Friday, 11 October 2013

Kwa Watanganyika ,Uwe Muhindi ,Uwe Buda,Uwe Patri ,Mbele ya Kuibinya Zanzibar hua kitu kimoja ,(Issa Shivj na Utanganyika wake)

                                                                                                                                                                                                        Mkataba wa Mafuta Zanzibar
Shivji amvaa Dk. Shein
Mwandishi Wetu
Toleo la 319
9 Oct 2013
..
Profesa Issa Shivji
MAKUBALIANO ya mkataba wa awali (MoU), uliosainiwa hivi karibuni baina ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein, na kampuni ya kimataifa ya mafuta ya Shell unaohusu utafutaji na hatimaye uchimbaji wa mafuta, umeelezwa kuwa ni mkataba ‘feki’ na usiokuwa na uhalali wowote kisheria.
Magwiji wa sheria na mikataba nchini, Profesa Issa Shivji na Dk Rugemeleza Nshala, kwa nyakati tofauti, wameliambia gazeti hili kuwa hicho kinachodaiwa kusainiwa na Dk Shein na kampuni hiyo ya Shell, hakipo kisheria kwa maelezo kwamba mafuta na gesi asilia ni mambo yaliyo chini ya Muungano, na kwa hiyo mwenye mamlaka ya kusaini mkataba wa aina hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, ni waziri mwenye dhamana kuhusu masuala ya nishati.
Katika toleo la wiki iliyopita, gazeti hili lilibeba habari kuu iliyokuwa ikielezea namna Dk Shein alivyoingia makubaliano ya awali (MoU) na kampuni kubwa ya kimataifa inayojishughulisha na biashara ya nishati ya mafuta na gesi asilia, Shell, wakati akiwa katika ziara yake ya kiserikali nchini Uholanzi, Agosti mwaka huu.
Katika mkataba huo wa makubaliano ya awali, SMZ imeipatia kampuni hiyo ya Shell idhini ya kutafiti na hatimaye kuchimba mafuta katika vitalu vinne, vilivyopo Zanzibar, vilivyopewa majina ya Block 9,10,11 na 12.
Akizungumzia hatua hiyo wiki iliyopita akiwa mjini Kilwa Masoko kwa ajili ya kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya mafuta na gesi kwa wanahabari nchini, yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Profesa Shivji, alisema Dk Shein hana mamlaka yoyote hadi sasa ya kisheria kusaini mkataba wowote unaohusiana na masuala ya mafuta na gesi ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Alisema mafuta na gesi ni mambo ya Muungano, na kwa hiyo mamlaka pekee yenye uhalali wa kisheria kusaini mkataba wowote unaohusiana na jambo hilo, ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Aidha, Profesa Shivji aliwataka Watanzania kuwapuuza wote wanaodai kwamba masuala ya mafuta na gesi asilia viliingizwa kinyemela katika mambo yote ya Muungano, akisisitiza kwamba maliasili hiyo iliongezwa kwenye mambo ya Muungano mwaka 1968 wakati wa utawala wa Mzee Abeid Amani Karume.
“Masuala ya mafuta na gesi yaliongezwa kwenye mambo ya Muungano na Mzee Karume mwenyewe mwaka 1968. Zitafuteni Hansard (taarifa mazungumzo yaliyofanyika ndani ya Bunge), zipo. Hao wanaopiga propaganda kwamba mambo hayo yaliingizwa kinyemela kwenye mambo ya Muungano ni watu wa kupuuzwa,” alisema Profesa Shivji.
Dk Rugemeleza Nshala Kwa upande wake, Dk Nshala alisema kwa kusaini makubaliano hayo, si tu kwamba Dk Shein amevunja Katiba, bali hata kampuni yenyewe ya Shell iliyosaini mkataba huo, imesaini mkataba kanyaboya (feki) kutokana na kile alichosema kampuni hiyo imeingia makubaliano na mtu asiyehusika kwa mujibu wa sheria ya sasa ya madini, mafuta na gesi.
“Mwenye mamlaka ya kisheria kusaini mkataba wowote unaohusu nishati na madini, kwa mujibu wa Katiba yetu, kwa niaba ya Serikali yetu, ni Waziri wa Nishati na Madini. Suala la mafuta na gesi asilia viko chini ya Muungano, Dk Shein hana uhalali wowote wa kusaini mkataba wa mafuta, gesi wala madini…unajua kuna watu wanataka kutumia kipindi hiki ambacho tuko kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya kuvuruga Muungano,” anasema Dk Nshala ambaye amebobea katika masuala ya mikataba ya madini, mafuta na gesi.
Raia Mwema linafahamu kwamba ingawa MoU inaonyesha kwamba walioingia makubaliano ni Shein na Mtendaji Mkuu wa Shell, Peter Voser, aliyesaini mkataba huo kwa niaba ya Shein ni Waziri wa Nishati wa SMZ, Ramadhan Abdallah Shaaban.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba na maelezo ya Prof. Shivji na Dk. Nshalla, aliyepaswa kusaini makubaliano kama hayo kwa sasa ni Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo
..- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/shivji-amvaa-dk-shein#sthash.sbSMMaJU.dpuf
Chanzo Raia Mwema

No comments:

Post a Comment