Ally Nkya na kumkuta muhudumu aliyejulikana kwa jina la Yasri Mohamedy au kwa jina maarufu Shabani na kuomba kuwekewa mafuta katika gari,” alisema Andengenye.
Alisema kuwa wakati muhudumu huyo akiweka mafuta hayo, ghafla akambadilikia na kupora fedha Sh. 350,000 za sarafu na kukimbia na gari hilo.
“Gari hilo lilipokuwa likikimbia eneo la sheri, liligonga gari namba T.412 BMH aina ya Toyota Hiace na wakaanza kubishana na ndipo mtu huyo alipotelekeza gari hilo na kukimbia,” alisema.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo, ndipo Polisi walipoanza kufanya mahojiano na kituo cha mafuta na kubaini katika maelezo ya awali kuwa askari huyo amehusika.
Hata hivyo alisema kuwa bado wanasubiri na upande wa pili dereva teksi aliyepigwa risasi aende kumtambua askari huyo, na akisema ndiye mwenyewe, basi jeshi litamchukulia hatua zaidi.
Tayari Abdul ameshatoka hospitali na mdogo wake ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema kuwa hali ya dereva huyo inaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment