Kufilisika kisiasa ndio huku kwa Wahafidhina ccm kumwaga sumu na chuki Zakuwagawa Wazanzibar
Written by makame silima // 10/10/2013
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Waziri wa zamani na wafanyakazi wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wametoa wito wakitaka visiwa vya Unguja na Pemba vijitawale. Wastaafu hao ni waliokuwa wanajeshi wastaafu, askari wa vikosi vya SMZ, wafanyakazi wa wizara na idara za mbalimbali za umma.
Katika kongamano lililofanyika siku chache zilizopita kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo eneo la Kikwajuni, walisema ipo haja ya kufanyika ‘mapinduzi ya heshima na adabu’, baada ya yale ya 1964.
Kongamano lilikuwa chini uenyekiti wa Ali Hassan Khamis, ambapo mbali ya wastaafu, pia lilihudhuriwa na wakulima na wafanyakazi wa SMZ.
Miongoni mwa walioshiriki ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Awamu ya Pili Zanzibar), Aboud Talib Aboud. Yeye aliondolewa madarakani pamoja na Rais Aboud Jumbe mwaka 1984, baada ya hali ya kisiasa kuchafuka visiwani humo.
Aboud alisema watu kutoka Oman walifika Zanzibar kama walowezi na kuigeuza ardhi mali yao hadi yalipofanyika Mapinduzi yaliyorejesha hadhi, utu na ukombozi wa wananchi wanyonge 1964.
“Jueni kwamba Zanzibar haitatawaliwa tena na wageni. Wanaosema ‘Zanzibar kwanza’, nawaeleza kuwa ni ‘wananchi kwanza’ na Mapinduzi ndio yaliyowakomboa Waafrika wanyonge, hatutakubali ng’o kuwa chini ya ukoloni mamboleo,” alisema Aboud.
Mbunge wa zamani wa Kikwajuni, Parmuk Hogan Sing, aliipoda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar akidai haikutokana na ridhaa ya Wazanzibari wengi na kudai wameingizwa viongozi wapinga sera za umoja, Mapinduzi na Muungano, hivyo inakosa uzani wa uhalali na kuaminiwa.
Mshiriki wa kongamano hilo, Ali Machano Khamis, alisema matatizo yanayokikumba kisiwa cha Unguja ni kitendo cha kuchaguliwa wagombea urais ambao si chaguo la Wazanzibari.
Alisema wagombea hao wasiofaa ndio chanzo na kiini cha kuanza kulegelega kwa utetezi wa misingi ya Mapinduzi, na kuwataka wazee kuanza kujirekebisha kuhakikisha wanaoteuliwa lazima wawe na uchungu wa nchi, si wasaka maslahi binafsi.
Akizungumzia mchakato wa kuundwa SUK, Suleiman Omar Suleiman, alisema ulifanyika kibabe na kwa hila bila kuwaweka vituoni mawakala wa kusimamaia kura za maoni kujua idadi ya waliosema “hapana” na “ndiyo”.
Alisema hakuna kigezo halisi cha kuwapo Muungano wa visiwa vya Unguja na Pemba tangu asili na jadi, na kwamba muda umefika sasa kwa visiwa hivyo kujigawa, kila upande uwe na mamlaka yake kamili.
“Ni vipi Pemba iwe ya Wapemba, Unguja iwe ya wote? Viwanja vya Unguja wamepewa Wapemba wakati Pemba hakuna Muunguja anayeishi na kujenga nyumba. Jamani, Waunguja tumechoka! Tunataka mamlaka yetu haraka,” alisema Suleiman.
Kuibuka kwa madai hayo wakati huu huenda kukaiweka Serikali ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein katika taharuki na kuitikisika SUK iliyopatikana baada ya mazungumzo kusaka muafaka, na kubadilishwa kifungu cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, hivyo kufanyika kwa kura za maoni ambapo asilimia 66 ya Wazanzibari waliikubali SUK.
Khamis Mwinyishehe Suleimna alisema Pemba haikushiriki katika harakati za Mapinduzi ya Zanzibar na hata walipotakiwa na Waingereza wakapigane Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939 hadi 1945), walikataa kwa madai kuwa wao walikuwa chini ya Wareno.
Alisema kati ya waasisi 14 wa Mapinduzi hakuna hata mmoja kutoka Kisiwa cha Pemba, hivyo suala la visiwa hivyo kujitenga halihitaji mapatano wala mazungumzo ya suluhu mezani.
Mzee Younus Haji alisema jambo hatari lililofanyika katika uundwaji wa SUK ni kuingizwa viongozi wenye itikadi za vyama vya zamani vya Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP), na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kufanya tathmini kuhusu Serikali hiyo na kutafuta Katiba mpya ya Zanzibar.
Wastaafu wengi waliozungumza walionekana kusikitishwa na kuvunjwa kwa miiko ya Mapinduzi ya Zanzibar wakisema waliomrithi Rais Abeid Amani Karume, walipuuzia wosia ulioachwa na viongozi wa Afro Shiraz Party (ASP) na waasisi wake.
“Kama watu hawa wangependa umoja na maridhiano tangu awali hata Mapinduzi ya mwaka 1964 yasingetokea, kwani kiongozi wa ZPPP, Mohamed Shamte Hamad, angeunganisha viti vyake vitatu na ASP basi,” alisema Mzee Kheir.
Madai yao mengine ni kwamba wazee wa Pemba wamewahi kwenda hadi Ofisi za Umoja wa Mataifa Dar es Salaam mwaka 2000 wakitaka wapewe mamlaka, na kwamba ni heri wakapewa sasa kuepusha shari.
Ahmed Khamis Mcheju alisema kitendo chochote cha kuyapuuza Mapinduzi ya Zanzibar hakivumiliki kwa Waafrika waliobaguliwa na kudharauliwa tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa Kiafrika, Mwinyimkuu, na Waarabu kutoka Oman mwaka 1804.
Madai hayo mazito ni kama ishara ya kutimia kwa utabiri Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema nje ya Muungano kutajitokeza Uzanzibari na Uzanzibara, kisha Uunguja na Upemba na Taifa halitabaki salama.
No comments:
Post a Comment