Thursday, 10 October 2013

Hotuba ya Maalim Seif alipozindua Nyumba Salama kwa waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD
KATIKA UZINDUZI WA NYUMBA SALAMA KWA WAATHIRIKA WA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE ZANZIBAR HUKO OCEAN VIEW RESORT ZANZIBAR TAREHE 9 OKTOBA, 2013
Mheshimiwa Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto,
Waheshimiwa MawazirI,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Mheshimiwa Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi, Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya Tanzania,
Viongozi wa Shirika la ActionAid,
Waheshimiwa waalikwa nyote Mabibi na Mabwana,
Asslam Alaykum
Awali ya yote sina budi kuelekeza shukurani zangu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai, uzima na wenye afya njema na kuweza kukutana hapa leo kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Vile vile nitowe shukurani zangu za dhati kwa Jumuiya ya Ulaya pamoja na washirika wake Shirika la ActionAid kwa kuandaa mradi wa kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake wa Zanzibar.
Aidha niwashukuru kwa kuona haja ya kunialika mimi kuja kujumuika nanyi katika shughuli hii ya Uzinduzi wa nyumba salama kwa akina mama waliopata athari za vitendo vya ukatili.
Najisikia faraja sana leo kuona kwamba nilipata fursa ya kuzindua mradi huu wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto mwezi Machi mwaka jana. Nilielezwa wakati wa uzinduzi wa mradi huu kwamba moja wapo ya malengo ya mradi huu ni uanzwishaji wa nyumba salama kwa watu walioathirika kwa vitendo vya ukatili.

Nifaraja kwangu kuona leo hii nipo tena katika ukumbi huu kusikia muendelezo wa mradi pamoja na kuzindua nyumba salama kwa akina mama hao waliopata athari za vitendo vya ukatili na udhalilishaji. Nasema kwangu mimi binafsi hii naona ni heshima kubwa mliyonipa.
Waheshimiwa viongozi na waalikwa
ActionAid ni Shirika la Kimataifa ambalo limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umasikini, utetezi wa haki na kupiga vita vitendo vya ukandamizaji na uvunjifu wa sheria. Shirika hili kwa hakika linatoa mchango mkubwa na wa kipekee katika kukuza maendeleo ya watu wote Tanzania, ikiwemo Zanzibar. Kuanzishwa kwa nyumba salama ambayo ni muendelezo wa hatua ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake Zanzibar itasaidia sana katika kulinda haki za akina mama na hivyo kutoa fursa ya kujenga jamii nzima ya Wazanzibari iliyo na uadilifu.
Lakini vile vile hatua hii ni muhimu katika kusaidia juhudi za serikali yetu hasa katika kazi muhimu inayoendelea ya kupiga vita aina zote za ukatili na udhalilishwaji wanawake na watoto.
Waheshimiwa viongozi na waalikwa
Vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni miongoni mwa matukio mabaya yanayoendelea kujitokeza katika jamii mbali mbali duniani na kusababisha madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na uhai wa binaadamu. Matukio ya aina hiyo tunayashuhudia yakiongezeka pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa katika ngazi za kitaifa na kimataifa kuyatokomeza.
Kimataifa takwimu zinaonesha mwanamke mmoja kati ya watatu amekumbana na vitendo vya ukatili, iwe wa aina moja au nyengine, hali ambayo inasababisha madhara makubwa, sio tu kwa wanawake waliohusika kufanyiwa vitendo hivyo, bali kwa watoto katika familia ambao hushuhudia vitendo hivyo.
Miongoni mwa madhara makubwa yatokanayo na ukatili dhidi ya wanawake ni kukosekana usawa katika jamii, athari za kisaikolojia, kurejesha nyuma maendeleo pamoja na kuchangia kukosekana hali ya amani.
Ukatili wa kijinsia ukiwemo ule unaolengwa wanawake hivi sasa ni uvunjifu wa haki za kibinaadamu.  Jumuiya ya Kimataifa inalazimika kupitisha maazimio na mikakati mbali mbali kwa nia ya kutokomeza kabisa matendo hayo. Miongoni mwa maazimio hayo ni lile la kupiga vita aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake la mwaka 1993, ambalo limeweka bayana vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa aina hiyo.
Aidha, azimio maarufu la Beijing mwaka 1995 ambalo limeweza kutoa mwamko mkubwa kwa mataifa katika vita dhidi ya ukatili kwa wanawake, pia limesaidia sana mataifa mbali mbali kuweka mikakati na malengo ya utekelezaji katika kuinua hali za wanawake, iwe katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, na vile vile limesaidia kuibua harakati za kuelimisha jamii umuhimu wa kukomeshwa ukatili dhdi ya wanawake na kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma maendeleo yao.
Tanzania inaunga mkono kwa dhati hatua za kupiga vita aina zote za ukandamizaji, ukatili na ubaguzi wa kijinsia, ikiwemo dhidi ya wanawake na watoto na imetia saini makubaliano na itifaki mbali mbali zinazohusu mambo hayo na sasa inazitekeleza.
Waheshimiwa viongozi na waalikwa
Hapa kwetu Zanzibar, Serikali imeweka mikakati mbalimbali katika kushughulikia tatizo hili ikiwemo Kamati ya Mawaziri iliyoanzishwa na Mheshimiwa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, kwa ajili ya kuchunguza ukubwa wa tatizo hili, lakini pia jukwaa ambalo litajadili changamoto zilizopo katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.
Pia uanzishwaji wa Kamati za Makatibu Wakuu ambao hukutana kujadili na kupeana miongozo juu ya utatuzi wa jambo hili. Serikali pia imeanzisha kamati mbali mbali za kitaifa, wilaya na hata vijiji, ili kupambana na kadhia hii. Kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa mkono na dawati la wanawake na watoto pia ni miongoni mwa jitihada za serikali za kupambana na matatizo yanayo wakabili akina mama na watoto.
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba pamoja na mataifa, ikiwemo nchi yetu kuchukua hatua tofauti kukomesha ukatili dhidi ya wanawake, bado safari ndefu ipo mbele yetu, kwasababu matukio hayo bado yanaendelea kujitokeza kwa wingi.
Sababu zinazoelezwa kuchangia ukatili dhidi ya wanawake ni nyingi na zinatafautiana kutokana na mazingira au jamii moja hadi nyengine, miongoni mwa hizo ni mifumo kandamizi ya kimaisha ambayo imeota mizizi katika jamii zetu na kuonekana kama ndio utaratibu wa maisha.
Kutokana na hali hiyo, ili tuweze kuing’oa mifumo ya aina hiyo na kuleta usawa miongoni mwa jamii pamoja na kukomesha kabisa ukatili dhidi ya wanawake, sote tunahitajika tushiriki katika vita hivi, kuanzia serikali, jumuiya zisizokuwa za kiserikali kama hii ActionAid na nyenginezo, lakini pia jamii nzima.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa        
Kwa masikitiko makubwa jamii ya Wazanzibari ni miongoni mwa zinazokabiliwa na aibu hii ya ukatili dhidi ya wanawake pamoja na watoto. Tafiti chache zilizofanyika katika baadhi tu ya maeneo zinadhihirisha ukubwa wa tatizo hilo, hali ambayo inatulazimisha tusimame kidete kukabilina na vitendo hivyo, ili wanawake nao waishi kwa amani bila ya bughudha kutoka kwa watu wengine na waweze kuchangia kikamilifu kukuza maisha yao na taifa lao.
Miongoni mwa sababu zinazoelezwa kuchangia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake Zanzibar ni kuwepo mitazamo potofu juu ya wanawake, ukimya miongoni mwa wanawake wenyewe na jamii inayowazunguka, kuona aibu na muhali kwa wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo na hivyo kushindwa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.
Matokeo ya hali hiyo ni matukio mengi ya udhalilishwaji wanawake kutoonekana kuwa ni makosa ya jinai, na badala yake jamii inayaona kama ni masuala ya kifamilia na hivyo kuyamaliza nje ya taratibu za kisheria ambapo haki za waliodhulumiwa hazizingatiwi.
Kwa upande mwengine kupungua kwa imani ya wananchi kwamba wanaweza kupata haki katika mifumo rasmi, kama vile Polisi na Mahakama kutokana na hali ya ucheleweshwaji wa kesi, ada za mahakama, gharama za usafiri kufuatilia kesi, pamoja na kuwepo vitendo vya rushwa, ambapo hata wale wanaotiwa hatiani ni wachache, hakuzuwii wahalifu kushawishika kuachana na matendo kama hayo.
Waheshimiwa viongozi na waalikwa
Kukosekana kwa mahali salama ambapo watu walioathirika watapatiwa huduma mbali mbali, ikiwemo za ushauri nasaha, kunalazimisha watu hao kukata tamaa na kwamba muendelezo wa kesi zao siku zote unakuwa ni wa vikwazo na mwisho haki haipatikani.  Kutokana na hali hii, mapatano ya kinyumbani ndio mara nyingi yanayotumika ambayo kamwe hayawezi kulimaliza tatizo.
Matukio ya wanawake kupigwa na waume zao na mara nyengine hata kujeruhiwa, vile vile yanaripotiwa siku hadi siku ndani ya jamii yetu ya Wazanzibari. Bila shaka tabia ya kuacha na kudharau maadili yetu mema ina sehemu katika kukithiri kwa ukatili na udhalilishaji wanawake.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa 
Ukatili dhidi ya Wanawake wenye Ulemavu ni mkubwa zaidi na unaoonesha sura mbaya zaidi ya kutojali utu na ubinaadamu katika jamii zetu. Tabia ya Wanawake wenye Ulemavu hasa wa akili kubebeshwa ujauzito mara kwa mara, kupigwa na kufanyishwa kazi nzito na aina mbali mbali za udhalilishaji, unaonesha jinsi jamii isivyo wajali wenzetu hao.
Aidha, katika siku za hivi karibuni, kumeripotiwa matukio ya  kuuwawa kwa wanawake na watendaji wa hayo ni waume zao. Huo ni unyama wa hali ya juu na ya kutisha, hatuna budi kuupiga vita kwa nguvu zote.
Kwa mara nyengine tena nazipongeza jitihada za wadau mbali mbali wakiwemo Actionaid na washirika wake katika kubuni mbinu zitakazosaidia kumaliza kabisa vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa
Nazihimiza kwa nguvu kubwa taasisi nyengine za Serikali na za binafsi, kutoa mashirikiano ya hali na mali katika uendelezaji wa nyumba salama. Aidha serikali kwa kupitia wizara husika  itakuwa na jukumu la kuhakikisha uendelevu wa program nzima ya nyumba salama zikiwemo upatikanaji wa huduma za kiushauri kwa watu waliopata athari kutokana na vitendo hivyo, kuangalia usalama wa wanawake wakiwepo ndani ya nyumba salama, uharakishaji wa kesi zinazohusiana na matendo ya ukatili kwa wanawake na watoto. Serikali pia itashirikiana na Actionaid na wadau wengine katika kutafuta ufadhili wa uendelezaji wa nyumba salama.

Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa
Ni imani yangu kubwa pia kwamba, Jumuiya ya Ulaya ambao ndio wafadhili wakubwa wa jitihada hizi, hawatatuacha mkono katika kuendeleza jitihada hizo.
Kwa upande wake serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali kukomesha aina zote za ukatili dhidi ya Wanawake, pamoja na watoto wetu, kwa kuweka sheria mpya na kuzirekebisha zile ambazo zitaonekana hazikidhi haja kutokana na wakati uliopo.
Vile vile tutawapa nguvu kubwa wanawake katika masuala ya kiuchumi na kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kuzipa msukumo wa kipekee jumuiya na taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazojitokeza kukomesha matendo maovu dhidi ya wanawake na watoto, na kujenga mazingira ya kukuza maendeleo yao.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa
Baada ya kusema hayo niruhusuni tena nitoe shukurani zangu kwenu nyote kwa kunisikiliza na kuwa watulivu katika muda wote nilipokuwa nikizungumza.
Na sasa kwa heshima na taadhima nachukua fursa hii kutamka rasmi kwamba, NYUMBA SALAMA KWA WATU WALIOATHIRIKA KWA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE ZANZIBAR, nimeizindua rasmi.
Ahsanteni.

No comments:

Post a Comment